Rafiki zangu tunaendelea na mada yetu ambayo safari hii imekuwa ndefu sana. Bila shaka kuna kitu umevuna na utaendelea kupata kupitia somo hili zuri. Bila kupoteza muda, naona nianzie pale nilipoishia wiki iliyopita.
Nilizungumzia suala la kuharakisha mapenzi. Ni kweli kuna ugumu katika kipengele hiki hasa kwenye dunia tuliyonayo lakini asikudanganye mtu, ukiweza kusimamia kipengele hiki, thamani yako itapanda maradufu na kudumu kwa mpenzi wako
Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba, wanawake ‘wagumu’ zaidi kukubali kutoa tendo la ngono au kukataa kabisa mpaka ndoa, huwa na nafasi kubwa zaidi ya kuingia kwenye ndoa.
Mtaalamu wa Saikolojia katika Uhusiano na Ndoa, Dk. Dennis Robbinson wa Uingereza, anaeleza katika kitabu chake cha Love & Life (Mapenzi na Maisha) kuwa wanaume ‘waoaji’ huvutiwa zaidi na wanawake ambao ni wagumu kukubali kuachia miili yao ichezewe na wanaume.
“The main point here is individualism; men like to have women to themselves only without sharing with anybody. To them, having easily accepted for making love means even if they marry such women, they could be easily giving love out of marriage than those who hardly accept such approaches or those who completely refuse such approaches,” anaeleza Dk. Robbinson katika sehemu ya kitabu hicho.
Kwa tafsiri isiyo rasmi, Dk. Robbinson anasema, hoja kubwa (katika suala la kuharakisha mapenzi) ni ubinafsi; wanaume wanapenda kuwa na wanawake wao peke yao bila kuchangia na mtu. Wanaamini kukubaliwa haraka faragha humaanisha kuwa hata wakioa ni rahisi zaidi wanawake hao kutoa penzi nje ya ndoa kuliko wale wagumu au wanaokataa kabisa.
Wakati fulani niliwahi kukutana na msichana mmoja ofisini kwangu akihitaji ushauri. Jambo lililokuwa linamsumbua ni kichekesho. Alikuwa akilalamilikia kitendo cha mpenzi wake (rafiki tu) kukataa kupokea simu na kujibu meseji zake, wakati mwingine akifanya hivyo huwa kwa kuchelewa sana.
Alisema kwamba, kinachomshangaza zaidi (eti) hata anapomhitaji mwanaume wake faragha humpiga chenga. Anaamini tendo la ngono kwa rafiki yake ni halali yake na akilikosa ni sawa amedharauliwa!
Nilimshangaa sana, lakini ilibidi nifanye kazi yangu ipasavyo. Nilitumia saa mbili kuzungumza naye. Alinieleza mengi, lakini kikubwa ni kwamba, yule bwana alimshamchoka! Dalili zote zilionesha kwamba, hakufikirii kuwa naye katika ndoa kama alivyokuwa akiwaza mwanzoni.
UMEJIFUNZA KITU?
Wepesi wa kutoa penzi na kujiachia na mwanaume ambaye hajakuoa huhatarisha nia ya ndoa. Ikumbukwe kwamba, si kila mwanaume anafaa kuwa mume na si kila mwanamke ni mke. Utajuaje uliyekutana naye kama ndiye au siye? Ni fumbo.
Wengine wanahamia kabisa kwa wanaume au wanakwenda weekend kufua na kufanya usafi wa nyumba. Ni makosa makubwa. Unadhani ataharakishia ndoa ya nini wakati kila kitu anapata? Amka dada yangu, tupo kwenye dunia nyingine.
SIKIA HUU USHAHIDI
Kijana mmoja ambaye hapa nitamtaja kwa jina moja la Jully, alinifuata kunitaka ushauri. Yeye anasema amejikuta amepoteza msisimko kwa mpenzi wake aliyedumu naye kwa miaka minne na anataka kumuacha ili aoane na mwingine.
Jully anasema: “Sikufichi kaka Shaluwa, nilimpenda sana Sarafina lakini sasa nahisi kama sikuwa sahihi kuwa naye. Kwanza ni mwepesi...hakunisumbua sana wakati namfuatilia, mbaya zaidi ameshatoa mimba zangu nne, wanini mwanamke kama huyo?”
Nilipomwuliza kuhusu mwanamke anayetaka kumuoa alisema: “Huyu anaitwa Veronica, nilikuwa naye kabla ya Sarafina. Wakati huo alikuwa sekondari, amemaliza UD mwaka jana (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam). Ana msimamo hatari! Mpaka ninavyozungumza na wewe hajawahi kunipa penzi na mpaka sasa amenithibitishia kwamba bado ana usichana wake. Kwa nini nisimuoe mwanamke huyu mzuri, anayejitambua na kujitunza? Hawezi kunisumbua kwenye ndoa yangu kama Sarafina.”
WANAWAKE MPO?
Kwahiyo mmeona kumbe wanaume japo wanawalaghai muwape penzi haohao ni hodari wa kuwasema vibaya na kuwashusha thamani wakati wakiwaza kuhusu ndoa. Ni vizuri wanawake mkaamka na kujitambua na kufahamu thamani mliyonayo.
Acha kudanganyika, penzi si kigezo cha upendo wa dhati. Mbona mambo yako wazi tu! Kama anakupenda atume wazee nyumbani kwenu, taratibu muhimu zifanyike, uolewe kwa heshima na thamani yako ikiendelea kuwa juu. Mwanaume wa aina hiyo ni vigumu kukutesa.
EREVUKA
Kusoma mada hii ni kitu kimoja lakini kuelewa na kubadilika ni kitu kingine. Badili utaratibu wa maisha yako huku ukizingatia kupandisha thamani ya utu wako.
Mada ni ndefu lakini ina mafunzo makubwa katika maisha ya uhusiano. Uvumilivu wako ni muhimu sana, wiki ijayo nitakuwa hapa kuendelea na darasa hili, USIKOSE!
GPL
No comments:
Post a Comment