Wednesday, February 6, 2013

Eto’o, Song kuikosa Stars leo

Wachezaji wa timu ya soka ya taifa ya Cameroon wakiwa mazoezini Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo, kujiandaa na mchezo wa kesho wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.( picha na Bin Zubeiry Blog)
Nyota wa klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi, Samuel Eto’o na Alex Song wa Barcelona ya Hispania hawatakuwamo katika kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon kitakachocheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo kutokana na majeraha, imefahamika.

  
Taarifa iliyoripotiwa jana katika tovuti ya Cameroon (cameroononline.org), ilieleza kwamba Eto’o (31) ambaye alitolewa katika mechi ya kirafiki ya klabu yake Jumamosi dhidi ya Dynamo Kiev ya Ukraine yuko shakani kucheza dhidi ya Stars kutokana na maumivu ya mgongo.

Tovuti rasmi ya klabu ya Barcelona iliripoti vilevile kuwa kiungo Alexander Song (25) hatakuwamo katika kikosi cha Cameroon kutokana na jeraha la goti.

Hata hivyo, Cameroon itakuwa na wakali wake kibao kama Fabrice wa Malaga ya Hispania, Achille Emana wa Al Ahly (UAE), mshambuliaji Vincent Aboubakar wa Valencienne ya Ufaransa na kipa Charles Itandje anayecheza soka la kulipwa nchini Ugiriki.

Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa Stars, Kim Poulsen, alisema kuwa kikosi chake kiko tayari kuwavaa Cameroon inayoundwa na wachezaji nyota na wenye uwezo na uzoefu wa kucheza katika ligi kuu mbalimbali za Ulaya.

Poulsen alisema kuwa wamefanya maandalizi mazuri na wako tayari kuonyesha soka la kiwango cha juu.

"Tunatarajia kukutana na wachezaji wenye uwezo dhidi yetu na hiyo ni fursa nzuri ya kuona ni kwa namna gani wachezaji wetu watakabiliana na changamoto hiyo," Kim alisema.
Nahodha wa Stars, Juma Kaseja, alisema kuwa wamejiandaa vizuri na malengo yao ni kuwapa Watanzania furaha, ingawa alikiri kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu.

Kaseja alisema kwamba wachezaji wanafahamu walichoelekezwa na wanaamini watatekeleza yale waliyofundishwa.

Kocha wa Cameroon, Jean Paul Akono, alisema kwamba amefurahi kupata sasa mechi dhidi ya Stars na kwamba, katika dunia ya sasa hakuna timu ndogo wala kubwa.

Akono alisema kuwa anaamini Stars itaipa timu yake maandalizi mazuri ya kuivaa Togo na Watanzania watarajie kuona soka la kuvutia.

Aliongeza kwamba wanaiheshimu Stars kwa sababu nao wapo kwenye maandalizi ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia (watakayocheza mwezi ujao dhidi ya Morocco) na hivyo mechi hiyo itakuwa na ushindani nkali.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2008 na Stars ililala ugenini 2-1 na waliporudiana nchini walitoka sare ya 1-1.

Wakati huo huo, meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager inayoidhamini Stars, George Kavishe aliwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi leo kuishangilia timu yao ili ipate matokeo mazuri dhidi ya Cameroon.
CHANZO: NIPASHE

No comments: