ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 11, 2013

MAKUNDI YA WANAUME NA MITAZAMO YAO YA KIMAPENZI KWA WANAWAKE-3


KWA kuanzia pale nilipokomea wiki iliyopita ni kwamba wanaume wanaounda kundi la kwanza (nililichambua matoleo mawili yaliyopita), mara nyingi ni sawa na mabomu ya sumu linapokuja suala la mapenzi.
Kwao, tafsiri ya mapenzi huishia katika eneo la kuitana majina mazuri, kutumiana zawadi na maonesho. Akilini kwao huzingatia mwanamke ambaye akionekana naye, watu watamuona mjanja.
Kwa kawaida hawana uamuzi wa kwao wenyewe. Huishi kimapenzi kwa kutazama watu wengine wanawaangaliaje. Hiyo ndiyo sababu ya kukita akili zao kwenye eneo moja tu kwamba lazima wawe na wapenzi ambao watawafanya waonekane ni vijana wa kisasa.
Kutokana na jinsi wanavyojiweka, mara nyingi inakuwa ngumu kwao kujenga familia bora. Siyo wanaume wazuri kama mwanamke anakuwa anahitaji mwanaume wa kujenga naye maisha. Ni wanaume sahihi sana kama unataka mapenzi ya ujana na kuendekeza kujirusha.
Kipindi ambacho uchumi umekaa vizuri, anaweza kudumisha upendo mpaka ukamuona ni mwanaume bora zaidi duniani. Tatizo ni kwamba hawaaminiki hasa pale inapotokea kuyumba kwa hali ya kifedha. Hawana uwezo wa kuvumilia shida, maisha yao yamejaa deko.
Utampa mapenzi yote lakini akiona mwanamke mwenye fedha atakusaliti. Ni tabaka la watu wasiojali sana hisia za mapenzi pale wanapopendwa. Wewe utaumia lakini yeye hatazingatia chochote. Daima matarajio yao huwa ya mkatomkato.
Tatizo kubwa ambalo linawaandama wanaume wa kundi hili ni hulka yao ya kutoka kimapenzi na wanawake wengi. Kwao ni sifa njema kuwa na idadi kubwa ya wapenzi. Tena hukaa na marafiki zao kujisifu kwa maneno, ‘yule tayari’, ni tabia mbaya sana.
Hii hutokana na aina ya maisha ambayo wao wenyewe wanakuwa wameamua kuishi. Huwezi kuwa mtu wa klabu, ukawa fundi wa kuchagua wanawake wa viwanja halafu usiwe na idadi kubwa. Mapenzi ya viwanja hayadumu ndiyo maana kwao, kuwa na wapenzi wengi ni fasheni.

BAHATI MBAYA
Pamoja na ukweli kwamba wanaume wa kundi hili ni wasaliti ila nao wanayo bahati mbaya moja kubwa ambayo ni kusalitiwa na wanawake. Sababu ni kuwa wanawake ambao humulikwa na wanaume wa kundi hili huwa na kiburi.
Wanawake hao (wale wa viwanja), hujiamini wao ni lulu inayogombewa kwamba ni wazuri na wanapendwa sana, kwa hiyo hukosa msimamo na utulivu wa kweli. Siyo ajabu mgogoro mdogo, mwanamke akatamka “usinitishe!”, kwa vile na mwanaume wa kimjinimjini, hatataka kunyenyekea. Mwisho wataachana.
Kwa vile wanawake wa kundi hili hupenda kulelewa na kutaka zaidi fedha, hutoka na wanaume wengine ambao wataonekana wana fedha zaidi. Kadhalika, hujiona wao ni tabaka maalum sana, kwa hiyo huwa wanataka wanyenyekewe hata kama ni kwa jambo ambalo linawahitaji kunyenyekea.
Wenye tabia ya kupenda wanawake kutokana na muonekano na aina ya wana viwanja wapo wengi, kwa hiyo unaweza kupenda kesho yake asubuhi mwingine naye akamtaka mwanamke huyohuyo wa kwako, hivyo kuleta ushindani wa kimaslahi.

KUNDI LA PILI
Kuna wanaume ambao hawajui kushukuru hata wafanyiwe kitu gani. Hawa ndiyo wanaunda kundi hili la pili ambalo linatokana na wale wenye tabia ya kutazama maslahi kwanza kabla ya kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Unaweza kushangaa mtu anakutana na warembo ambao wapo singo lakini hajishughulishi nao, badala yake anapoona wake za watu akili inamtoka. Tatizo kubwa lililopo ndani yake ni kwamba anakimbia majukumu. Hawezi kuhudumia.
Atatokea mrembo anayetazamika hasa. Atampa mapenzi yote lakini hataridhika kwa hilo. Atakachokifanya ni kuhamishia uhusiano wake kwa mwanamke mwenye fedha ili apate kuchota noti za benki kuu. Siku zote ni wasafi na hujiweka kwenye muonekano wa kati.
Si kila mke wa mtu anaweza kumtolea macho. Kuna vipimo huvizingatia, kama vile anapomuona mwanamke anaendesha gari, pengine amechakaa madini shingoni na mikononi na kadhalika.

Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: