ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 17, 2013

Saba washikiliwa kwa vurugu za kidini Geita

Jeshi la Polisi mkoani Geita, linawashikilia watu saba akiwemo Mchungaji wa kanisa la TAG, Isaya Rutha (54), kwa madai ya kuhusika katika tukio la vurugu za kidini zilizosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila wa kanisa la PAGT, mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Leonard Paulo aliwataja watuhumiwa wengine waliohusika na mauaji hayo ni Khasim Abeid(44), Ramadhani Pastory (35) wakazi wa kijiji cha Busererere wilayani Chato.

Kamanda Paulo, alisema watatu kati yao akiwemo Mchungaji mmoja wamefikishwa mahakamaniJuzi na kusomewa mashtaka mawili likiwemo la kuua kwa kukusudia, ambapo walirejeshwa rumande hadi kesi hiyo itakaposikilizwa tena.

Aliongeza kuwa ili kuhakikisha tukio hilo linafanyiwa uchunguzi wa kina bila kuegemea upande wowowte, serikali kupitia Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka nchini (DPP), imemtuma mwanasheria wake ili kubaini chanzo cha vurugu hizo ndipo washtakiwa wachukiliwe sheria.

“Serikali kupitia DPP imemtuma mwanasheria ambaye atashirikiana na timu iliyoundwa ikiongozwa na Kamanda Hezron Kigondo kutoka Makao Makuu ya polisi kwa ajili ya kuchunguza mashtaka hayo mawili, moja likiwa linamkabili mchungaji Rutha kwa kuamasisha watu kuchinja nyama kinyume cha sheria ya chakula, dawa na mifugo ”,alisema Kamanda Paulo.
Aidha, alisema endapo kuna watu, au askari waliochangia vurugu hizo kwa uzembe wowote baada ya uchunguzi na kubainika sheria itafuata mkondo wake.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewasili mkoani humo kwa ziara ya siku mbili , kwa ajili ya kukutana na viongozi wa dini kwa lengo la kutoa rambirambi ya kifo cha Mchungaji Kachila.

Mbali na hilo, Pinda atazungumza pia na viongozi hao, juu ya sakata lililojitokeza hivi karibuni katika mkoa wa Geita na Mwanza juu ya uhalali wa uchinjaji nyama kisheria kati ya muumini wa kiislamu na mkristo.
CHANZO: NIPASHE 

No comments: