Msafiri Jeremia akiwa na mkewe Monica Daniel.
NDOA ya Msafiri Jeremia na Monica Daniel, wakazi wa Kijiji cha Munisagale,Wilaya ya Kilosa mkoani hapa imekuwa ya mateso baada ya mume kupata ajali na kupoteza mkono na mguu.
Hayo ni maneno ya baadhi ya wanakijiji wa Munisagale waliyoyatoa kwa nyakati tofauti mbele ya mwandishi wetu huku wakiwa na majonzi wakidai kwamba tangu mwaka 2000, Jeremia alipopata ajali ya treni na kukatwa mguu na mkono, familia hiyo imekuwa ikiishi maisha ya dhiki huku Monica akibeba jukumu la kuilisha.
Jeremia alipohojiwa na gazeti hili alisema akiwa kwenye hekaheka za kutafuta riziki ndipo alipopata ajali iliyomtia kilema cha maisha.
“Ajali ya treni iliyotokea mwaka 2000 katika Kijiji cha Msagali mkoani Dodoma, mimi nilikuwemo ambapo nilikatwa mguu na mkono na tangu kipindi hicho maisha yangu ni ya tabu kwani jukumu la kulea familia limekuwa la mke wangu ambaye hufanya vibarua vya kulima, akikosa tunalala na njaa na watoto wetu wawili,” alisema Jeremia.
Akaongeza: “Kama unavyotuona tumekuja kuchapa barua ya kwenda kwa waziri mkuu nikiomba anipatie msaada wa mguu bandia, inatakiwa na picha inayoonyesha jinsi nilivyokatwa viungo, fedha ya kupiga picha sina, tulikuwa na elfu mbili tu, hivyo tumeweza kununua soda ndogo na biskuti.”
Mke wake alikuwa na haya ya kusema: “Namshukuru Mungu kwa kumnusuru mume wangu na kifo kwenye ajali hiyo kwani wengi walikufa lakini baba watoto wangu alinusurika na kukatika mguu na mkono, hayo ni mapenzi ya Mungu.
“Naamini hapa duniani kila mtu ni mlemavu mtarajiwa na kama walivyosema wahenga kwamba kabla hujafa haujaumbika, haya yaliyomkuta mume wangu yanaweza kumkuta yeyote hata mimi.
“Familia yetu tuna watoto watatu, Simon (20), Thomas (17) na Magreth (13) hawa wawili wamemaliza shule huyu wa mwisho kutokana na gharama kubwa za shule tumeshindwa kumsomesha kwa sababu ya ukata,” alisema Monica.
Mwandishi wetu aliamua kumpiga picha bure na akaziambatanisha katika waraka wake wa kwenda kwa waziri mkuu kitengo cha maafa ambapo kwa sasa wanasubiri majibu ya barua hiyo.
Mtu aliyeguswa na habari hii anaweza kumsaidia Jeremia kwa kuwasiliana naye kwa
namba +255715 289 073.
No comments:
Post a Comment