Kwa nini mapenzi yameharibu baadhi ya maisha ya watu? Huwa najiuliza maswali mengi yenye kwa nini, yakihusisha mapenzi. Kwa ujumla kama nilivyo na maswali mengi, majibu pia yamekuwa mengi.
Kwa vyovyote itakavyokuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha hayawezi kukamilika bila mapenzi. Ninapozungumza mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Mapenzi hayo, hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo uliyemzimikia, hatari kubwa iko mbele yako.
Nasema hatari iko mbele yako najua huwezi kuwa na mwisho mzuri. Kama ni msichana utachezewa na mwisho wa siku utaachwa solemba kwa kuwa tu uliyemruhusu aingie kwenye moyo wako hajakupenda kwa dhati.
Lakini pia kukubali kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye moyo wako unasema ‘no’ siku za baadaye unaweza kujikuta unachukua maamuzi ambayo yanaweza kuyaathiri maisha yako kwa kiwango kikubwa.
Kumbuka mapenzi ni nguzo ya maisha yetu tena nguzo muhimu sana. Kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utatawaliwa na amani siku zote.
Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda. Yaani yeye anaonesha kukuzimikia ile mbaya huku akikuahidi mambo mazuri lakini ukijaribu kufanya mawasiliano na moyo wako unakujibu kuwa hauko tayari kumpokea.
Ukweli wa mambo ni kwamba, mtu huyo unatakiwa kumweleza ukweli, yaani umkatalie kiroho safi tu kwa kuwa hakuna sababu za msingi za kukufanya wewe ulazimishe kuwa naye. Unalazimisha kumpenda kwa sababu za utajiri wake? Utakuwa unaidhulumu nafsi yako hivyo kwa kuwa moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, muache apite.
Muache aende kwa kuwa, penzi linaloweza kukupa amani ni lile ambalo moyo wako umeridhia. Kulazimisha penzi eti kwa kuwa umeona jamaa ana fedha za kutosha ni sawa na kujiingiza kwenye kaburi wakati bado hujafa.
Uchunguzi wangu mdogo umenionesha kuwa, kuna wasichana wengi ambao maisha yao yako gizani kwa kuwa wamekubali kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na wanaume ambao hawawapendi.
Baadhi wakitongozwa na mwanaume ambaye anaona wazi kuwa hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo.
Hufanya hivyo akijidanganya kuwa eti atakuwa akiunda penzi taratibu kitu ambacho hakiwezi kufanyika na kama kitafanyika lazima usanii utakuwepo ndani yake.
Hili ni tatizo kubwa na ndiyo maana nikaona leo nilizungumzie ili kuwanusuru wale wanaohatarisha maisha yao kwa kukubali kuingia kwenye uhusiano/ndoa na watu ambao hawawapendi kwa sababu ya tamaa zao.
Kuanzi leo, kama uko kwenye uhusiano hakikisha uliyenaye unampenda na si kwamba unalazimisha kumpenda kwa sababu ya mali alizonazo. Kama hujaingia kwenye uhusiano, kuwa makini na watu wanaokutokea, unayemkubali kuwa wako hakikisha moyo wako umemuidhinisha na si vinginevyo.
Kwa leo ni hayo tu, tukutane
wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
1 comment:
Mtoa mada,naona una bifu na wanawake wa tz. Kama wewe ni mtz,rudi kupata ushauri wa wanaume tz. Chunguza wanaume wengi wenye demu wabongo,wao ndio wanatunzwa na majike,so wadada siku hizi wamechoka,kuchuna mabuzi tu. Sikufichi,nimekuwa na mahusiano na kaka wa nchi tofauti,wao kutunza wanawake ni jambo la fahari,hawalalamiki,wewe kulipia chakula,drinks usiku moja unasimanga? Check ur manners plz.
Post a Comment