ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 7, 2013

Utalii waingiza Sh10.8 trilioni

JUMLA ya Dola za Marekani 6.3 bilioni sawa na Sh10.8 trilioni,zilipatikana katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2011,kupitia njia ya utalii kwa kupokea watalii 3,854,467, Bunge lililezwa jana.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,Adam Malima ambaye alikuwa akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utali, Hamisi Kagasheki.
Malima alikiri kuwa ni kweli Tanzania ina vivutio vingi na ambavyo ni maarufu ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),licha ya kuwa havijatangazwa kikamilifu.
Alisema kwa sasa wastani wa watalii wanaoingia Tanzania ni kati ya 770,894 ambao huingia kwa ajili ya kufanya shughuli za utalii katika maeneo ya uwindaji, utalii wa picha pamoja na kuangalia ndege.
Katika swali la msingi,Kombo Khamisi Kombo (CUF) alitaka kujua Tanzania inaingiza mapato kiasi gani ikilinganishwa na vivutio vilivyoko nchini kuliko nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mbunge huyo alitaka kujua pia wastani wa watalii wanaoingia nchini kwa kila mwaka na kuhoji kwa nini serikali inaendelea kulifumbia macho na kuwaachia wananchi wa Kenya kuendelea kuutangaza Mlima Kilimanjaro kuwa wanaotaka kuuona lazima wapitie kwao.
Naibu Waziri alisema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2011 Tanzania iliingiza Dola za Marekani 1,353.29 milioni kutokana na watalii 867,994 waliotembelea nchini.
“Aidha mapato yatokanayo na utalii kwa nchi ya Kenya katika kipindi hicho cha 2011 yalikuwa ni Dola za Marekani 1.10 bilioni kutokana na idadi ya watalii 1,265,136 waliotembelea nchi hiyo,” alisema waziri.
Hata hivyo, waziri alitetea kuwa Kenya bado inaonekana kuwa juu katika suala zima la kutangaza utalii na kwamba walianza siku nyingi, lakini akasema si tatizo kwa kutangaza kuwa wageni lazima wapitie Kenya ili wauone Mlima Kilimanjaro kwani dunia nzima inajua kuwa mlima huu uko Tanzania. 


No comments: