ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 19, 2013

Werema amshukia Balozi wa Uswisi

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema amekerwa na kauli ya Balozi wa Uswisi nchini Olivier Chave, aliyesema kuwa Serikali ya Tanzania haijaonyesha nia ya dhati kutaka kuchunguza na kupata ukweli wa mabilioni ya fedha yaliyofichwa nchini humo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumamosi katikati ya wiki hii, Werema, alitaja hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu suala hilo kuwa ni kuwasiliana na mamlaka husika nchini Uswisi na kuundwa kwa kamati maalumu ya kufuatilia suala hilo.

Jaji Werema alisema kuwa hawezi kumjibu chochote balozi huyo kwa kuwa ni mtu mdogo kwake.
“Najua kuwa huyu balozi ana kinga, ila siyo adabu hata kidogo kuzungumza maneno yale kwenye nchi ya watu. Kama ingekuwa ni balozi wa Tanzania huko Uswisi kasema maneno haya, angeambiwa tu arudi nyumbani kupumzika hadi watakapomhitaji,” alisema Werema.

Januari 11, mwaka huu, Balozi Chave
aliliambia gazeti hili katika maojiano maalumu kuwa hadi sasa hakuna jitihada zozote zilizofanywa na Serikali ya Tanzania kutaka ufumbuzi wa tuhuma za watu walioficha fedha nchini humo.
Katika ufafanuzi wake, Werema alisema kwamba tayari timu iliyoundwa imeshafanya kikao cha kwanza Januari 9, mwaka huu na sasa inaendelea kutekeleza majukumu iliyopewa.
Alifafanua kuwa timu hiyo iliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baada ya kupata kibali cha Rais Jakaya Kikwete na itafanya kazi zake kwa usiri mkubwa kutokana na unyeti wa suala hilo.
Werema alieleza kuwa hadi kufikia Aprili mwaka huu, watakuwa na jambo la kueleza umma kutokana na uchunguzi huo.
“Suala hili ni nyeti, ndiyo maana unaona sisi wengine tumefunga midomo yetu. Tunafanya kazi kama Chui na Simba, huku hakuna Kambale wala nini,” alisema na kuongeza:
“Kazi iliyo mbele yetu ni ngumu, tunafanya kazi hii na benki zinazofanya shughuli zake kwa usiri mkubwa, ingekuwa zipo huku kwetu hizi fedha tungezipata, kwa hiyo Watanzania watuombee tuimalize kazi hii vizuri.”
Alibainisha kuwa, watakuwa na vikao vingi ikiwamo cha wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, ili kujadili suala hilo na kuangalia namna ya kulikamilisha.
Werema alisema kwamba baada ya kuibuka kwa habari za Watanzania kuficha fedha nchini Uswisi, Serikali iliandika barua kwa vyombo vya nchi hiyo vinavyohusika na masuala ya fedha, wakivitaka viwape taarifa za akaunti za Watanzania.
“Walitueleza tunachojaribu kufanya ni sawa na mtu anayevua samaki, anajua kabisa kuwa baharini kuna samaki, lakini mahali walipo hapajui. Walitaka tuwape majina ya wahusika tunaowataka, kisha kuwaeleza kwa nini tunazitaka,” alieleza.
Alisema katika kufuatilia hilo, wataenda mbali zaidi kwa kufuatilia majina yote watakayopata na kuangalia wahusika kama wana kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuweka fedha hizo katika nchi hiyo.
Alisema katika kutekeleza majukumu yao, watataka pia ushirikiano kutoka kwa watu mbalimbali wenye taarifa za walioficha fedha hizo, ikiwa ni pamoja na wanaotajwa katika majukwaa na wale ambao hawajatajwa.
Alieleza kuwa Zitto Kabwe ambaye ndiye aliyeeleza suala hilo bungeni ni mtu muhimu kwao, hivyo wakati utakapofika atashirikishwa.
“Hawezi kuwa mjumbe wa timu hii kwa kuwa imeshaundwa, lakini muda utakapofika tutamshirikisha. Hatuwezi kabisa kuacha kumshirikisha kwa sababu ni mtu muhimu katika suala hili, ila kwa sasa tupo katika hatua za awali kabisa,” alisema na kuongeza:
“Mnatakiwa kuwa wazalendo, waandishi wa habari mnakutana na watu wengi na kuwapeni taarifa. Pia kama kuna mtu yeyote mwenye taarifa atusaidie ili tuweze kutekeleza hili, nchi hii ni yetu wote jamani.”
Hata hivyo, alisisitiza kuwa, jambo la msingi wanalochunguza kwa sasa ni endapo watu hao wameficha fedha hizo kihalali au la.
“Tukipata taarifa kwa sasa tunaweza kwenda kwenye hizo benki, hatutaki kwenda tu na kusema tupewe majina ya Watanzania walioweka fedha zao huko, ukifanya hivyo kama huyo mtu atakuhurumia sana atakufukuza, lakini kama ni mweledi atakuitia polisi,” alisema Werema.
Alisisitiza kuwa, ili kubaini suala hilo watatumia njia zote ikiwamo zilizo rasmi na zisizo rasmi na kwamba suala la fedha hizo, linaakisi kwa kiasi kikubwa ripoti ya rushwa iliyotolewa na Jaji Warioba.
“Tukisema tutazipata, ina maana tuna uhakika kuwa zipo, kwa hiyo suala letu kwanza hapa ni kuangalia kama zipo na kama zipo kihalali kisha tuanze kuzifuatilia,” alisema
Alichokisema Balozi
Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Chave alisema: “Uswisi iko tayari kushirikiana na Tanzania kujua uhalali wa fedha hizo na endapo zikigundulika ni fedha chafu basi tutazirejesha nchini.”
Aliongeza: “Serikali ya Uswisi haina tatizo kwani tumeshafanya hivyo kwa nchi za Ufilipino na Nigeria, hivyo tutafurahi na Tanzania kama tutamaliza suala hili.”
Alisema habari zinazoandikwa kuhusu mabilioni hayo kuhifadhiwa katika benki za Uswisi, yanaharibu picha ya nchi hiyo mbele ya mataifa mengine, hivyo angependa suala hilo kumalizwa na kwamba wao wako tayari.
Katika Kikao cha Tisa cha Bunge, Novemba mwaka jana, Zitto aliwasilisha hoja binafsi kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.
Kauli ya Zitto
Kwa upande wake, Zitto alisema hadi sasa Serikali haijamfuata kutaka kutoa ushirikiano wa aina yoyote kuhusu tuhuma hizo.
Alisema kuwa ingawa Serikali ilitaka iachiwe tuhuma hizo ili iweze kuzifanyia kazi, lakini hadi sasa ukimya umetawala.
Alisema: “Nitaandika barua na kumkabidhi AG siku ya Jumatatu (Januari 16), nitahoji nini kinachoendelea katika uchunguzi huo.”
Alisema Serikali ya Tanzania haionyeshi nia ya kuzihitaji fedha hizo.
Aliongeza kwamba kuna njia mbili za kuwabaini walioficha mabilioni hayo nchini Uswisi, kwanza ni kwa Serikali ya Tanzania kushirikiana na Serikali ya Uswisi, pili ni ulipaji wa kodi wa fedha ambazo Watanzania wameweka katika benki nchini humo.
Ilivyokuwa
Katika Kikao cha Tisa cha Bunge mwaka jana, Zitto aliwasilisha hoja yake binafsi kuhusu kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza Serikali kuchukua hatua dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.
Bila ya kuwataja kwa majina, Zitto aliwataja watu hao kwa nyadhifa kuwa ni watu wote walioshika nyadhifa za uwaziri mkuu katika kipindi cha 2003 hadi 2010, walioshika nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini katika kipindi hicho na waliokuwa makatibu wakuu Wizara ya Nishati na Madini.
Wengine ni mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi, wakuu wa majeshi, wanasheria wa Serikali, makamishna wa nishati, walioshika wadhifa wa Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Werema alisema kuwa Serikali imeanza kuzifanyia uchunguzi tuhuma hizo.
Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

Huyu WEREMA ni kichefuchefu kitupu. Hapa tunapata kuona umuhimu wa kumpunguzia madaraka Rais.. nchi kuwa na Attorney General kama huyu ni hasara kubwa. Huyu jamaa kazi yake ni kulipa fadhila kwa Rais kwa kazi yake aliyopewa..Huna hata aibu? Mwanasheria gani na ulisoma wapi wewe Werema? Hivi bado unafikiri waTanzania ni mbumbumbu? Hapana hatujalala... tunaelewa kinachoendelea huko serikalini.. Mwanasheria wa serikali anaomba wananchi waiombee serikali iweze kufanikiwa kurudisha pesa za nchi zilizofichwa? ...lol..kweli? Inaingia akilini kwa mtu hii? Halafu unasema balozi wa Uswis ni mtu mdogo? Je na pesa mnazoomba kwa ajili ya bajeti ya kila mwaka kutoka Uswis ni ndogo pia? Ebo...? We mzee muogope Mungu kabla ya shida zako...Wananchi wa Uswis wanatumia kodi zao kusaidia serikali ya Tanzania ambayo imejaa mafisadi na wewe ni mmojawapo kwa hiyo balozi anayohaki kuhoji serikali ya Tanzania. Tunafahamu fika mmekasirika kwa sababu mnataka kufunika hizi pesa.. Kama kweli mnafuatilia hizi pesa kwa nini iwe ni siri na kuomba muombewe dua? Wenye nchi wako tayari kuwasaidia sasa ugumu uko wapi? Hamtaki kwa sababu mtaumbuka, tunafahamu bora uendelee kunyamaza kuliko kuja kuongea utumbo.Hampendi kukosolewa wala kukumbushwa ndiyo maana mnang'ang'ania Rais aendelee kuwa na nguvu za kifalme:( Na wala usidanganye watu na demokrasia ya Uswis... Balozi anaweza kukosoa hapa na wala haijawahi kutokea kufukuzwa balozi hapa. Siku ipo utasimama mahakamani kujibu madhambi unayoyaficha kwa wanyonge waKiTanzania.

Anonymous said...

Asante kwa maelezo yako baba.

Huyu Werema ni kichefuchefu tuu. Watanzaia tumeamka, hapa inaonyesha kabisa kuwa wewe Bwana Werema ovyoooo huwezi kutetea haki za wananchi kabisa.