Mamia ya majumba ya kifahari kuvunjwa Dar
Mkurugenzi wa Utekelezaji na Usimamizi wa Nemc, Dk. Robert Ntakamulenga, alisema kabla ya operesheni ya kuzibomoa nyumba hizo, itaanza kazi ya upimaji wa mto huo.
Alisema kazi hiyo inalenga kuzibaini nyumba zilizopo ndani ya mita 30 kuanzia mto huo.
Dk. Ntakamulenga alisema Sheria ya Mazingira ya 2004 kifungu cha 55 inazuia mtu yeyote kujenga majengo ya makazi au biashara ndani ya mita 60 kutoka ukingo wa bahari, mto au ziwa.
Alitaja maeneo yatakayoathirika na bomoa bomoa hiyo kuwa ni ya makazi ambako mto huo unapita.
Maeneo hayo ni Kawe, Makongo Juu, Msasani, Bonde la Mpunga, Mlalakuwa na Mzimuni. Alisema bomoa bomoa hiyo inalenga kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi ifikapo mwaka 2015.
Dk. Ntakamulenga alisema kazi ya upimaji wa mto huo itaanza leo na itafanywa na mkandarasi, Mhandisi Nanai Nanai, kutoka kampuni ya Kimsons Limited na itafanyika kwa siku 30.
Alisema kazi hiyo itakuwa endelevu kwa mito yote iliyopo jijini Dar es Salaam kwa kuwa zaidi ya asilimia 75 wanaishi katika maeneo, ambayo hayajapimwa.
“Sheria za mipango miji hazifuatwi. Viwanja vingi havijapimwa. Kwa sasa tunaanza kazi na wakazi waliojenga kandokando ya mto Mlalakuwa. Wakazi walioko katika mito mingine wajiandae kwa kuondoka wenyewe,” alisema Dk. Ntakamulenga.
Alisema katika upimaji huo, watazingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2002 ya kubomoa nyumba zilizomo ndani ya mita 30 kwenda kushoto na mita 30 kwenda kulia. Dk. Ntakamulenga alisema suala la ulipaji fidia kama litakuwapo au la litatolewa ufafanuzi na serikali hapo baadaye.
Alisema baada ya kazi ya upimaji kukamilika, kikosi kazi kitafuata na kuweka alama ya `X' kwenye nyumba zinazotakiwa kubomolewa pasipo upendeleo wowote. Dk. Ntakamulenga alisema hata ukuta wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kama upo ndani ya mita 30, pia utabomolewa.
Alisema mto huo umevamiwa na viwanda vinavyotoa maji machafu pamoja na makazi ya watu kuelekezea mabomba ya maji machafu jambo ambalo alisema linatishia mto kukauka na kutoweka kabisa.
“Mito imegeuka kuwa dampo la takataka. Kila mtu anatupa takataka ovyo. Hali ni mbaya katika mito yote iliyopo Dar. Hivyo, tunaanza na mto Mlalakuwa na mingine itafuata,” alisisitiza Dk. Ntakamulenga.
Mwanasheria wa Nemc, Manchare Heche, alisema wakazi wengi wa jijini Dar es Salaam, si watiifu wa sheria.
Alisema Sheria ya Mazingira na ile ya mipango miji zitatumika katika kuwahamisha wakazi wote waliojenga kando kando ya mto huo.
Heche alisema Sh. milioni 75 zimetolewa na kampuni ya Coca Cola na GIZ ya Ujerumani kufanikisha kuusafisha mto huo. Aliwataka wakazi waliojenga kando kando ya mto huo kubomoa wenyewe kabla nguvu ya serikali haijatumika.
Naye Mhandisi Nanai, alisema kazi kubwa itakayofanyika leo ni kuweka alama zinazoonyesha mwisho wa kingo za mto huo. Bomoa bomoa kama hiyo iliwahi kufanywa na Nemc dhidi ya nyumba zilizojengwa kando ya mito ya Mbezi Beach, Mindumbwe na eneo la Hifadhi ya Mikoko, jijini Dar es Salaam, Julai, mwaka jana.
Nyumba hizo zilibomolewa katika operesheni ambayo ilihusisha Wizara ya Maliasili na Utalii na kusimamiwa na askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU). Hatua hiyo ilichukuliwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa tamko la Makamu wa Rais la mwaka 2004, ambalo lilitaja maeneo tengefu ambayo yalipaswa kuhifadhiwa, zikiwamo fukwe za bahari zenye mikoko ambayo ni mazalia ya samaki baharini.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment