ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 20, 2013

Askari polisi 240 kupewa mafunzo kulinda watalii

POLISI imesema itatenga askari 240 na kuwapa mafunzo maalumu kwa ajili ya ulinzi wa watalii katika mikoa yenye watalii wengi nchini.
Hayo yalisemwa jana na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Benedict Kitalika wakati akitoa mada kwenye mkutano wa kujadili jinsi ya kuwapatia ulinzi watalii na watu wenye hadhi ya kidiplomasia wanaotembelea mbuga za wanyama, hifadhi na vivutio mbalimbali nchini.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na Chama cha Kuratibu Shughuli za Utalii Tanzania (TATO), alisema kuwa tayari wamepeleka mapendekezo ili kutengewa zaidi ya Sh80 milioni kutoka katika bajeti ya Mambo ya Ndani kwa ajili ya kazi hiyo.Kitalika alisema kuwa kitengo hicho kilichoanza Julai mwaka jana ni maalumu baada ya kuibuka mauaji na uporaji kwa watalii wanaofika nchini kutembelea vivutio hivyo.
Alisema kuwa nguvu zaidi zitaelekezwa katika mikoa ya Arusha, Mara, Manyara na Zanzibar ambako ndiko kwenye idadi kubwa ya watalii.
Awali akiwasilisha mada yake, Mkurugenzi Mtendaji wa TATO, Mustapha Akunaay, alisema kuwa kuna haja ya kuundwa kwa kitengo hicho kwa ajili ya kuwalinda watalii ambao huuawa ama huporwa na kuharibu sifa ya Tanzania katika sekta hiyo.
Alisema kuwa, haja ya kufanya hivyo inatokana na sekta ya utalii kuchangia asilimia 17.5 ya pato ghafi la ndani na kutoa ajira rasmi 500,000 na 800,000 zisizo rasmi pamoja na kufikisha watalii 867,994 walioingiza Dola za Marekani Sh1.35 bilioni mwaka 2011.   
Mwananchi  


No comments: