Advertisements

Monday, January 21, 2013

RC Mwananzila alazwa Muhimbili

Robert Manumba
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

Akizungumza na NIPASHE jana mmoja wa wanafamilia ambaye alipokea simu ya Mkuu huyo wa mkoa alisema Mwananzila amelazwa hospitalini hapo tangu Jumatano ya wiki iliyopita.
Alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda amemtembela jana kumjulia hali na kwamba hata hivyo anaendelea vizuri na madaktari wamekuwa karibu naye kumtibu.

Naye Ofisa habari wa Muhimbili, Aminael Aligaesha, alisema Mkuu wa Mkoa wa Lindi hali yake inaendelea vizuri ukilinganisha na siku alipopelekwa hospitalini hapo.

Wakati huo huo, Hospitali ya Aga Khani inatarajia kutoa taarifa kwa umma leo kuhusu maendeleo ya afya ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba ambaye amelazwa katika hospitali hiyo kwa matibabu.Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk. Jaffer Dharsee, alisema Manumba bado anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo na kwamba leo (Jumatatu) atatoa taarifa rasmi kwa waandishi wa habari.

Hata hivyo, vyanzo vya habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi vimeeleza kuwa hali ya Manumba siyo ya kuridhisha kwani bado yupo chumba cha uangalizi maalum (ICU) akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo.

Manumba alifikishwa katika hospitali hiyo akitokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kuugua ghafla na baada ya kufanyiwa vipimo ilibainika kuwa alikuwa na wadudu wengi wa malaria.
CHANZO: NIPASHE

No comments: