Muda huu gazeti lako ulipendalo la Championi Ijumaa likiwa mkononi, sitaki kuzungumza sana bali naianzisha mada yetu mara moja kama inavyosomeka hapo juu: Kuogopa maradhi ni kigezo cha uaminifu? Swali kama hili ukimuuliza mtu, nina imani utapata majibu mengi.
Kwa mfano, leo dawa ya Ukimwi ikitangazwa imepatikana, nina imani itakuwa shangwe na vigeregere si kwa waathirika tu, bali hata ambao hawajaathirika, hii inatokana na nini? Uzito wa ugonjwa wenyewe au aibu impatayo mtu pale anapojua ameathirika na kumuona mtoa roho yupo mbele yake? Jibu unalo.Watu bado wana ufahamu mdogo kuhusu Ukimwi, lakini navipongeza vyama vyote vya ushauri nasaha kwa kuwa mstari wa mbele kuwaeleza wananchi kuwa ugonjwa huu ni kama maradhi mengine.
Najua watu wameshaanza kuniona nimeingia katika ushauri nasaha, la hasha, japo kila mtu ni mwalimu kwa lile analolielewa. Bora kuwaelimisha wengine na kuwafanya wasiwe na wasiwasi wa kwenda kupima kwa hiyari na kupokea majibu yoyote bila hofu yoyote.
Kwa vile mada ya leo imelenga huko, lazima nianze na maelezo mafupi ili twende pamoja. Kilichosababisha niandike mada hii ni ujumbe mwingi ambao nimewasikia watu wakiwatumia wapenzi wao, hasa katika salamu za lala kwa unono au kuwakumbuka muwapendao.
Utamsikia mtu akimsalimia mpenzi wake na mwisho kutoa ujumbe usemao: “Namuomba mpenzi wangu awe mwaminifu kwa sababu maradhi ni mengi.”
Ninyi nyote mnaowaasa wapenzi wenu wawe watulivu au waaminifu kwa kuhofia ugonjwa usio na dawa, je, kama Ukimwi usingekuwepo mngewaruhusu watoke nje?
Najua jibu litakuwa hapana, lakini imeonyesha jinsi gani watu wanavyouogopa ugonjwa wa kuambukizwa kwa njia ya kujamiiana kuliko usaliti katika mapenzi.
Hii inamaana kuwa kama ugonjwa huu usingekuwepo, pengine wengi wangewaruhusu wapenzi wao watoke nje ya ndoa.
Nia kubwa ya kuandika mada hii ni kutaka kuelezea umuhimu wa uaminifu katika mapenzi bila kuangalia mpo kwenye kipindi gani au katika hali gani.
Unapompokea mwenzio moyoni mwako na kuamua kuwa naye, ni wazi umewaona wengi lakini moyo wako umeangukia kwa huyo ambaye ndiye chaguo lako.
Ni kweli kuna baadhi ya maradhi hayana dawa, lakini jambo la msingi ni uaminifu, tofauti na hapo ni kujaribu bila uhakika. Lakini upendo wa dhati na huruma kwa mpenzi wako, ndiyo njia pekee ya kujilinda na magonjwa ambukizi kwa njia ya kujamiiana.
Siku zote tamaa za kuonja kila chungu ndiyo sababu inayomfanya mtu kula hata visivyoliwa.Ukimwi ubakie kama ugonjwa lakini uaminifu ndiyo njia pekee ya kujiepusha na yote hayo.
Mwisho, namalizia kwa kusema, tangu upendane na mpenzi wako na kuufanya mwili kuwa mmoja, fahamu umebeba uhai wa mwenzio, ni wewe wa kumlinda na wewe ndiye wa kumuangamiza.
Nategemea ujumbe wa mada hii fupi utakuwa umeeleweka na kuwafanya wote walioifungua mioyo yao kwa ajili ya wenzao, wasiwe sehemu ya maumivu yao.
Uaminifu na huruma kwa mwenzio ndiyo njia pekee ya kuwaepusha na wasiwasi wa mioyo yenu. Aliyepata Ukimwi ni bahati mbaya, lakini ugonjwa huo si laana, bali ni kama ugonjwa mwingine. Kwa kufuata maelekezo, maisha yako ni zaidi ya yule anayejiamini.
Kwa haya machache tukutane wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment