Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
UMOJA wa vyama tisa vya siasa vya upinzani, vinavyoongoza hoja ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara kupinga mradi wa usafirishaji wa gesi kwa njia ya bomba kwenda Dar es Salaam, umekutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kumfikishia ujumbe unaoeleza kuwa wananchi wa Mtwara hawajamwelewa.
Kikao hicho kilifanyika nyumbani kwa Pinda jijini Dar es Salaam, Jumamosi ya Februari 2, baada ya umoja huo kukosa nafasi ya kukutana naye kwa mara ya pili, wakati Waziri Mkuu huyo alipofanya majumuisho ya ziara yake mkoani Mtwara katika Ukumbi wa Veta mjini humo.Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mtwara jana, mmoja wa wajumbe wa umoja huo Mustafa Nchia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mtwara Mjini, alisema kuwa walilazimika kufunga safari kwenda kuonana na Waziri Mkuu, ili kumfikishia ujumbe kuwa wananchi wa Mtwara bado hawajamwelewa.
“Tulikutana Jumamosi nyumbani kwake Dar es Salaam, tukamwambia kuwa wananchi wa Mtwara bado hawajakuelewa… Baada ya kumaliza ziara yake katika majumuisho hakutuuliza kama tumekubaliana au la,” alisema Nchia na kuongeza:
“Alikwenda kwenye vyombo vya habari na kusema amemaliza mgogoro, sisi tumemwambia bado wananchi wa Mtwara wana manung’uniko moyoni mwao, wanataka gesi isisafirishwe kwa njia ya bomba.”
Alieleza pia kwamba walimfikishia Pinda, kilio cha wana-Mtwara cha kumkataa Mkuu wa Mkoa, Joseph Simbakali, kwa maelezo kuwa tayari watu wamekosa imani naye, hivyo hawawezi kushirikiana vyema katika maendeleo.
Januari 28, mwaka huu katika kikao cha majumuisho cha ziara ya Waziri Mkuu, Simbakalia aliwaomba radhi wakazi wa mkoa huo kwa kuwaita wapuuzi na baadaye wahaini, wakati walipomwalika kupokea maandamano yao Desemba, 27 mwaka uliopita.
“Tulimshauri Waziri Mkuu amhamishe siyo tu kwa sababu watu wa Mtwara hawamtaki, pia hata kama ataendelea kuwapo Mtwara, watu hawapo tayari kumpa ushirikiano…ili wananchi wa Mtwara wawe na ari ya kutoa ushirikiano kwa Serikali yao na kufanya kazi vizuri ni vyema Simbakalia akahamishwa,” alisema Nchia.
Aliongeza: “Ametuhakikishia kulifikisha hili kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa yeye ndiye aliyemteua…; Masuala haya mengine alitujibu kuwa ametusikia.”
Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo, Uledi Abdallah aliongeza kuwa katika kikao hicho pia walimwomba Waziri Mkuu awafungulie kuendesha mikutano ya hadhara, ili wananchi waweze kupata taarifa sahihi za mustakabali wa madai yao.
“Mtakumbuka kuwa kanda hii ya Kusini kumezuiliwa kufanya mikutano ya kisiasa, sisi tumemwambia Pinda kwamba hapo hatatui tatizo bali anaongeza…Tatizo la watu wa Mtwara hawapati taarifa sahihi kwa wakati na njia ya kuwapa taarifa hizo ni mikutano ambayo wameizuia…Hapo tunaandaa tatizo lingine,” alisema Abdallah na kuongeza:
“Iwapo hatutaruhusiwa kuendesha mikutano, tutaandaa maandamano makubwa ambayo hata kama hatutapata kibali, tutayafanya kudai haki yetu ya kueleza hisia na mawazo yetu, haki ya kupata na kutoa habari.”
Naye msemaji wa umoja huo Hamza Masoud Licheta alisema kuwa siyo kweli kwamba umoja huo umehongwa fedha ulipokwenda kuonana na Waziri Mkuu, bali ulikwenda kufikisha ujumbe sahihi wa watu wa Mtwara.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment