Thursday, February 14, 2013

NHC kuwatimua wapangaji wasio na mikataba



Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limewapa mwezi mmoja watu waliopanga kwenye nyumba zake, ambao mikataba yao imeisha au wasiokuwa na mkataba, kupata mkataba, vinginevyo watatolewa kwenye nyumba walizopanga na kupangishwa watu wengine.
 
Pia, limewapa miezi mitatu watu waliopanga kwenye nyumba za shirika kinyume cha taratibu kujitokeza wapewe upangaji moja kwa moja ili kuhalalishwa ukaaji wao katika nyumba hizo.
 
Mkurugenzi Usimamizi Miliki wa NHC, Hamad Abadallah, alitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam jana ambao alisema ni utekelezaji wa mchakato wa kuboresha mazingira ya upangaji na upangishaji wa nyumba za shirika.
 
Sababu nyingine alisema inatokana na kuwapo watu, ambao hawakujitokeza kupewa upangaji wa moja kwa moja ili kuhalalisha ukaaji wao kwenye nyumba hizo tangu shirika liwatangazie suala hilo mwaka 2010.
 
Pia baada ya kuonekana kuna wapangaji, ambao hawakujitokeza kupata mikataba mipya yenye muda maalum baada ya shirika kufuta ile iliyokuwa haina kikomo kufuatia uhakiki wa wapangaji uliofanywa na shirika mwaka 2006 pamoja na kutoa mikataba ya aina hiyo.
 
 Alisema sababu nyingine inahusu wapangaji wengine waliopewa mikataba ya muda maalum kuisha muda wake na kuwa miezi waliyopewa inaanzia tangu kutolewa tarehe hiyo.
 
Alisema shirika limewaandikia barua za kuwakumbusha wapangaji hao kwenda ofisi za shirika kuchukua mikataba na kwamba, baadhi wamekwenda na wengine hawajafanya hivyo na kubaki bila mikataba.
 
Pia alisema mpangaji kutopewa mkataba ndani ya kipindi hicho itachukuliwa kuwa ni ukiukaji wa masharti ya upangaji.
CHANZO: NIPASHE

No comments: