Na Salma Said, ZNZ
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuimarisha huduma za zima moto na uokozi katika maeneo yote ya Unguja na Pemba kwa lengo la kukabiliana na majanga mbali mbaliya moto yanayotokea.Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Dk Mwinyihaji Makame ametoa ahadi hiyo wakati akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa jimbo la Chaani (CCM) Ussi Jecha Simai aliyetaka kujuwa mikakati ya kuimarisha huduma za zima moto na uokozi ikiwemo hasa vijijini zimefikiya wapi hadi sasa tokea serikali kutoa ahadi ya kuimarisha huduma hiyo.
Dk Mwinyihaji aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba hadi sasa jumla ya vituo vipya vitatu vimejengwa Unguja na Pemba ikiwemo katika bandari ya Mkoani Pemba kwa ajili ya kupambana na matukio ya moto.
Alisema tayari gari saba za kuzima moto zimenunuliwa na serikali ya mapinduzi ya zanzibar kwa ajili ya kukabiliana na matukio ya zima moto ambayo hivi sasa yamekuwa mengi siku hadi siku yanayotokea hapa nchini.Waziri huyo alisema serikali imefanikiwa kununua magari mapya na wanategemea kwamba watakuwa wamepunguza tatizo hilo loa ukosefu wa gari hizo za zima moto ambazo zilikuwa zikihitajiwa katika matukio mbali mbali ya kukabiliana na majanga ya moto ambayo yanaonekana kukithiri siku hadi siku kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo yale ya umeme.
Aidha Dk Mwinyihaji alisema mipango ya baadaye ni kujenga kituo cha kukabiliana na majanga ya moto huko Marumbi wilaya ya kati Unguja ambapo tayari eneo la kazi ya ujenzi wa kituo hicho kimepatikana.
”Waheshimiwa wajumbe tayari tumepata eneo la kujenga kituo kipya cha kukabiliana na majanga ya moto huko Marumbi wilaya ya kati Unguja ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha huduma hizo vijijini kwa hivyo hiyo ni hatua moja nzuri” aliwaahidi wajumbe wa baraa hilo.
Serikali kufanya uhakiki wa watumishi hewa tumishi wa vikosi vya ulinzi smz kuhakikiwa...
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukabiliana na wimbi la wafanyakazi hewa imekusudia kufanya uhakiki kwa baadhi ya taasisi zake za ulinzi kujuwa idadi kamili ya watumishi wake.
Hali hiyo imekuja kufuatia matukio ya ubadhirifu wa fedha na kukabiliana na tatizo la kulipa mishahara kwa watumishi hewa.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haji Omar Kheri wakati akijibu swali la mwakilishi wa jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujuwa serikali imekabiliana vipi na tatizo la mishahara hewa kwa kikosi cha KMKM.
Katika suali lake Jaku alisema kwamba katika kikosi cha KMKM serikali inalipa watumishi hewa waliostaafu zaidi ya shilingi millioni 18 kwa mwezi jambo ambalo linaipa serikali wakati mgumu wa kutoa mishahara isivyo stahiki.
Akijibu swali hilo Waziri Kheri alikiri kuwepo kwa ubadhirifu huo ambao umegunduliwa kutokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali na ambapo kwa sasa tukio hilo linafanyiwa kazi na wahusika.
”Waheshimiwa tumepokea taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kuhusu upotevu mkubwa wa fedha za umma katika kikosi cha KMKM ambao hulipwa wastaafu hewa....hatuna wasiwasi na taarifa ya mkaguzi lakini ripoti hiyo hivi saa inafanyiwa kazi” alisema Waziri huyo.
Aidha alisema ni marufuku kwa watumishi wa umma kulipwa fedha wakati wanapostaafu utumishi wa umma serikalini na kitendo hicho ni kinyume na sheria za utumishi wa serikali na kuwataka watu ambao wanawatambua wenye kufanya ubadhirifu huo waripoti katika vyombo vya sheria.
Akijibu swali la nyongeza la mwakilishi wa jimbo la Chake Chake (CUF) Omar Ali Shehe aliyesema kwamba zipo taarifa katika kikosi cha Mafunzo tatizo kama hilo lipo la kulipa watumishi hewa mishahara na hivyo kupoteza fedha nyingi za serikali.
Kheri alisema serikali itafanya ukaguzi wa taasisi zake ikiwemo vikosi maalumu vya serikali ya mapinduzi ya zanzibar kujuwa ukubwa wa tatizo hilo na hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wanaokwenda kinyume na sheria za utumishi. Zitachukuliwa.
“Waheshimiwa wajumbe suala hili tumelipokea na tutalifanyia kazi kuchunguza kama kuna ubadhirifu unaofanywa na iwapo watagundulikana wenye kufanya vitendo hivyo basi watachukuliwa sheria za kinidhamu na kisheria” aliahidi waziri huyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali katika ripoti yake ya mwaka jana, alisema na kukitaja kikosi cha KMKM kwa mwezi kinapoteza jumla ya shilingi millioni 18 kulipa mishahara kwa watumishi hewa ambao wengi wao ni wastaafu na marehemu.
Serikali inatafakari uwekezaji kiwanda cha saruji
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inafanya uchambuzi yakinifu kuweza kujuwa kama upo uwezekano wa kuwekeza kiwanda cha saruji nchini.Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshungulikia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar Omar Yussuf Mzee aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi wakati wa kipindi cha masuali na majibu ndani ya ukumbi wa baraza la wawakilishi linaloendelea Chukwani Mjini Unguja.
Akijibu suali la la Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani (CUF) Hijja Hassan Hija aliyetaka kujuwa kwa nini wawekezaji wanaotaka kuwekeza kiwanda cha saruji wamezuiliwa kuwekeza hapa Zanzibar wakati hakuna sababu za msingi za kuwazuwia.
Mzee alisema mradi wa ujenzi wa kiwanda cha saruji ni mkubwa ambao unahitaji kufanyika kwa utafiti mbali mbali ikiwemo uharibifu wa mazingira zaidi ambapo Zanzibar ni kisiwa.
Mzee alisema hakuna tatizo kwa kuwekeza Zanzibar lakini kabla ya kuwekeza ni muhimu kutazama na kufikiria athari ambazo zinaweza kujitokeza katika uwekezaji huo ambao unalalamikiwa na wawekezaji wenyewe.
”Ni kweli tumeupokea mradi wa ujenzi wa kiwanda cha saruji muda mrefu lakini kwanza tunafanya uchambuzi yakinifu ili kujuwa uhalali wa mradi huo lakini pamoja na kuzingatia suala zima la mazingira kwani hatuwezi kukubali kila mradi unaotaka kuwekezwa tu lakini kwanza tuwe na uhakika wa kutunza mazingira yetu' aliwaambia wajumbe hao.
Mzee alisema serikali kwanza inataka kujiridhisha kujuwa muwekezaji atakayejenga kiwanda cha saruji wapi atapata malighafi yatakayoweza kutumika katika uwekzaji wake lakini uchimbaji wa jasi utafanyika katika maeneo gani.
Lakini pia serikali inataka kupata taarifa za kina za kimazingira kuhusu mradi huo ikiwemo kutokuwepo kwa maingiliana ya maji safi na salama katika vyanzo vyake katika eneo ambalo linataka kuwekezwa kiwanda hicho.
Waziri Mzee alisema jiografia ya Zanzibar ni kisiwa ambapo kunahitajika umakini sana katika suala zima la kulinda mazingira yake ili kuepuka uharibifu wa aina yoyote pamoja na kuwa kuzingatia hali halisi ya visiwa zilivyo ambapo nafasi yake huwa ni ndogo kulinganisha na nchi zisizo za visiwa.
Alisema wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza lakini jambo la msingi ni kuzingatia uhalisia wa miradi inayohitaji kuwekezwa ili kusije kutokea madhara kwa nchi na wananchi wenyewe.
Waziri alisema haiwezekani kukubali miradi ambayo itaweza kuleta madhara kwa nchi au wananchi na hivyo wataalamu baada ya kufanya utafiti watawasilisha ripoti serikalini na ndipo serikalli inaweza kuwa na jibu juu ya mradi huo wa kiwanda cha saruji.
Suali la muwekezaji wa kiwanda cha saruji limekuwa likijirudia kila mara katika vikao vya baraza la wawakilishi kutokana na kuwa serikali imekuwa ikishindwa kutoa jibu la muwekezaji huo mzalendo ambaye kwa zaidi ya miaka 10 sasa amekuwa akitaka kuwekeza kiwanda hicho hapa Zanzibar.
Wawakilishi wapitisha mswada wa kuanzishwa kwa shirika la meli...
Wajumbe wa baraza la wawakilishi jana wamepitisha kwa sauti moja mswada wa kuanzishwa kwa shirika la meli litakalotoa huduma bora za kisasa zenye ushindani nchini Tanzania.Waziri wa mawasiliano na miundo mbinu Rashid Seif Suleiman aliwaambiya wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mikataba ya kununuwa meli itakayotoa huduma kwa abiria wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Waziri huyo alisema serikali bado inahitaji kuwa na shirika la meli litakalotoa huduma za kusafirisha abiria pamoja na usalama wao ili kuepuka ajali mbali mbali ambazo zimesababisha vifo vya wananchi wengi mara mbili katika miaka ya hivi karibuni.
”Waheshimiwa wajumbe wa baraza la wawakilishi mswada wa kuanzisha kwa shirika la meli lengo lake kutoa huduma bora kwa wananchi wa mwambao wa pwani ya visiwa vya Unguja na Pemba ambao wanaishi na kuzungukwa na bahari, na kama mnavyofahamu suala la usafiri ni muhimu sana kwa kuwa nchi yetu imezungukwa na bahari' alisema waziri huyo.
Awali wajumbe wa baraza la wawakilishi waliochangia mswada huo waliitaka serikali kulivunja shirika la meli liliopo sasa ambalo limeshindwa kufanya akzi kwa ufanisi na halina sifa ya kufanya kazi kwa ushindani wa kutoa huduma bora nchini.
Akichangia mswada huo, mwakilishi wa kuteuliwa na rais ambaye ni mwenyekiti wa bodi la shirika la meli Ali Mzee Ali alisema shirika linatakiwa kukaguliwa upya na kusafishwa ikiwemo kustaafishwa wafanyakazi wake ambao ni wengi, jambo ambalo linaongeza hasara kwa serikali.
”Mheshimiwa Spika shirika la meli nalifahamu sana kwa sababu mimi ni mwenyekiti wa bodi hiyoniwaambie wajumbe wenzangu kwamba shirika limeoza sana na idadi kubwa ya wafanyakazi ambao hawana kazi za kufanya kwani hilo pia ni tatizo kwa sasa wapo wafanyakazi 160 wakati ipo meli moja tu, sasa wafanyakazi wote hao wa nini? Alihoji Mzee.
Mwakilishi huyo alisema ni wakati mwafaka kwa serikali kuchukua hatua za kurekebisha kasoro zake pamoja na kulifanya shirika hilo kuwa bora na lenye kutoa huduma kwa jamii ili kasoro zilizojitokeza huko nyuma zisitokee tena.
Hata hivyo Mzee aliipongeza serikali ya mapinduzi ya zanzibar kwa kukusanya zaidi ya shilingi billioni 17 kwa ajili ya matayarisho ya ununuzi wa meli mpya itakayotoa huduma kwa abiria wa Unguja na Pemba.
Aliyekuwa waziri wa mawasiliano na miundo mbinu ambaye alijiuzulu kutokana na matukio ya kuzama kwa meli Masoud Hamad alitaka shirika jipya litakaloundwa kufanya kazi kwa ushindani na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazowea.
”Waheshimiwa tunahitaji shirika la meli litakalofanya kazi kwa ushindani katika mazingira ya kibiashara kwa ajili ya kuleta faida na kutoa huduma kwa wananchi wa Unguja na Pemba, tunasema hivi kwa sababu shirika bado linafanya kazi kimazowea' alisema.
Alisema Zanzibar kwa kuwa ni kisiwa inahitaji kuwa na shirika la meli lake litakalotoa huduma za uhakika kwa wananchi licha ya kuwepo kwa taasisi binafsi za wananchi.
SMZ po katika hatua za mwisho za kusafisha wafanyakazi wa shirika la magari.
Serikali ya mapinduzi ya zanzibar imesema ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kuwastaafisha wafanyakazi wa shirika la magari ambalo limeshindwa kujiendesha katika ushindani wa kibiashara.Naibu waziri wa biashara viwanda na masoko Thuwaiba Edington Kisasi alisema hayo wakati alipokuwa akijibu swali la mwakilishi wa viti maalumu (CCM) Salma Bilali aliyetaka kujuwa hatma ya wafanyakazi wa shirika la magari ambalo serikali imeamuwa kulivunja shirika hilo.
Kisasi alisema uamuzi wa serikali wa kulifunga shirika hilo tayari umetekelezwa kwa mujibu wa sheria za kazi na utumishi wa serikali ambapo kazi iliyobaki kwa sasa ni kukamilisha kulipa stahili zao ikiwemo mafao.
'Serikali kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kuwalipa wafanyakazi wa shirika la magari ikiwemo viinua mgongo pamoja na pencheni'alisema.
Akifafanua zaidi alisema shirika la magari limeamuwa kuvunjwa baada ya kushindwa kujiendesha kwa faida pamoja na kushindwa katika mazingira ya ushindani wa kibiashara.
Alisema shirika hilo lilikuwa na majukumu ya kuagizia na kufanya biashara ya gari kutoka nje ya nchi,ambapo kwa muda mrefu walifanikiwa kutekeleza majukumu hayo.
Hata hivyo alisema kutokana na ushindani wa kibiashara na kupunguwa kwa mtaji wa shirika.liliyumba na baadaye kufanya biashara ya kununuwa na kuuza baiskeli.
'Hayo ndiyo mazingira ambayo yalipelekea shirika la magari nchini kufa baada ya kushindwa kujiendesha kwa faida katika mazingira ya ushindani'alisema.
No comments:
Post a Comment