ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 25, 2013

MAISHA NDIVYO YALIVYO:Mwanamke anamtesa mwanamke mwenzie ili aneemeke…ni kwanini?

NA FLORA WINGIA
Mpenzi msomaji, yapo matukio mengi ambayo yamedhihirisha kuwa wanawake wengi ni wakatili sana dhidi ya wanawake wenziwe. Hivi tatizo hapa ni kitu gani? Mimi nachokoza mada lakini msomaji wangu naomba uchangie maoni tuelimishane.

Naam. Kwanza nitoe mfano wa wanawake wanaochukua wasichana wa kike kutoka vijijini na kuwaleta mijini kwa ahadi za kuwapatia kazi au kuwasomesha lakini mabinti hawa wanaoishi kwenye madanguro na kusulubiwa kingono. Hii ni hatari sana.

Wanachukuliwa wakiwa watoto au wasichana wadogo, wengine hawajavunja hata ungo lakini wanajikuta wakiangukia mikononi mwa mijibaba iliyoshiba na kuharibu kabisa ndoto za maisha yao.

Mfano ni binti ambaye kisa chake kilichapishwa kwenye gazeti hili toleo la Jumamosi na Jumapili iliyopita, akitokea mkoa wa Manyara na kuletwa Dar na mama anayedai ni msamaria na kuahidi kumsomesha baada ya mama yake kufariki. Alimchukua kijijini akiwa na miaka 12 na akatoroka kwenye danguro alikokuwa anafungiwa na wasichana wengine akiwa na umri wa miaka 27.Kumbe kule kijijini mama huyo aliwakusanya na mabinti wengine kwa hadaa ya kuwasomesha kumbe akaishia kuwalundika kwenye danguro lake na kuwabadilishia wanaume huku ujira akiweka kibindoni. Huu ni ukatili ulioje?

Watoto hao walipochukuliwa kwao waliamini kuwa mama huyo atawasaidia kuinuka kimaisha lakini kumbe akawageuka na yeye kuneemeka kupitia biashara hiyo chafu. Hivi mama wa aina hii anajua Mungu Muumba yupo? Na je, anajua malipo ya Mungu ni hapa hapa duniani? Asubiri moto wake kwani vilio vya mabinti hao havitamweka mahali salama.

Naam. Msomaji wangu, hapa nataka kuonyesha jinsi baadhi ya kinamama walivyo wakatili dhidi ya watoto wa wanawake wenzao. Mabinti wanaojikuta katika mateso ya aina hii ni mama watarajiwa katika ukuaji wa familia zetu. Lakini wanaishia kuzimwa ndoto zao na watu wenye uchu usio kifani.

Hata wanaume hao wanaokwenda kuwasulubu mabinti waliofungiwa ndani ya madanguro hawako salama. Mkono wa Mungu ni mrefu utawafikia, na hakika wataadhibiwa sawasawa na matendo yao hayo maovu.

Matukio ya wanawake kutesa wanawake wenzao au mabinti za wanawake wenzao yako mengi. Matukio haya tunayashuhudia kila kukicha ndani ya jamii na familia zetu. Swali ni je, yanasababishwa na nini? Na nini kifanyike kuyatokomeza? Maswali haya na mengine ndiyo sote tunapaswa kuyatafutia majawabu ili matendo hayo ya aibu tuyatokomeze.

Hebu nijaribu kugusia mifano michache ya matukio au vitendo ambavyo naamini kabisa vinakiuka misingi ya binadamu na hivyo kutoa picha mbaya katika jamii na kulipotezea sifa taifa letu.

Ukiacha ile kasumba ya wanaume kutesa wake zao kwa kuwapiga au kuwanyanyasa na wakati mwingine kuwataliki kwa mikwara, lipo wimbi la wanawake huwatesa wanawake wenzao kwa kuwazushia mambo ya uongo yanayosababisha migogoro ya ndoa. Na hili limechangia ndoa nyingi kuvunjika au wanandoa kutengana.

Kinachotokea hapa ni kwamba wapo baadhi ya kinamama huamua kuvunja ndoa za wenzao kwa kuwajaza waume zao maneno pengine baada ya kujua siri za wake zao na matokeo yake huchekelea na kujiona washindi.

Wapo wanawake ambao wamethubutu hata kuwapora wenzao waume zao, tena moja kwa moja na kusababisha mateso kwa mama aliyeachwa pamoja na watoto. Huu ni ukatili usiovumilika.

Lakini katika matukio mengine, wanaume wanaojikuta kwenye mitego ya aina hii, wapo wanaojutia maamuzi hayo na wengine pengine kwa kuwachoka wake zao, hutupa jongoo na mti wake.

Wanawake wengine wabaya ni wale wanaochukua watoto wa kike toka kwa wazazi wao au ndugu zao toka vijijini kwa ahadi ya kuwaajiri kazi za majumbani au kwenda kuwasomesha mijini, lakini mabinti hao kuishia kufichwa kwenye madanguro kama nilivyodokeza hapo juu.

Wengine wanaishia kufanyishwa kazi za suluba kama vile kukamua ng’ombe maziwa, kulima bustani za mboga au hata zile kazi za kupika, kufua, kutunza watoto lakini kwa ujira mdogo na wengine hawapewi kabisa kwa maelezo kwamba watapewa baadaye ambayo haijulikani ni lini. Wakiuliza huambiwa wasubiri. Huu ni unyanyasaji usiokubalika.

Mpenzi msomaji, je, nawe walizungumziaje tatizo hili kama kichwa cha maneno katika makala haya kinavyouliza? Na je, linasababishwa na nini? Na nini kifanyike kulitokomeza?

Naamini unayo mengi ya kusema na hata ikiwezekana toa ushuhuda wa yeyote umjuaye anayenyanyasa mwanamke mwenzie bila kutaja majina ili mradi ni kisa cha ukweli. Karibu!

Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige) au barua pepe; flora.wingia@guardian.co.tz au fwingia@yahoo.com

No comments: