Thursday, February 21, 2013

Lowassa: Sikutoswa UVCCM

Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amesema kuwa aliomba mapema kutoendelea na wadhifa wa uenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kinyume cha taarifa ya kwamba ameondolewa.

Lowassa alisema kuwa aliwaambia viongozi wa UVCCM kwamba asingependa kuendelea na wadhifa huo aliokuwa nao kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi.

Katika kikao chake cha hivi karibuni mjini Dodoma, Baraza Kuu la UVCCM lilimteua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi, kuchukua wadhifa huo.

“Niliwaambia nisingependa kuendelea, baada ya kufanikisha ndoto yangu ya kuona Umoja wa Vijana unajitegemea,” alisema Lowassa jijini Dar es Salaam jana huku akijivunia ujenzi wa jengo la umoja huo lilikoko barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Lowassa, Umoja wa Vijana hivi sasa una mradi mkubwa wa jengo refu na kuwa hayo ni mafanikio makubwa kabisa.

Alisema kuwa katika miaka ya nyuma kuna baadhi ya watu waliosema kuwa kulikuwa na harufu ya rushwa kwenye mkataba wa jengo hilo, lakini hakuna mkataba bora kama huo kwa kuwa UVCCM itakuwa inalipwa Dola 50,000 (Sh. milioni 80) kwa mwezi na kuongea kuwa fedha hizo zitaufanya umoja huo kujilipa mishahara pamoja na gharama nyingine.
Lowassa alisema kutokana na mkataba huo ambao umoja huo ulitiliana na kampuni ya Espirit Developer Ltd ya jijini Dar es Salaam kujenga jengo hilo, sasa UVCCM inajitegemea.

Alieleza kuwa hayo ni mafanikio makubwa na hiyo ndiyo ilikuwa ndoto yake huku akiwashukuru waliokuwa wajumbe wenzake kwa kazi nzuri.

Aidha, aliwashukuru vijana waliowaamini ambao kwa sasa wanayaona mafanikio hayo.
“Nimetimiza ndoto yangu ya kuona umoja huo unakuwa mfano kwa jumuiya nyingine. Nawaomba wanielewe kuwa mimi ni mtumishi nisiye na faida, nimeyafanya yale tuliyopaswa kuyafanya,” alisema.

Jumatatu wiki hii, UVCCM ilisema mbali na Lowassa, pia imemuondoa mjumbe mwingine ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji) na Mbunge wa Hanang, Dk. Mary Nagu.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela, alisema kuwa Baraza Kuu lililoketi kwa siku mbili limemteua Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwa mwenyekiti mpya wa baraza hilo.

Wengine walioteuliwa kuwa wajumbe ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge) na Mjumbe wa Kamati kuu (CC), William Lukuvi; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Profesa Anna Tibaijuka.

Wengine ni Naibu Waziri wa Fedha, na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), Janeth Mbene; Mbunge wa Kikwajuni ambaye pia ni mjumbe wa Nec, Hamad Yusuf Masaun na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mohamed Abood ambaye pia ni mjumbe wa Nec na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Baraza la zamani la wadhamini mbali na Lowassa na Dk. Nagu, wajumbe wengine walikuwa ni Lukuvi; aliyekuwa Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi; Hemed Yusuf Ahamed na Said Amour.

Shigela alisema baraza hilo ndilo litakuwa wasimamizi wa mali zote za umoja huo na kwamba wameona waingize damu ya vijana katika dhana nzima ya kujitegemea kama jumuiya.
Shigela pia alisema kuwa wajumbe wengine wameteuliwa kwa lengo la kuisaidia jumuiya hiyo kutokana na utaalamu wao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: