ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 11, 2013

Wanafunzi waishauri serikali mabadiliko ya mitaala

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki
Serikali imeombwa iwe na mitaala madhubuti katika elimu ili kufanya wanafunzi wawe na maendeleo mazuri katika masomo yao.

Hayo yalisemwa na mhitimu wa kidato cha sita, Bobu Chahawange, wakati alipokuwa akisoma risala kwa mgeni rasmi Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki, katika mahafali ya nane ya shule ya Sekondari Mtakatifu Mathew ya mkoani Pwani.

Wahitimu hao waliiomba serikali kuweka mitaala maalum kwani imekuwa ikibadilishwa mara kwa mara na kuwafanya wawe na mambo mengi ya kusoma na hii inaweza kusababisha kujichanya katika masomo yao.

Pia waliiomba serikali kuboresha sera ya mikopo ya elimu ya juu, kwani kuna baadhi ya wanafunzi hushindwa kujiunga na vyuo vikuu kwa kukosa ada.Kwa upande wake, Waziri Kagasheki ambaye aliwakilishwa na Mkurugenzi wa Wizara hiyo, Dornatus Kamamba, alisema kuwa atafanyia kazi maombi hayo yaliyotolewa na wanafunzi hao.

Pia aliupongeza utawala wa shule kwa kujali walimu wake kwani ni shule chache nchini ambazo zinajali walimu wake kwa mantiki hiyo iwe mfano wa kuigwa.

Aidha, aliwataka wanafunzi hao wajiepushe na matendo maovu kama uvutaji wa sigara au bangi, unywaji wa pombe na matendo mengineyo ambayo hayakubaliki katika jamii inayowazunguka.

Kagasheki aliwapongeza wanafunzi kwakuwa mahiri katika masomo yao na kuona ubunifu wao wakati anatembelea maonyesho ya wanafunzi hao.

Chanzo:Nipashe

No comments: