ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 11, 2013

TANZANIA YAZOA TUZO TATU ZA MAAJABU SABA YA AFRIKA.


Na Mahmoud Ahmad,Arusha 
TANZANIA imepata tuzo tatu za maajabu saba ya Afrika kupitia vivutio vyake bora vya utalii vya Mlima Kilimanjaro,Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Serengeti ambayo ndio iliongoza kwa kupata kura nyingi kuliko nchi nyingine yeyote.
Akitangaza matokeo hayo jana mjini hapa rais wa taasisi iliyoandaa tuzo hiyo Dk. Phillip Imler wa Marekani mbele ya waziri mkuu Mizengo Pinda alisema sababu iliyopelekea Tanzania kupata ushindi huo ni kutokana na kuwa na vivutio vya kipekee.
Akielezea hifadhi ya taifa ya Serengeti alisema kuwa ndio hifadhi ya kipekee iliyopata kura nyingi na kutokana na tabia za misafara ya wanyama wanaohama kwa msimu maarufu kama annul animal migration.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyekuwa mgeni rasmi katika ghafla hiyo, alisema kuwa nchi za Afrika zina vivutio vingi vya utalii na fursa kubwa ya kukuza pato kupitia utalii huo.
Alisema kutokana na sifa ambayo Tanzania imezipata kupitia vivutio vyake vitatu itaendelea kuvitunza kuhakikisha kuwa vinavutia zaidi watalii na kuongeza pato la taifa.
“Afrika ina vivutio vingi vyenye kuvutia hivyo kila nchi ni lazima ijivunie rasilimali hizo kwa kuvitunza na kuviendeleza,”alisema
“Kwa Tanzania ni bahati ya pekee kwa kuweza kupata tuzo tatu za maajabu saba ya Afrika ambazo ni za Mlima Kilimanjaro, Bonde la Ngorongoro pamoja na hifadhi ya Taifa ya Serengeti hivyo ni wajibu wa kuvitunza na kuviendeleza,”alisema Pinda.
Aliongezea kuwa iwapo watanzania wataendeleza tabia ya utunzaji wa vivutio vilivyopo nchini, nchi itaendelea kupata sifa duniani kote.

Naye Mkurugenzi wa Hifadhi za Taifa,(TANAPA),Dkt. Alan Kijazi alisema mlima Kilimanjaro ni mlima mrefu barani Afrika na hivyo una kila sababu ya kushinda na watanzania waendelee kuutunza.
Dkt Kijazi alisema kuwa hifadhi hiyo imeshinda kwa kuwa kuwa na wanyama wa kila aina kama Big Seven, Simba, tembo, Viboko, Nyati, Vifaru, Sokwe na Mamba.
Mbali na Tanzania Dk.Imler alivitaja vivutio vingine vilivyoshinda kuwa ni Red sea Reefs, Okavango Inland delta iliyopo nchini Botwasana, Sahara Desert na River Nile.

Aidha Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alisema ushindi huo ni historia kubwa duniani na kwamba ni jambo la watanzania wote kujivunia.

Pia aliwashukuru wananchi walioshiriki katika mchakato mzima wa kupiga kura na kuviwezesha kuingia katika ushindi kwa mara tatu.

No comments: