Chuo hicho kimepanga kutumia Sh8 bilioni kama kianzio katika ujenzi wa hospitali hiyo ya kimataifa itakayosaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi.
Taasisi hiyo pia inajenga chuo cha kisasa cha afya kitakachosaidia kutoa ajira kwa wanafunzi watakaohitimu na kufanya vizuri katika masomo yao.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Baraza la STJUT, Joffer Maggira, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Maggira alisema hospitali hiyo ndiyo itakayokuwa mwarobaini wa wananchi wanaokwenda nje ya nchi kwa matibabau ya maradhi mbalimbali.
Alisema Watanzania wengi wakiwamo viongozi, wamekuwa wakikimbilia nje ya nchi hususan India, kupata matibabu na kwamba kukamilika kwa hospitali hiyo kutapunguza idadi yao na gharama wanazozitumia kwenda nje.
“Hospitali hii haitakuwa tofauti na Hospitali za Apollo za nchini India ambako wananchi wengi na viongozi wetu wamekuwa wakienda kutibiwa, nadhani safari hizi zitapungua na tutaanza huduma mwaka huu baada ya vifaa kuwasili na kufungwa,” alisema Maggira.
Alisema STJUT ina hospitali kama hizo katika nchi za Zambia, Ethiopia na Malawi na kwamba hospitali ya hapa nchini itakuwa ya rufaa.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, wagonjwa kutoka nje ya nchi wataletwa na kutibiwa katika hospitali hiyo.
Alisema kwa kuanzia, watakuwa na madaktari kutoka India na Italia wakisaidiwa na wafanya kazi wazalendo ambao watapatiwa ujuzi.
“Madaktari hawa ndiyo watakaoanza kutoa huduma za matibabu wakishirikiana na wazalendo. Huduma zitakuwa za gharama nafuu na kwa wale wasiojiweza watatibiwa bure,” alisema Maggira.
Kwa mujibu wa Maggira, ujenzi wa chuo na hospitali hiyo, unalenga katika kuisadia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, katika kutekeleza mpango wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Hiyo ni hatua nyingine muhimu baada ya Mei mwaka 2011, Serikali ya India kusaini makubaliano na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu ujenzi wa Tawi la Hospitali ya Apollo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya huduma za upasuaji wa moyo.
Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa India, Dk Manmohan Singh, walitiliana saini makubaliano hayo yatakayowezesha kujengwa kwa hospitali hiyo katika eneo la karibu na Mlimani City.
Ujenzi huyo utafadhiliwa na NSSF.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Hospitali za Aga Khan Tanzania, Dk Jaffer Dharsee alisema wakati akiwasilisha taarifa kuhusu ongezeko la magonjwa ya moyo nchini katika kongamano la wataalamu wa magonjwa hayo lililofanyika mwishoni mwa juma Jijini Dar es Salaam.
Dk Dharsee alisema huduma hizo zinatarajiwa kutolewa kwa gharama ya Dola 1,500 milioni sawa na Sh2.4 milioni badala ya Sh5.6 milioni zilizokuwa zinatumika kumpeleka mgonjwa India kufanyiwa upasuaji.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment