ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 7, 2013

Samatta aizamisha Cameroon

Kipa wa Cameroon, Effala Komguep, akipangua penalti ya Erasto Nyoni wa Taifa Stars wakati wa mechi yao ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa 
jijini Dar es Salaam jana.
Mbwana Samatta alifunga goli moja na Erasto Nyoni alikosa penalti wakati timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ilipoinyanyasa Cameroon kwa kuipa kipigo cha goli 1-0 katika mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Samatta anayechezea klabu ya TP Mazembe ya DRC, aliifungia Stars goli la ushindi katika dakika ya 89 akimalizia krosi safi ya kiungo wa Yanga, Frank Domayo na kuamsha shangwe kubwa kwenye uwanja uliopata mahudhurio makubwa ya mashabiki.


Stars, ambayo Desemba 22 mwaka jana iliwabwaga mabingwa wa Afrika, Zambia 'Chipolopolo' kwa goli 1-0 la Mrisho Ngassa kwenye uwanja huo, ingeweza kupata ushindi mnono zaidi kama Erasto Nyoni angefunga penalti yake ya dakika ya 28, ambayo hata hivyo ilipanguliwa na kipa wa Cameroon, Effala Komguep.

Refa Munyemana Hudu kutoka Rwanda aliamuru ipigwe penalti hiyo baada ya beki wa kati wa klabu ya Union Douala  ya Cameroon, Ngoula Patrick, kuunawa mpira wakati alipoanguka akijaribu kuzuia mpira uliopigwa na Mwinyi Kazimoto usimfikie mlengwa Mbwana Samatta.

Hadi mapumziko matokeo yalikuwa 0-0 na kila timu ikiwa imepata kona 3, huku kona za Tanzania zikijumuisha iliyotokana na mabeki wa Cameroon kuosha mpira wa penalti iliyookolewa na kipa Effala.

Kipindi cha pili, Stars ilianza kwa kuwashambulia mfululizo Wacameroon huku mabadiliko yaliyofanywa na kocha Kim Poulsen ya kumtoa kiungo wa Simba, Kazimoto, katika dakika ya 56 na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji wa TP Mazembe, Thomas Ulimwengu yaliwapa wenyeji nguvu mpya.

Ulimwengu alionekana kuwanyima usingizi mabeki wa Cameroon iliyowakosa nyota wake majeruhi Samuel Eto'o wa Anzhi Makhachkala ya Urusi na Alex Song wa Barcelona ya Hispania, kutokana uwezo wake wa kukaa na mpira.

Stars walicheza kwa kujituma na kutokata tamaa jambo lililozaa matunda kwa kupata goli la ushindi ikiwa imesalia dakika moja mechi kumalizika.

Kocha Kim aliwasifu wachezaji wake kwa kujituma na kwamba hakutaka kufanya mabadiliko mengi kwa kutaka kupima pumzi ya wachezaji wake.

Alisema mechi hiyo ni kipimo kizuri kwa Stars kwa sababu Cameroon ni timu kubwa barani Afrika.

Aliwasifu pia wadhamini Bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa kuipa timu mandalizi mazuri akisema yamechangia ushindi huo mwingine mkubwa dhidi ya taifa kubwa Afrika baada ya kuilaza Zambia iliyokuwa ikijiandaa kwenda kutetea taji lake la Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini.

Kocha wa Cameroon, Jean Paul Akono alikiri kuwa Tanzania ni timu nzuri na imeipa wakati mgumu timu yake ingawa hali ya hewa pia imechangia nyota wake kushindwa kucheza vizuri zaidi.

Vikosi vilikuwa; Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomarui Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Salum Abubakar 'Sure Boy', Mrisho Ngassa, Frank Domayo, Mbwana Samatta, Mwinyi Kazimoto/ Thomas Ulimwengu (dk. 56) na Amri Kiemba.

Cameroon: Effala Komguep, Bonnoit Assou-Ekotto, Aminou Bouba, Mgoula Patrick, Nyom Allan, Pierre Wome, Kingue Mpondo, Bedimo Henri/ Ashu Clovis (dk.73), Tchami Herve/ Elundu (dk.57), Olinga Fabrice/ Makoun Thierri (dk. 68) na Aboubakar Vincent/ Bakinde Gerrard (dk. 85).    

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: