KUNA utata kuhusu tuhuma za meneja wa moja ya hoteli za kitalii zilizo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kukutwa na ngozi ya chui nyumbani, akiwa hatua za mwisho kuisafirisha nje ya nchi bila vibali kutokana na kauli zinazokinzana kati ya jeshi la polisi na kampuni inayomiliki hoteli hiyo kuhusu tukio hilo.
Wakati kampuni ya Elewana Africa (T) Ltd inayomiliki hoteli hiyo ikidai uchunguzi wa polisi umegundua kuwa Ryan McFarlane ambaye ni raia wa Afrika Kusini hana hatia kutokana na kupandikiziwa ngozi hiyo na mmoja wa wafanyakazi, polisi mkoani Arusha wanasema uchunguzi bado unaendelea.
Lakini uchunguzi wa gazeti hili umegundua kuwa tayari mfanyakazi mmoja wa hoteli hiyo anayeitwa Emmanuel Adam, aliyekuwa msimamizi msaidizi wa huduma vyumbani, amefukuzwa kazi kuanzia Januari 24, mwaka huu kwa tuhuma za kumpandikizia meneja ngozi ya chui kwa nia ya kumtia hatiani.
Katika kile kinachodaiwa ni juhudi za kuvuruga ushahidi, mkuu wa kitengo cha ulinzi katika hoteli ya Tarangire Treetop, Kibori Sindalo na meneja wa usafi hotelini hapo wamehamishiwa hoteli ya Serengeti Pioneer.
Desemba 21, mwaka jana, Saa 11:00 jioni, kikosi kazi cha askari kutoka jeshi la polisi, Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa), kilimtia mbaroni meneja huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa anajihusisha na biashara ya nyara za serikali kinyume cha sheria.
Pamoja na kudai kuwa uchunguzi wa polisi haukumkuta na hatia, Uongozi wa Kampuni ya Elewana Afrika (T) Ltd inayomiliki hoteli ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Tarangire, umeamua kumhamisha kutoka Treetop kwenda hoteli yao nyingine ya Serengeti Pioneer kwa wadhifa huo huo wa meneja.
Mkurugenzi wa Biashara, Habari na Mawasiliano wa Elewana Africa (T) Ltd, Jason Barry, amethibitisha kuwa McFarlane ambaye ni mmoja wa mameneja wakuu waandamizi wa kampuni hiyo, amehamishiwa hoteli yao iliyoko hifadhi ya Serengeti.
“Baada ya polisi kujiridhisha kuwa McFarlane hana kesi ya kujibu kuhusu tuhuma hizo, sasa anaweza kurejea kwenye kazi na majukumu yake ya kawaida ndani ya kampuni na hivi sasa yuko Serengeti kwenye moja ya hoteli zetu,” alisema Barry.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo alikataa kuzungumzia taarifa za baadhi ya wafanyakazi kufukuzwa kazi au kuhamishwa kutoka hoteli ya Tarangire, akidai kampuni hiyo haina utaratibu wa kuzungumzia watu binafsi.
Uongozi wa Elewana Afrika (T), Limited ni kampuni tanzu ya Sopa Lodge inayomiliki hoteli kadhaa katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Serengeti na Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro. Sopa pia wanamiliki hoteli katika hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya.
Wakati Elewana Afrika (T) Ltd ikidai polisi imemsafisha mfanyakazi wake dhidi ya tuhuma za kukutwa na ngozi ya chui, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas, amekanusha taarifa hizo akisema uchunguzi bado unaendelea.
“Nakuhakikishia kwamba vita dhidi ya uwindaji haramu na biashara ya dawa za kulevya tuliyoianzisha haitamsalimisha yeyote anayejihusisha na biashara hizo. Tutafanya hivyo bila kujali cheo, fedha, rangi wala utaifa wa mtu. Nitakupa taarifa baada ya muda mfupi,” alisema Kamanda Sabas.
Hatua ya kufukuzwa Adam zimegubikwa na utata baada ya mfanyakazi mwenzake, Leyan Leyaseki anayefanya usafi nyumbani kwa meneja aliyedaiwa kusema alimshuhudia (Adam) akiweka ngozi ya chui kwa meneja kukanusha maneno hayo na kufikia uamuzi wa kuacha kazi kupinga mwenzake kufukuzwa kwa tuhuma za wongo.
“Kama kweli mimi ndiye niliyemwona Ema (Emanuel Adam) akiweka ngozi kwa meneja, kwanini sikuitwa kuyathibitisha mbele ya kikao. Hayo maneno ni ya uongo yaliyotungwa kumlinda Mzungu (McFarlane), dhidi ya tuhuma zake na kwa sababu sipendi maneno yao ya Kiswahili, nimeamua kuacha kazi,” alisema Leyaseki
Kikao kilichosikiliza tuhuma dhidi ya Adam na kufikia uamuzi wa kumfukuza kazi kilifanyika Januari 24, mwaka huu. Wajumbe wake wametajwa kuwa ni Kanali Elisamia Nnko, Elisaria Makivao ambaye ni Meneja Uajiri wa Sopa na Elewana Afrika (T), Limited na viongozi wa Chama Cha Wafanyakazi (Chodawu), tawi la Tarangire Treetop Lodge.
Mwananchi

No comments:
Post a Comment