ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 12, 2013

Wanafunzi 136, 923 waliofeli kurudia

Naibu Waziri wa wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi, Philipo Mulugo

Mbeya yang'ara
Dar yaongoza kwa kufeli
Lindi na Mtwara zashika mkia

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imetangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha pili ambapo wanafunzi 136,923 wamefeli.
Kutokana na matokeo hayo wanafunzi wote waliofeli watalazimika kurudi kidato cha pili mwaka huu.Kwamujibu wa matokeo ya mtihani huo uliofanyika kuanzia Novemba 5 hadi 16 mwaka jana, mkoa wa Dar es Salaam ndio unaoongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi watakaorudia mtihani huo kutokana na kufanya vibaya.

Akitangaza matokeo hayo jana mbele ya waandishi wa habari, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philipo Mulugo, alisema Shule ya Sekondari ya St. Francis ya mkoa wa Mbeya inaongoza kwa kutoa mwanafunzi bora kitaifa na wanafunzi sita bora.

Alisema wanafunzi ambao hawakufaulu mtihani huo ni sawa na asilimia 35.45 ambapo wasichana ni 74,020 na wavulana ni 62,903.

Mulugo alisema wanafunzi waliofaulu mtihani huo ni 249,325 sawa na asilimia 64.55 ya wanafunzi 386,271 waliofanya mtihani huo kati yao wasichana ni 113,213 na wavulana ni 136,112, na kwamba kiwango cha ufaulu kimepanda kwa asilimia 19.15 kutoka asilimia 45.40 mwaka 2011.

Alitoa mchanganuo kuwa watahiniwa waliofaulu kwa kiwango cha alama A, B, na C ni 127,981 sawa na asilimia 33.13 na waliofaulu kwa kiwango cha D ni 121,344 sawa na asilimia 31.42 ambapo alama ya juu ya ufaulu ilikuwa ni asilimia 92.

Aliongeza kuwa wastani wa ufaulu kwa masomo yote ilikuwa ni asilimia 38 ukilinganisha na asilimia 31 ya mwaka juzi na kwamba idadi ya waliofeli mwaka jana imepungua kwa watahiniwa 91,836 ya watahiniwa 228,759 waliofeli mwaka juzi.

Alisema idadi ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani walikuwa 430,327 lakini watahiniwa 386,271 ndio waliofanya mtihani huo kati yao wasichana ni 187,244 na wavulana 199,027.

Watahiniwa 44,056 ambao ni sawa na asilimia 10.24 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo utoro, kuugua, kudaiwa ada, kufukuzwa shule, kupata mimba na vifo.

UDANGANYIFU MITIHANI WAPUNGUA
Mulugo alisema watahiniwa 23 kutoka shule za sekondari 10 wamefutiwa matokeo ya mtihani huo kutokana na tuhuma za udanganyifu ambao umepungua kwa kiwango cha asilimia 98.Alisema Shule za Sekondari za mikoa ya kanda ya Magharibi zimeongoza kwa kuwa na idadi ya wanafunzi 11

waliofanya udanganyifu, shule hizo ni Shule ya Sekondari Bukene ambayo wanafunzi saba wamefutiwa mtokeo ya mtihani, nyingine ni Kili, Binza,Kizumbi na Kolndoto.

Shule za Sekondari za mikoa ya kanda ya Ziwa zimeshika nafasi ya pili kwa udanganyifu wa mitihani ambazo ni Nyashishi,Thaqaafar,Paroma na Murangi, wakati kanda ya Mashariki ni shule ya Sekondari ya Kiyongwire.

Naibu Waziri huyo alisema hata hivyo wanafunzi waliofutiwa matokeo ya mtihani huo watalazimika kurudia kidato cha pili mwaka huu.

“Kukariri kidato si adhabu bali ni kutoa fursa nyingine kwa mwanafunzi kuweza kupata maarifa, stadi na ujuzi wa elimu ya sekondari kidato cha kwanza na pili kwa kiwango kizuri,”alisema Mulugo.

SHULE KUMI BORA ZATAJWA
Mulugo alizitaja shule za serikali zilizoshika nafasi kumi za mwanzo kuwa ni Shule ya Sekondari Mzumbe, Tabora wavulana, Iliboru, Kibaha, Iyunga, Msalato, Malangali, Ifunda ufundi, Samora Machel na Kilakala.

Shule za sekondari binafsi zilizoshika nafasi kumi za mwanzo ni Kaizirege, Marian wavulana, ST Francis, Donbosco, Bethel SABS, Marian wasichana, Don Bosco (Moshi), ST. Joseph Iterambogo sem na Carmel.

SHULE ZILIZOFANYA VIBAYA ZATAJWA
Shule za sekondari za serikali za mikoa ya kusini ambayo ni Mtwara na Lindi zimeshika nafasi kumi za mwisho.

Shule hizo ni Mihambwe, Dinduma, Kiromba, Marambo, Mbembaleo, Kinjumbi, Litipu, Luagala, Miguruwe na Napacho, wakati shule binafsi ni Mfuru, Pwani, Doreta, Kigurunyembe, Ruvuma, AT-Taaun, Jabal HIra sem, Mkono wa Mara, Kilepile na Kiuma. Aidha Mulugo, ametoa onyo kwa wazazi watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao watakaorudia kidato cha pili kuwa wakibainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
CHANZO: NIPASHE

No comments: