TANZANIA imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na tatizo la rushwa ndani ya jeshi.
Taasisi ya Transparency International (TI), ambayo hutafiti masuala ya rushwa duniani imeitaja Tanzania kwamba jeshi lake lina rushwa kubwa na ndogondogo.Kwa mujibu wa gazeti dada la The Citizen la jana Jumapili, uongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) umekanusha vikali taarifa ya taasisi hiyo.
TI inadai katika taarifa yake kuwa sekta ya ulinzi ya Tanzania inakabiliwa na tatizo hilo na hiyo ni kutokana na mambo yake kuendeshwa kwa usiri mkubwa.“Hakuna kitu kibaya kama la rushwa kwenye jeshi, maana kuna fedha nyingi inatembea kutokana na ughali wa vifaa vya kijeshi. Bado Serikali nyingi zinafanya mambo haya kuwa siri na kutoa mwanya kwa rushwa kutembea.“Fedha inayotumika vibaya kwa masuala ya kijeshi, ingeweza kutumia vizuri zaidi katika masuala ya maendeleo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyoandikwa na Mark Pyman, ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha masuala ya Ulinzi cha Transperancy International.
Transparency International inaeleza kuwa fedha ya rushwa inayotembea kwenye sekta ya ulinzi inakadiriwa kufikia kiasi cha Dola 20 bilioni (Sh32 trilioni).
“Ripoti ya Transparency International itufungue macho Watanzania maana kwa kawaida huwa kila watu wakihoji mapato na matumizi ya jeshi tunaambiwa hatuwezi kujibiwa kwa madai ya woga wa kuhatarisha usalama wa taifa,” alikaririwa mbunge mmoja na gazeti la The Citizen.
Tanzania, hata hivyo, iko juu ya nchi nyingi za Afrika kwa tatizo la rushwa ingawa inatakiwa kurekebisha mianya mingi kwenye sekta hiyo.
“Tunaona Tanzania ina changamoto ya kuimarisha vyombo vya kutupa jicho kwenye jeshi. Mathalani, kuna Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Mambo ya Nje, lakini haina meno ya kuingia kwa undani masuala ya kijeshi,” iliongeza Transparency International.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, hata hivyo, alikaririwa na gazeti la The Citizen akidai kuwa taasisi yake imekuwa ikifanya kazi kitaalamu na kimaadili akitolea mfano jinsi wanavyoajiri wanajeshi kwa kufuata vigezo.
Transparency International inasema kuwa kuna Kitengo cha Utawala Bora cha Serikali ambacho hufanya ukaguzi kwenye jeshi ingawa halijatoa ripoti ya aina yoyote kuhusiana na ukaguzi wa bajeti ya jeshi. “Mfano kuna taarifa kuwa Kitengo cha Kilimo cha Jeshi la Kujenga Taifa (Suma-JKT) kuna kinajishughulisha na uchimbaji madini na biashara nyingine lakini kuna udhibiti mdogo,” iliongeza taarifa yao.
Julai mwaka jana, maofisa saba waandamizi wa Bodi ya Zabuni ya Suma-JKT walifunguliwa mashitaka ya matumizi mabaya ya ofisi na uhamishaji usio wa halali wa zaidi ya Sh 3.8 bilioni.
Waliotuhumiwa ni pamoja na Kanali Ayoub Mwakang’ata, Luteni Kanali Mkohi Kichogo, Luteni Kanali Paul Mayavi, Meja Peter Lushika, Sajini John Laizer, Meja Yohana Nyuchi na Luteni Kanali Felix Samillan wanaodaiwa kufanya makosa hayo mwaka 2009.
Tanzania imewekwa katika Kundi D kwenye orodha hiyo ya Transperancy International ya nchi zinazokabiliwa na kiwango cha juu cha rushwa na vigezo vinavyoangaliwa ni sekta za siasa, fedha, utumishi wa Kundi la D ni nchi ambazo zinakabiliwa na kiwango cha juu cha rushwa na katika orodha hiyo zimo pia nchi za Russia na China.
Hata hivyo, nchi zenye kiwango cha juu cha rushwa ziko katika Kundi F wakati zile zenye kiwango cha chini cha rushwa ziko Kundi A.
“Inasikitisha kuona kuwa Tanzania bado hakuna uwazi katika matumizi ya fedha za jeshi. Hata Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya nje haina meno,” alikaririwa Semkae Kilonzo wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Policy Forum.
Haya yanatokea wakati hivi karibuni Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje iligawanywa. Sasa kutakuwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama na nyingine itakuwa inashughulikia Mambo ya Nje.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment