Marafiki waaminifu wachache, hubaki na rafiki aliyepatwa na majanga. Hata hivyo, nao wanaweza kukimbia pale ambapo matatizo yanazidi. Marehemu Juma Issa Kilowoko ‘Sajuki’ na Wastara Juma Issa, hawakutupana, walishikamana mpaka kifo kimewatenganisha.
Kama Sajuki alivyofumba macho, akasisitiza Wastara ndiye mke wake pamoja na ulemavu aliopata mrembo huyo wakati wanakaribia kufunga ndoa, vivyo hivyo, Wastara naye akamshikilia mume wake alipoandamwa na maradhi mpaka kifo kilipomchukua.
Mimi najua ni kiasi gani Wastara alihangaika kutafuta fedha za matibabu kwa ajili ya mume wake. Mapito waliyopita pamoja wengi yamewashinda. Tamaa za kibinadamu na matarajio ya muda mfupi, vikawafanya waachane wakati ambao mmoja anakuwa anahitaji msaada wa mwenzake.
Unamuacha mwenzi wako kisa anaumwa, auguzwe na nani? Ukichunguza kwa makini utaona kwamba kufanya hivyo siyo tu usaliti, bali ni ukatili wa kiwango kikubwa. Unaweza kumsababishia akafa kwa kihoro katika kipindi ambacho hakukitarajia.
Mpenzi wako amepata matatizo, yupo jela. Badala ya wewe kuonesha uaminifu wako ukawa unakwenda kumjulia hali na kumfariji amalize kifungo chake au aione mahabusu ni rahisi, huku ukimsaidia namna ya kushinda kesi, unamtelekeza bila huruma.
Utamu wa dunia kwa upande mmoja na majanga katika sehemu nyingine, ni kichocheo cha mapenzi kutetereka au kufa kabisa. Mwanamke anajionea jinsi ambavyo mwenzi wake anavyosota, hana fedha lakini mtaa wa tatu kuna mwanaume mwenye fedha zake anamtaka.
Mke anaumwa, mume anakutana na wanawake wa kila aina. Wengine ni rahisi kiasi kwamba hawangoji kutongozwa, wao wenyewe wanakuwa wa kwanza kurusha ndoano. Mwanaume anapovuka vishawishi hivyo na kuendelea kushikamana na mkewe, anakuwa ametimiza maana halisi ya mapenzi.
Sajuki na Wastara wanapata alama nyingi zaidi kwa sababu ya kigezo cha umri. Wamepata mitihani wakati ambao ni vijana wadogo, wazuri, maarufu na kadhalika. Walikuwa na sifa nyingi ambazo zingeweza kuwafanya washawishike kusalitiana.
Jumlisha na kawaida ya walimwengu kusemana. Ukioa au kuolewa watasubiri ndoa ivunjike ndiyo wakae pembeni wakucheke. Badala ya kukushauri au kukusaidia ndoa yako idumu, wao wanakuwa kama fisi anayesubiri mkono wa binadamu uanguke.
Hata ukipata kazi wao watasubiri ufukuzwe, ukianza biashara watangoja ianguke, ukipata cheo watatamani mambo yaharibike ili mradi wapate la kusema. Maneno yasiyo na msingi hayakuwa na nafasi ndani ya vichwa vya Wastara na Sajuki.
Hawakuvunjwa moyo wala kukatishwa tamaa na misukosuko iliyowakuta. Wakawa na mioyo ya chuma, wakasonga mbele bila kurudi nyuma. Ona sasa, leo tunaweza kuandika makala, kupongeza na kuwatumia kama mfano wa mapenzi ya kweli.
Kuna wale waliokuwa wepesi kuzusha. Ndani ya uhusiano wa Wastara na Sajuki, yakaibuliwa mambo ambayo kama si imani ya kila mmoja kwa mwenzake, basi wangeweza kukimbiana mapema. Hata uchawi ukanenwa.
Wapo waliothubutu kusema kwamba ili Sajuki apone ni sharti amwache Wastara. Binadamu wana mengi sana. Wao wakafumba macho, wakaweka pamba masikioni, wakayakabili yanayowahusu, ya walimwengu wakayaacha kwa ulimwengu.
Kama Winnie Mandela alimvuruga mzee Nelson Mandela, kwa nini usione kama Wastara ni mwanamke wa kipekee? Ikiwa mke wa Ayubu alichoshwa na mitihani ya mumewe alipopatwa na maradhi ya kila aina, mpaka akamkufuru Mungu kwa maneno, kwa nini usimsifu Wastara alipomvumilia Sajuki?
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
1 comment:
Waaaaaaaaooooooo,hili ni mfano wa kuigwa katika maisha yetu. R.I.P Sajuki na dada Wastara nakutakia kila l heri katika maisha yako,Mungu akubariki sana,aendelee kukupa huo moyo wa upendo,huruma,uadilifu na uvumilifu.
Post a Comment