Advertisements

Thursday, February 21, 2013

Mwakyembe akutana na uongozi wa Tazara Zambia

Dk Mwakyembe
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harisson Mwakyembe inasemekana kuwa jana aliwasili nchini Zambia kwa ajili ya mkutano na uongozi wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (Tazara) kwa lengo la kukutana na viongozi mbalimbali katika kutathimini utendaji kazi ndani ya mamlaka hiyo.

Akithibitisha kuwasili kwa Waziri Mwakyembe nchini humo, Ofisa habari wa mamlaka hiyo, Regina Tarimo alisema ni kweli viongozi hao wamekutana na Waziri Mwakyembe katika mkutano wa pamoja.
Hatua hiyo imefuatia baada ya Dk Mwakyembe
kuwaahidi wafanyakazi wa mamlaka hiyo kutafuta sababu za matatizo yanayoikabili mamlaka hiyo itakayosaidia kuziondoa kwa upande wa Tanzania.

“Ni kweli leo (jana) wamekutana wote kuanzia menejimenti, Bodi ya Wakurugenzi na Waziri wa Mawasiliano na Usafirishaji wa Zambia, Yamfwa Mukanga kama jinsi alivyoahidi siku ya mkutano na wafanyakazi,” alisema Regina.
Regina aliongeza kuwa kuhusu taarifa za kuwasilishwa kwa ripoti za uchunguzi ndani ya mamlaka hiyo kwa upande wa Tanzania bado haijafahamika rasmi mpaka pale watakapotumiwa taarifa hizo kutoka Zambia.

“Kuna kamati zilizokuwa zinafanya kazi ya ukaguzi wa majukumu kwa Dar es Salaam na zilitakiwa kukabidhi ripoti zake ila haijafahamika rasmi mpaka pale watakapozituma kutoka Lusaka,” alisema Regina.

Hata hivyo Msemaji wa mamlaka hiyo kutoka nchini Zambia, Cosmas Simuchile aliliambia gazeti hili kuwa, kamati hizo zilitakiwa kukabidhi ripoti za ukaguzi huo Februari 18, mwaka huu.

Hivi karibuni akizungumza na wafanyakazi hao, Dk Mwakyembe alitoa ahadi ya kusafiri kwenda nchini Zambia ambapo atakutana na uongozi wote ili kutathimini maagizo waliyoagiza katika bodi hiyo kama yalitekelezwa ipasapavyo.

Dk Mwakyembe aliahidi mbele ya wafanyakazi hao kutoendelea kufanya kazi na Mkurungenzi wa mamlaka hiyo, Akashambatwa Lewanike na kuiomba mamlaka impatie kaimu atayeshika nafasi hiyo kabla ya kumalizika kwa ukaguzi.

Alisema mbali na mkurugenzi huyo, bodi ya mamlaka hiyo ilishindwa kutekeleza agizo walilokuwa wamepewa ikiwa ni pamoja na kuwashughulikia maofisa saba wa ngazi za juu katika mamlaka hiyo.

Dk Mwakyembe alisema mbali na suala hilo kuwa mahakamani,bodi ilikuwa na mamlaka ya kuchunguza na kujiridhisha juu ya uhalali wa watumishi hao kuendelea na kazi lakini hata hivyo hawakutelekeza hivyo.

“Bodi yote haifai, haiwezekani mtu ana kesi na iko mahakamani lakini anaendelea kula mshahara, tuliwaagiza wajiridhishe na wafanyakazi hao kama wahafai waondolewe kuliko kuendelea kutia hasara, lakini haikutekelezwa,”alisema Dk Mwakyembe.
Chanzo:Mwananchi

No comments: