Mpenzi msomaji wangu, katika ulimwengu wa mapenzi kuna mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza na kuwafanya baadhi ya watu kuishia kusema kuwa ni bora waishi peke yao kuliko kuwa na wapenzi.
Wanaosema hivyo ni wale ambao wametendwa kwa kiwango kikubwa. Wapo ambao wametokea kuwapenda sana wapenzi wao lakini kinyume chake ikawa ni kulizwa kila siku huku usaliti ukiwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Kimsingi hakuna kitu kinachouma kama kusalitiwa, tena kusalitiwa na mtu ambaye moyo wako umempa nafasi kubwa sana. Zaidi ya yote inaumiza sana unapompenda mtu lakini yeye akawa hakupendi, matokeo yake yakawa ni mpenzi kukutesa. Kwa hayo kweli unaweza kufikia wakati ukasema ni bora kumuacha na kuishi peke yako.
Cha kujiuliza ni kwamba, ni kweli unaweza kuishi peke yako bila kuwa na mpenzi? Ni wangapi ambao waliwahi kusema hivyo lakini leo hii wako kwenye uhusiano na watu wengine? Ni wengi tu na imetokea hivyo kwa kuwa, mapenzi ni sehemu muhimu sana katika maisha ya binadamu.
Hata kama una uwezo mkubwa kiasi gani lakini huwezi kusema umetosheka bila kuwa na mpenzi na ndiyo maana wapo ambao wana kila kitu lakini mapenzi yakiwakorofisha kidogo tu wanakonda na kutoona umuhimu wa kuendelea kuishi.
Ndiyo maana tunaambiwa kwamba, tunapokwazwa na wale tuliotokea kuwapenda sana tusione kuwa ni mwisho wa sisi kupenda. Tuone ni hatua ya kuelekea kuwapata wale wenye mapenzi ya kweli na sisi.
Nimeshawahi kusema huko nyuma kwamba, wale ambao leo unawaona wako kwenye uhusiano bora wenye furaha wengi waliwahi kutendwa sana, nikasema katika safari ya kumpata mtu mwenye mapenzi ya kweli ni lazima uwe tayari kuumizwa kwanza, huo ndiyo ukweli wenyewe.
Utakuwa ni mtu wa ajabu kama utakata tamaa ya kuwa na mpenzi baada ya kuumizwa na mtu wa kwanza. Hivi unajuaje kama baada ya huyo utampata yule uliyepangiwa na Mungu?
Tusiwe watu wa kukata tamaa mapema na kufikia hatua ya kusema hauko tayari kupenda. Kama hauko tayari kupenda basi utakuwa hutaki kuendelea kuishi na kama ni hivyo ni bora uondoke tu duniani.
Najua wakati mwingine tunatamka maneno hayo kwa hasira hasa tunapofikiria jinsi tulivyopoteza muda wetu kwa watu tuliotokea kuwapenda sana lakini maumivu hayo yasitupeleke kule ambako tunaweza kuyaharibu maisha yetu kwa kupoteza furaha.
Wapo ambao eti mpaka leo wanajifanya ni wagumu. Hawataki kuwa na wapenzi kwa sababu waliwahi kutendwa. Sikatai, hayo ni maamuzi ya mtu lakini watu hao ukijaribu kuwafuatilia utabaini wanakosa furaha iliyokamilika. Wanajikaza wakidhani wanaziridhisha nafsi zao lakini kiukweli wanaathirika sana.
Naomba nisema tu kwamba, unaposema hutaki tena kuwa na mpenzi unajiweka kwenye mazingira mazuri ya kuathirika kisaikolojia. Mpenzi ni muhimu sana kwenye maisha yako lakini uvumilivu pia unatakiwa kuchukua nafasi yake.
Mpende akupendaye na asiyekupenda achana naye ili kumpa nafasi yule ambaye Mungu amepanga kuwa wako. Unapofanyiwa yale ambayo hukutarajia kufanyiwa na ‘mtu’ wako, kama yanavumilika, vumilia lakini kama unaona yanaukwaza moyo wako, muweke pembeni kisha kuwa na subira kwani naamini Mungu hawezi kukutupa.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment