ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 15, 2013

Spika: Bunge limepwaya

Spika wa Bunge,  Mh. Anne Makinda
Asema limezidi mno ushabiki wa kisiasa
Ataka iundwe seneti ya masuala ya kitaifa
Jaji Mkuu: Katiba ilinde uhuru wa mahakama
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amependekeza Katiba Mpya itamke kuwapo mabunge mawili; Bunge la sasa na lile la Seneti, huku Jaji Mkuu, Othman Chande, akipendekeza Tume ya Utumishi wa Mahakama iwezeshwe na katiba hiyo kuilinda Mahakama ya Tanzania kuingiliwa na chombo chochote.

Mapendekezo hayo, ambayo ni sehemu ya maoni ya Spika Makinda na Jaji Mkuu Chande kuhusu uundwaji wa Katiba Mpya, yalitolewa na viongozi hao kwa niaba ya taasisi wanazoziongoza, kwa nyakati tofauti walipokutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini Dar es Salaam jana.

SPIKA MAKINDA
Kwa upande wake, Spika Makinda alisema anapendekeza kuwapo kwa Seneti kwa kuwa viwango na uzoefu wa wabunge wake (seneti) vya kuchambua na kupambanua mambo yanayohusu maslahi ya Taifa havilingani na vile vya Wabunge wa Bunge la sasa.

Alisema kwa mfano, katika Bunge la sasa, Wabunge wanaweza kujadili hoja yenye maslahi kwa Taifa, lakini mwisho wake wanajikuta wakiangukia kwenye kuingiza itikadi za vyama vya siasa wanavyotoka katika hoja husika.
“Kwa hiyo, tunaona kuna umuhimu wa kuwa na Bunge la Seneti, ambalo watu (wabunge wake) watakuwa na uzoefu wa kuchambua na kupambanua mambo kwa maslahi ya Taifa bila kuingiza itikadi za kisiasa,” alisema Spika Makinda.

Alisema sababu nyingine anayoiona kuwa ni mwafaka kwa Tanzania sasa kuwa na mabunge mawili, ni ukubwa wa nchi.

Spika wa Bunge, Anne Makinda, amependekeza Katiba Mpya itamke kuwapo mabunge mawili; Bunge la sasa na lile la
Mbali na hilo, pia alipendekeza Spika wa Bunge asitokane na vyama vya siasa na pia asiwe mbunge.

Alisema mfumo huo mpya utamuwezesha Spika kufanya maamuzi kama Spika na pia utasaidia kumudu shughuli za Bunge, ambazo alisema kuwa ni nyingi.

Pia alipendekeza Katiba Mpya itamke kuwapo naibu makatibu wawili wa Bunge.
Alisema pendekezo hilo ni muhimu kwa kuwa Bunge limepanuka, lina shughuli nyingi na Katibu wa Bunge amekuwa akizidiwa na kazi nyingi.

Vilevile, Spika Makinda alipendekeza mawaziri wasiwe wabuge na kusema mfumo huo utawawezesha kufanya kazi zao kwa usawa. Kuhusu viti maalum vya wabunge wanawake, Spika Makinda alisema bado vinahitajika kuendelea kuwapo.

Alisema anapendekeza hivyo, kwa kuwa mfumo dume bado upo majimboni, ambako alisema wanaosimama kuwania ubunge katika maeneo hayo, wanawake ni wachache.

“Hivyo, tukiondoa viti maalum tutarudi nyuma. Bado wanawake wetu wanaendelea kuelimika,” alisema Spika Makinda.

Kuhusu ukomo wa wabunge kukaa bungeni, Spika Makinda alisema katiba inaweza kuweka ukomo.
Lakini akasema kuna mtu anaweza kuendelea kung’ara jimboni kadiri anavyosimama kuwania ubunge kutokana na utekelezaji wake mzuri wa ahadi kwa wananchi.
“Kwa hiyo, hatuoni sababu ya kuona ukomo kwa wabunge. Kwa sababu pengine bado mtu atakuwa anapendwa jimboni,” alisema Spika Makinda.

JAJI MKUU CHANDE
Kwa upande wake, Jaji Mkuu Chande, alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama siyo ya kisiasa, hivyo akapendekeza Katiba Mpya iiwezeshe kuilinda Mahakama ya Tanzania kuingiliwa na chombo chochote nchini.

Pia alipendekeza Tume ya Uteuzi wa Majaji kupanuliwa, kwamba badala ya kuwa na wajumbe sita wawe 12, pia wajumbe wawe washauri wa mwisho katika kuteua majaji.

Vilevile, Jaji Mkuu Chande alipendekeza Katiba Mpya itambue haki ya wananchi kupata fursa ya kupata haki, pia itamke fursa ya wananchi kupata haki na katiba iwe ndiyo mtawala wan chi na kila mtu aifuate.

TUME YA MIPANGO
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema jana walikutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kupendekeza kuwa Katiba Mpya itamke kuwa kiongozi awe mcha Mungu, mwenye nidhamu na anayeguswa na mtatizo ya wananchi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: