ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 19, 2013

Maafisa tume wafunzwa stadi za uchunguzi


Na Mbaraka Kambona, Arusha

Maafisa uchunguzi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wanahudhuria mafunzo ya stadi za uchunguzi juu ya taasisi za umma na binafsi kuhusu uvunjwaji wa misingi ya utawala bora.
Mafunzo hayo ya wiki mbili kuanzia februari 18 hadi februari 28 yanafanyika katika hoteli ya Palace Arusha iliyopo jijini Arusha na yanaendeshwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi kwa kushirikiana na Center for International for Legal Cooperation (CILC).
Wakufunzi katika mafunzo hayo ni Paul Brookes,Mkurugenzi wa Utafiti na Nyaraka wa tume,Bi.Epiphania Mfundo, Profesa Martin Kuijer na Steven Mubiru.
Akifungua mkutano huo,Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Mhe.Jaji Kiongozi(mstaafu)Amiri Manento alisema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwaongezea stadi za uchunguzi maafisa hao ili waweze kufanya uchunguzi wao kwa ufanisi na kwa wakati pamoja na kupata wakufunzi.
‘’Mafunzo haya yatawawezesha maafisa uchunguzi kutofautisha masuala ya kiuchunguzi yanayohusu taasisi za umma na zile za binafsi’’,alisema
‘’Hivyo ni ni matumaini yangu mafunzo haya yatawapa vitendea kazi bora vitakavyowawezesha kutimiza malengo ya tume kwa wakati’’,aliongeza
Aidha,aliwakumbusha washiriki kuwa Tume imepewa mamlaka makubwa ya kikatiba na kisheria ya kuhamasisha,kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.
‘’kwa mamlaka haya,ni wazi kuwa Tume ina jukumu kubwa la kulinda watu dhidi ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora’’,alisistiza
Ubalozi wa Uholanzi nchini pamoja na Tume walikubaliana kufanya mafunzo haya kwa pamoja ili kukuza ujuzi na stadi za kiuchunguzi wa kwa maafisa wa Tume ili kuwaongezea uwezo wakati wa kutekeleza majukumu yao.

No comments: