Monday, February 4, 2013

chadema yataka serikali ichunguze mashirika yake


Salma Said, Zanzibar

CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelitaka Baraza la Wawakilishi kupitia kamati teule kuendelea kuchunguza taasisi za serikali na mashirika ya umma ambazo zinaonekana kufanyika ubadhirifu wa fedha za umma katika taasisi hizo.

Akizungumza na wandishi wa habari Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Hamadi Mussa Yussuf huko afisini kwake Kidongo Chekundu Mjini Zanzibar alisema kumekuwa na mfumo mchafu wa ubadhilifu katika tasisi za serikali na baadhi ya mashirika ya umma unaofanywa na watu waliokabidhiwa majukumu.Akiyataja mashirika ambayo yanapaswa kuchunguza, Yussuf alisema ni pamoja na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZBB), Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) Mfuko wa Hifadhi ya jamii Zanzibar (ZSSF) na bodi ya mikopo ya Zanzibar ambazo zinaonekana kuwa na mashaka kutokana na kukosekana uadilifu katika mashirika hayo.

Alisema baadhi ya watendaji katika mashirika hayo wamekuwa wakichukua fedha za umma na kufanya mashirika kama ni kampuni zao binfasi bila ya kujali fedha za wavuja jasho ambao hutozwa kodi kila siku huku maisha ya wananchi maskini yakiwa duni siku hadi siku.

Yussuf alisema hivi karibuni Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) limeonekana kufanya ubadhirifu wa mabillioni ya shilingi na kuitia hasara kubwa serikali kutokana na watendaji wake kutokuwa waaminifu.

Naibu huyo alisema taarifa ya kamati ya baraza la wawakilishi iliyotoa ripoti ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), kuna mambo kadhaa yameibuka katika ubadhirifu uliofanywa na watu wenye mamlaka serikalini ambapo mabilioni ya fedha za umma yameteketea.

Amesema kamati iliyochunguza kadhia ya manispaa ya mji wa Zanzibar pamoja na kamati iliyochunguza ufisadi wa ardhi zote zimethibitisha pasipo na shaka kwamba viongozi wengi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi wanatumia madaraka yao vibaya lakini bado serikali imeshindwa kuchukua hatua dhidi ya wale watu waliotajwa licha ya kuwepo na ushahidi wa waziwazi.

Hamad alisema viongozi hao wamekuwa wakijinufaisha wao binafsi kwa kushiriki vitendio vya ubadhilifu wa mali ya umma na wizi wa kupindukia kwa kuwa mabillioni ya shilingi ya wavuja jasho yamepotea.

“Chadema tunalani vitendo vyote vya wizi ubadhilifu na ufisadi vilivyofanywa na watendaji na viongozi wa serikali waliopewa dhamana na wananchi na tunaitaka serikali ichukue hatua stahiki za kisheria kwa wote waliohusika kwenda kinyume na kiapo cha utii na kwa mujibu wa sheria wanapaswa kuwajibika”alisema Naibu huyo.

Alisema Chama chake kitaendelea kufatilia hatua kwa hatua ili serikali iweze kutekeleza mazimio ya baraza la wawakilishi kwa waliohusika na wizi kuwajibishwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Sambamba na hilo Aidha alisema serikali inapaswa kuweka wazi kiasi cha fedha asilimia nne (4.5%) zinazopatikana kila mwaka katika serikali ya jamhuri ya Muungano pamoja na matumizi yake.

Chama cha Demokrasia kimetoa pongezi kwa kamati teule ya baraza la wawakilishi iliyotoa tarifa za uchunguzi wa matumizi mabaya ya madaraka na ufujaji wa fedha za wananchi iliyotolewa mbele ya baraza la wawakilishi.

Aidha ametoa wito kwa Baraza la wawakilishi kuendelea kuisimamia na kuielekeza serikali ianzishe uchunguzi maalum kutokana na ubadhilifu unaofanyika katika tasisi muhimu za umma na sekta za umma.

No comments: