Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi. |
Kadhalika, mahakama hiyo imemuamuru Mzombe kulipa Sh. milioni 37 baada ya kumaliza kutumikia kifungo chake.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi, Geni Dudu aliyesikiliza kesi hiyo.
Hakimu Dudu alisema baada ya upande wa mashitaka kuita mashahidi saba akiwamo Mzee Mwinyi, Katibu Muhtasi wake na wapangaji wake, mahakama imemuona mshtakiwa ana hatia bila kuacha shaka.Alisema katika ushahidi uliotolewa na Rais mstaafu Mwinyi, alidai alikuwa rafiki wa familia ya babu wa mshtakiwa, marehemu Seleman Mzombe.
Mzee Mwinyi katika ushahidi wake alidai kuwa alimfahamu Abdallah, akiwa dalali hivyo alimuamini na kumpa kazi zake mbalimbali ikiwamo ya kutafuta nyumba namba 481 iliyopo Mikocheni na nyumba namba 55 ya Msasani Village na kumkabidhi fedha za kufanya ununuzi wa nyumba hizo.
Alidai kuwa baada ya kununuliwa kwa nyumba hizo, Mzee Mwinyi na Mzombe, walikubaliana kuzipangisha na fedha zitakazopatikana zitumike kufanyia matengenezo na kiasi kitakachobaki apeleke kwa Mzee Mwinyi.
Aliongeza kuwa nyumba ya Mikocheni ilikuwa na wapangaji wanne na ya Msasani Village ilikuwa na mpangaji mmoja.
Mzee Mwinyi aliionyesha mahakama mikataba iliyokuwa imeingiwa na wapangaji hao na Mzombe.
Hata hivyo, katika ushahidi huo, Rais mstaafu Mwinyi, alidai kuwa tangu Mzombe anunue nyumba hizo na kuzipangisha, hakuwahi kupelekewa hata Shilingi ila anaamini ama mshtakiwa huyo amezihifadhi au ameziiba.
Mzee Mwinyi aliiambia mahakama kuwa wakati nyumba hizo zikifanyiwa matengenezo, mbali na fedha za kodi zilizokuwa zikikusanywa na Mzombe, yeye pia aliwahi kutoa Sh. 500,000 kwa ajili ya matengenezo hayo.
“Mzombe alijipatia pato la pango la jumla ya Sh. milioni 37.4 hata kama alitumia kufanya matengenezo kwenye nyumba hizo, haziwezi kufikia Sh. milioni 17, mimi nina imani ameziiba, hivyo naiomba sheria ichukue mkondo wake,” alidai.
Hata hivyo, mshtakiwa alidai kuwa kesi hiyo imetengenezwa ili kumfanya Mzee Mwinyi asitimize ahadi yake kwake ya kumjengea nyumba.
Lakini Hakimu Dudu alisema ushahidi wa mshtakiwa unatia shaka kwa sababu hata siku moja hakuwahi kusema polisi wakati akichukuliwa maelezo.
“Yote haya yanazidi kuubomoa utetezi wa mshtakiwa na mahakama inaona kuwa fedha alizozikusanya mshtakiwa kama ada ya pango la nyumba, hazijawahi kupelekwa kwa Mzee Mwinyi, alitenda kosa hilo la wizi,” alisema Hakimu Dudu.
Alisema upande wa mashitaka umethibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa ni mkosaji katika makosa yote mawili hivyo mahakama inamuona ana hatia.
Mshtakiwa aliiomba mahakama isimpe adhabu kali kwa madai kwamba ana familia kubwa inayomtegemea wakiwamo wazee na watoto wadogo.
Hakimu Dudu alimhukumu kifungo cha miaka mitatu jela katika kosa la kwanza na kifungo kingine cha miaka mitatu jela katika kosa la pili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment