Timu ya Simba
Timu ya Yanga
Na Michael Momburi
UKIANGALIA mazingira ya Ulaya ambako Yanga ilikuwa imepiga kambi ya mazoezi kwa wiki mbili utagundua kwamba sisi bado tunaigiza mpira hatuchezi mpira wala hatuujui mpira.
Si hilo pekee. Kwa aina ya timu, viongozi na miundombinu yetu itachukua miaka mingi sana kukaribia kuujua mpira wanaoucheza wenzetu bado tuna kipindi cha kuendelea kuigiza.
Hakuna dalili ya kukaribiana na mpira wa ukweli, kumbuka hapa sizungumzii England, Hispania, Ujerumani au Italia nazungumzia Uturuki tu tena Antalya siyo Istanbul kwenye makao ya nchi.
Wenzetu wamewekeza. Achana na maisha binafsi ya mchezaji mmojammoja kuanzia timu ya wakubwa mpaka klabu zao za vijana. Timu zaidi ya 1000 zimefikia kwenye kambi zenye kila kitu. Kila hoteli mjini hapa ina kila kitu kinachofaa kwa kambi.
Ina uwanja wa kisasa ambao hata wachezaji wa Yanga saa nyingine walikuwa hawaamini kama kweli ndiyo wenyewe wanatumia viwanja hivyo kutokana na mazingira waliokulia na waliozoea kwenye mchanga wa Jangwani na Loyola.
Timu zote za Ligi Kuu ya Uturuki zimetenga bajeti kubwa za maendeleo na nyingi makao yake ni Istanbul, lakini zimekuja hapa kwa muda kuweka kambi kutokana na hali ya hewa ya Istanbul kuchafuka na kuambatana na barafu na baridi kali. Lakini ukiingia kwenye mazoezi na kambi unaona kweli timu iko makini. Upande mmoja inafanya timu ya wakubwa upande wa pili zipo timu mbili za vijana na zenye vifaa vya kutosha na unaona kabisa wachezaji wanatunzwa na wanafanya kazi.
Tofauti na timu zetu ambazo hata jezi ni tatizo licha ya kuwa na viongozi wenye maneno mengi na wanaopenda sifa. Wajerumani walikuwa wanashangaa Yanga inapashia jezi hizohizo na kuchezea hizohizo wanaona kituko. Hiyo ni Arminia tu ya daraja la nne si Werder Bremen.
Bado kwa mfumo wa uendeshaji wa klabu za Tanzania tuna safari ndefu ya kufikia kwenye mafanikio ya ukweli. Ubabaishaji bado ni mwingi na wajanja wachache wanaopiga makelele na wenye masilahi binafsi wanarudisha nyuma soka la Tanzania.
Tunafanya mambo kwa kuigiza zaidi, kwa mfano safari ya Yanga Uturuki itakuwa na faida zaidi kwa mchezaji binafsi kumkuza kiupeo na kumwonyesha nini kinafanyika duniani, lakini haitakuwa na masilahi kwa klabu labda kishabiki kwamba tulienda Ulaya na nyie mkaenda Arabuni, ila mwisho wa siku tukirudi uwanjani ni yaleyale.
Miundo mbinu hairuhusu mchezaji kufunguka ndio maana Jerry Tegete aliyekuwa akitupia Uturuki unaweza usimsikie kabisa atakapoanza kutumia uwanja kama Kaitaba.
Kwa nini nasema hivyo, ukiangalia mazingira Yanga ilipofanyia mazoezi hapa Antalya na itakapokuwa kuanzia wiki ijayo hapo Jangwani au Loyola ni vitu viwili tofauti mno. Ukipiga picha za video ukifananisha na kuangalia utajiuliza maswali mengi sana na hutapata majibu. Makeke aliyokuwa akifanya kwenye kapeti la Uturuki hawezi kuingiza kwenye vitendo katika vumbi la Sokoine pale Mbeya.
Ndiyo ukweli ingawa baadhi hawatapenda kuusikia. Ndiyo maana ni ngumu kumleta Wayne Rooney au Demba Ba Sheikh Amri Abeid nakutegemea akuonyeshe ufundi wake.
Simba na Yanga walipaswa kuwa na viwanja vyao vya hadhi kama vya hapa kwavile wana utajiri wa mashabiki na mbinu za kufanya mambo kama hayo. Kama tumeamua kutumia mamilioni ya fedha kufanyia maandalizi sehemu kama Arabuni au Ulaya tutengeneze na miundombinu nyumbani ambayo itatusaidia kuendeleza kile tunachokipata huku.
Azam imesimama yenyewe na kuonyesha mabadiliko hata Galatasaray au Fenabahce ikija Dar es Salaam inaweza kushawishika kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Azam pale Chamanzi, lakini Jangwani ni aibu, Simba ndiyo imebaki stori tu kila siku keshokesho.
Tubadilike tuache kutafuta sifa za kijinga kwa mashabiki, tubuni mambo ya maana zaidi kwa masilahi ya klabu zetu. Kama Mzee wa mwaka 1930 aliweza kujenga ghorofa ambalo ni makao makuu ya klabu kiongozi msomi wa karne ya 21 unashindwa kutengeneza hata uwanja wa mazoezi na gym ya maana? Tuache mchezo. Ipo siku hao wanachama wataujua ukweli na kitanuka kwelikweli.
Tuwekeze kwenye mambo ya maana kama Yanga tayari ina eneo tena lipo mjini, lakini kila siku ni propaganda tu na kuchimbachimba umma hauoni kitu cha maana kinachoendelea.
Mambo ambayo wachezaji wamejifunza Ulaya walitakiwa kufikia kwenye mjengo wenye viwanja vya maana na kuendelea kupasha kujiandaa na msimu.
Lakini hata gym ni tatizo mpaka timu ikachanganyike na raia uswahilini asubuhi na jioni. Hii ni aibu, tuache kufanya mambo kwa sifa.
Hawa wataalamu wa kizungu tunawaowaajiri kwa mamilioni ya shilingi, tuwatumie kutengeneza misingi imara. Lakini kama kocha anakuja klabu haina hata uwanja wa mazoezi, haina gym, haina kambi maalum ni kazi bure.
We ukimwambia tutafutie kambi Uturuki au Oman ndiyo faida kwake anakwenda kufanya kazi yake kwa hizo wiki mbili au tatu kesho yake anakurudishia timu yako Dar es Salaam unamfunga Polisi Morogoro kwa chenga za ujanja ujanja mwisho wa siku unachukua ubingwa wa kununua hufiki popote tunabaki kubishana tu hapo Ilala.
Siyo fasheni kuweka kambi nje ya Afrika tathmini mwisho wa siku kuanzia mchezaji binafsi mpaka klabu inafaidikaje? Ni hayo tu karibuni Dar es Salaam. 0713704195
1 comment:
Thanx A lot 4 Ur Opinions...Ukweli Mtupu ...
Post a Comment