ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 13, 2013

Tuache kulea chokochoko za kidini


Juzi yalizuka mapigano makali kati ya Wakristo na Waislamu katika kijiji cha Buseresere, wilaya ya Chato, mkoani Geita, ambayo yalisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine sita kujeruhiwa vibaya huku mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi zikiharibiwa.
 
Habari za kipolisi zilithibitisha kuwa aliyeuawa ni Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God Tanzania, Mathayo Kachila, ambaye alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita, kutokana na kupata majeraha makubwa kichwani, usoni na shingoni na kupoteza damu nyingi. 
 
Habari ambazo zilichapishwa na vyombo vingi vya habari jana zilisema kuwa waumini waliohusika na vurugu hizo, wanatoka katika vijiji vya Katoro, wilaya Geita na Buseresere, wilaya ya Chato, ambazo zinapakana, chimbuko lake ni juu ya uhalali na haki ya kuchinja kitoweo! Iliekezwa kuwa mapigano hayo yalianza  saa 2:00 asubuhi baada ya waumini wa Kiislamu kuvamia bucha la kuuza nyama iliyopo katika kijiji cha Buseresere wakimtuhumu mmiliki wake kuuza nyama iliyochinjwa na Wakristo. Wengi wa waliovamia bucha hiyo wanadaiwa kufanya vitendo vya aibu na uvunjifu wa amani, walikuwa ni vijana.
 
Kwa kitambo sasa Geita kumekuwa na mvutano juu ya haki ya kuchinja kitoweo mabishano hayo yakielekezwa kwenye misingi za kiimani; hali hii ilimfanya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, kwenda kukutana na makundi yanayovutana na kufikia hitimisho kwamba wenye haki ya kuchinja ni Waislamu. Hata hivyo, baadhi ya Wakrsito walikataa kukubaliana na msimamo huo na kuahidi kwamba wataendelea kuchinja.
 
Ni katika misimamo hii inayosigana kiimani imesababisha sasa kifo, damu kumwagika na mali ya thamani kubwa kuharibiwa, lakini kubwa zaidi kutoweka kwa amani katika vijiji hivyo. Hali hii ni ya hatari siyo kwa waumini wanaovutana tu, bali ni hatari kwa utengamano na ustawi wa taifa hili.
 
Kwa kitambo sasa hapa nchini tumeshuhudia chokochoko za kidini, hizi zinafanywa na kuchochewa na watu ambao ama wananufaika kwa njia moja au nyingine na vurugu hizo au wanatumwa kufanya hivyo kwa faida wanazozijua wao. Mengi yametokea na yameandikwa na hadhari nyingi kutolewa juu ya mwelekeo wa taifa hili hasa suala la udini linapozidi kupaliliwa na kupigiwa chapua na baadhi ya watu kwa sababu wanazozijua wao.
 
Sote tu mashahidi hata inayoitwa mihadhara ya dini ya kutukana imani za watu wengine kwa kitambo sasa imefumbiwa mno macho na serikali ama kwa kuogopa lawama au kwa sababu ya uzembe tu wa wenye mamlaka kushindwa kuwajibika ipasavyo.
 
Matokeo ya hali hii ni hapa tulipofika sasa, kila kitu sasa kinatazamwa kwa macho na mwanga wa kidini, akipewa mtu cheo serikalini inaulizwa dini gani, wasipojua wanajaza wenyewe kwa kulitazama jina lake. Hali hii inadhaniwa kuwa ni nyepesi na itapita tu bila wenye mamlaka waliopewa na umma kuwajibika ipasavyo kuifanya Tanzania iendelee kuwa taifa lisilo na dini, serikali isiyo na dini na kwa maana hiyo iwe ni marufuku mtu yeyote kutumia kisingizio cha dini kuleta vurugu, uchochezi na usumbufu wowote kwa jamii.
 
Mapigano ya Geita yanatukumbusha yaliyotokea miaka ya mwanzoni mwa tisini wakati wa utawala wa awamu ya pili, watu  waliokuwa wamejihami kwa silaha za jadi walivamia bucha za kuuza nyama ya nguruwe jijini Dar es Salaam eneo la Ubungo na kuvunjavunja kila kilichokuwako.
 
Rais Ali Hassan Mwinyi alisimama kidete wakati huo kwanza kwa kukemea na kulaani vitendo hivyo, lakini pia aliagiza wote walioshiriki tukio lile washughulikiwe kwa mujibu wa sheria za nchi, na alisema wazi kuwa kila mtu ana rukhsa ya kula atakacho, hayupo yeyote wa kumzuia mwingine kula atakacho. Na kweli umma uliona dola ikitenda kazi na hali ile haikupata kurudia nchini.
 
Kwa bahati mbaya suala la haki ya kuchinja limechukuliwa mno kisiasa, hakuna kiongozi anayesimama hadharani na kusema kuwa kila mtu ana haki ya kufanya afanyalo alimradi havunji sheria za nchi. Dini siyo kitu cha shuruti, ni hiari, ni utashi wa kila mmoja anavyoona, haifai na wala haipendezi serikali kuweka mikono yake kwenye mambo ya dini, haitaweza na hakika haitafanikiwa.
 
Ni lazima waliokabidhiwa madaraka ya dola wajiulize kama kwa miaka yote hii kabla ya uhuru na baada ya uhuru watu wamekuwa wanakula kitoweo kutoka mabucha nchini, siku za hivi karibuni nini kimetokea maswali juu ya uhalali wa kuchinja yanaibuka? Nini hasa kimetokea?
 
Wakati tukilaani vurugu zozote zinazobebeshwa sura ya ugomvi wa imani, na kwa kweli tukiiomba serikali kuacha masihara na suala hili kwa sababu kwingine duniani tumeona jinsi dini zimekuwa vyanzo vya mauaji na umwagaji mkubwa wa damu, tungependa kuona misingi ya katiba ya nchi hii ikiheshimiwa kwamba taifa hili halina dini na serikali iliyopo haina dini, kwa maana hiyo kila raia ana haki na hiari ya kuwa na imani atakayo bila kushurutishwa au kuingiliwa na yeyote alimradi mwenendo wa imani yake hauvunji sheria za nchi.
 
Tukatae chokochoko za dini kwa sababu inavyoelekea kuna watu wamejipanga kuitumbukiza nchi hii katika machafuko ya dini. Tunaomba kauli na msimamo thabiti kama ule wa Rais Mwinyi miaka ya tisini juu ya chokochoko za Geita.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: