ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 9, 2013

BAADA YA HOJA ZAO 'KUTUPWA' BUNGENI:Wabunge wa upinzani kutua Dar kwa kishindo

James Mbatia.

Chadema yaratibu maandamano, mkutano wa hadhara Temeke
Polisi yapiga marufuku, yasema mambo ya Dodoma yaishie Dodoma
CUF yajiweka kando na Temeke ni ngome yao, hawatashiriki

Baada ya hoja binafsi za wabunge wa upinzani `kuzimwa’ bungeni, sasa wanaelekea kutaka kuungwa mkono kupitia nguvu ya umma.

Wabunge hao wakiongozwa na uratibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), watarejea jijini Dar es Salaam kesho na kupata mapokezi, kisha kuandamana hadi wilayani Temeke ambapo watahutubia mkutano wa hadhara.Hata hivyo, Polisi imeonya kwamba mapokezi hayo hayapaswi kuhusisha maandamano, isipokuwa mkutano wa hadhara pekee.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, alisema kinachotarajiwa kufanywa na wapinzani ni mkutano wa hadhara na si maandamano.

Lakini Benson alipoulizwa baadaye na NIPASHE Jumamosi, alisema chama hicho kimeshaandika barua polisi, kuwataarifu kuhusu maandamano hayo.

“Tumewaandikia barua juu ya azma yetu ya kuwapokea wabunge wote wa upinzani kesho, kisha maandamano yatakayoanzia Ubungo, Tazara hadi Temeke kwenye mkutano wa hadhara,” alisema.

Aliongeza, “maandamano yatakuwa makubwa kwani yatashirikisha vyama vingine vya upinzani ambavyo tumeviandikia barua.”

Hata hivyo, Kamanda Kiondo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi alisema, barua ya Chadema imekaa ‘kimtego-mtego’ na kwamba wameibaini ‘janja’ yao.

“Maandamano hayatakuwepo, kilichoruhusiwa ni mkutano wa hadhara tu,” alisema katika hali inayoashiria (pengine) kukatokea vurugu.

Benson alisema mkutano huo ni mwanzo wa mfululizo wa mikutano itakayofanyika kwenye kanda 10 zilizotengwa na Chadema, kuanzia mwenzi huu.

“Tunakwenda kuwauliza Watanzania ni Spika na Naibu Spika wa namna gani wanayemtaka,” alisema.

“Huyu Anne Makinda (Spika) na Job Ndugai (Naibu Spika) wamekigeuza kiti kile kama kijiwe cha CCM na serikali yao. Kiti wamekigeuza kama cha Mungu. Tunataka Bunge ambalo ni sauti ya wananchi na si kijiwe,” alidai.

Aliongeza, “Watanzania ndio watakaoamua kama wanawahitaji Makinda na Ndugai wabaki kwenye nyadhifa zao.”

Benson alidai kuwa kilichotokea bungeni si kwamba kanuni zina matatizo kwa maana zimekuwepo hata wakati wa Bunge lililopita likiongozwa na Waziri wa Mambo ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Alisema wakati wa Sitta akiwa Spika, Bunge lilikuwa na heshima na utaratibu mzuri na hivyo kanuni za sasa `zinaharibiwa’ na Makinda na Ndugai.

CUF YAKANA KUSHIRIKI
Wakati Chadema ikisema shughuli hiyo itahusisha vyama vya upinzani, Chama Cha Wananchi (CUF) kimejiweka kando na kusema hakitashiriki.

“Hakuna kikao chochote tulichokaa, wanataka kuwahadaa wananchi tu. Suala hili ni lao wao wasilazimishe kutushirikisha. Hatutakuwepo,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro.

Mtatiro alisema inawezekana Chadema wamebaini kuwa Temeke ni ngome ya CUF, hivyo wanawahadaa wananchi ili wapate muitikio kwenye maandamano na mkutano huo.

“Wakitaka kufanya siasa wafanye tu, lakini wasiwahadae wananchi,” alisema.

Kamanda wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alikana kupata taarifa kuhusu maandamano na mkutano huo.

“Wanawapokea wabunge wao wanatoka Ulaya? Mi sina taarifa hebu wasiliana na kamanda wa Temeke,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda Kiondo alisema, “taratibu za kuomba maandamano zinaeleweka, barua waliyotuletea imeandikwa kimtego-mtego, tumewakubalia mkutano na si maandamano.”

Aliongeza, “hawa watu hawana maslahi na hii nchi, wanataka kuleta vurugu tu, kuwatia hasara watu na hata kusababisha mauaji.

“Juzi tu matatizo yametokea Mtwara, leo wanataka kuhamishia Temeke, hatukubali. Suala la Dodoma limekwisha jadiliwa limekwisha, hao wabunge wao watashuka Tazara watawapokea bila maandamano,” alisema.

Chadema imelazimika kuratibu maandamano hayo na mkutano wa hadhara kama ishara ya kumpokea mbunge wao wa jimbo la Ubungo, John Mnyika kwa madai ya kufanyiwa mizengwe bungeni kwa kuondolewa kwa hoja yake binafsi.

Hoja binafsi ya Mnyika ilikuwa ni kupendekeza Bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika jiji la Dar es Salaam, hoja ambayo ilitupiliwa mbali na kuzua mtafaruku bungeni.

Hoja nyingine ni ya Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliyoitoa bungeni juu ya udhaifu wa mitaala ya elimu nchini.

Pamoja na katazo hilo la polisi kuhusu kutokuwepo kwa maandamano hayo, lakini maandalizi yalipamba moto huku magari yenye vipaza sauti yakiwa yameandaliwa katika ofisi za makao makuu ya Chadema, Kinondoni ili kuwahamasisha watu kujitokeza kwenye maandamano hayo ya kuwapokea wabunge wao.

CHANZO: NIPASHE

No comments: