Thursday, February 14, 2013

Kada CCM akamatwa na shehena ya sukari mbovu


  Ni tani 100 hutumika kutengeneza ARV
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ramadhan Madabida.
Manispaa ya Temeke, mkoani Dar es Salaam imekamata shehena ya sukari nyeupe (industrial white sugar) mbovu ambayo hutumika kutengeneza dawa za kupunguza makali ya ukimwi (ARV’s) ambayo inamilikiwa na kiwanda cha kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ramadhan Madabida.

Shehena hiyo ambayo ni tani 100 za sukari zilikamatwa kwenye ghala maeneo ya Chang’ombe jijini Dar es Salaam zikiwa zinatolewa kinyemela kupelekwa Arusha tayari kwa matumizi.
Vyanzo vya uhakika viliiambia NIPASHE jana kwamba sukari hiyo hutolewa kwa usiri mkubwa kwenye ghala hilo lililopo barabara ya Mbozi-Chang’ombe na kwamba huwa halifunguliwi mchana au mara kwa mara.


Taarifa hizo zilidai kwamba inakadiriwa juzi takribani tani 10 za sukari hiyo ambayo imekwisha muda wake wa matumizi zilikuwa zinatolewa. Kufuatia mwenendo wa utoaji wa bidhaa kwenye ghala hilo, raia wema walianza kufuatilia na kubaini kwamba ni sukari ambayo inamilikiwa na kada huyo.

“Jana (juzi), tukaona malori yamekwenda pale kama kawaida kuchukua mzigo, sisi tukawasiliana na viongozi wa kata kuwaeleza waje wakague kama kweli bidhaa zinazotoka huku ni salama…alikuja bwana afya, polisi pamoja na viongozi wengine,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilieleza kwamba wakati Bwana Afya akiwa kwenye ghala hilo, alipigiwa simu na baadhi ya viongozi wa CCM wakimtaka kutochukua hatua zozote kwa kuwa suala hilo litampotezea kazi.

Mmoja wa viongozi hao ni Diwani wa Kata mojawapo ya Manispaa ya Temeke, ambaye alimweleza kwamba ghala hilo linamilikiwa na mmoja wa viongozi wa CCM wanaoheshimika hapa nchini.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Naibu Mkurugenzi wa kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI), kinachotengeneza ARV’s, Zarina Madabida, alisema: “Nipo safarini subiri nikifika nitakujulisha.”

Hata hivyo, NIPASHE ilimwandikia ujumbe mfupi wa mkononi kumsisitiza kuhusu umuhimu wa kauli yake kwa suala hilo na ndipo alipopiga simu na kuhoji:
“Hivi unaona hiyo ni habari?”

NIPASHE ilipomwambia ni kwa ajili ya manufaa ya umma alisema: “Ni kweli kuna sukari ambayo imeharibika tangu mwaka jana, tulikuwa tunaipeleka kiwandani Arusha ikakae tu kule.”

Zarina ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), alisema: “Najua aliyekupa hiyo taarifa ni mtu mmoja ambaye alitaka nimuuzie kwa magendo, hiyo sukari nikakataa…kama unataka kuiandika utakuwa umenisaidia sana na utaisadia pia serikali japokuwa sioni kama ni habari.”

“Hayo ndiyo madhara ya serikali kufunga kiwanda, ni kweli haifai kutengeneza dawa, lakini inaweza kutumika kwa matumizi mengine,” alisema Zarina.

Hata hivyo, alisema hajui kiasi cha sukari hiyo na wala mwezi ambao imemalizika muda wake wa matumizi.

Badala yake alisema: “Nipo njiani naenda Mbeya na Kamati ya Bunge, nitarudi Jumapili ukinitafuta Jumatatu nitaweza kukueleza kwa undani suala zima.”
NIPASHE ilipomtafuta Bwana Afya wa Kata ya Chang’ombe ambaye alifunga ghala hilo, Mohamed Mrindoko, alithibitisha kufunga ghala hilo na kueleza kwamba bado jambo hilo lipo kwenye uchunguzi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: