Monday, February 4, 2013

Wachungaji 14 watimuliwa Moravian


KANISA la Moravian Jimbo la Kusini, limetangaza kuwafukuza kazi wachungaji wake 14 na makatibu wanne wa idara mbalimbali kwa kosa la kuchochea vurugu ndani ya kanisa hilo.
Uamuzi huo ulifikiwa jana na Halmashauri Kuu ya Jimbo la Misheni Mashariki na Zanzibar baada ya wachungaji hao kujitangazia halmashauri yao mpya, wakijitenga na uongozi ndani ya kanisa.
Pamoja na kuwaondoa wachungaji hao, uongozi huo wa jimbo, umefanya mabadiliko ya uongozi katika Wilaya ya Morogoro na kuwateua wachungaji wengine kadhaa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na wachungaji waliofukuzwa.
Uamuzi huo umekuja wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Jimbo la Mashariki na Pwani ya Kanisa la Moravian Tanzania, Clement Fumbo na wenzake saba wakiwa wamefungua kesi namba 222 Mahakama Kuu ya Tanzania, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Moravian Jimbo la Rungwe kupinga kuvuliwa madaraka na kusimamishwa kazi.
Katika kesi hiyo iliyopangwa kuendelea kusikilizwa Februari 6, mwaka huu mbele ya Jaji Augustini Mwarija, Fumbo na wenzake saba wanapinga kuondolewa madarakani na kusimamishwa kazi na wanaiomba mahakama iamuru walipwe Sh500 milioni kama fidia na gharama ya kesi.
Kadhalika uamuzi wa kufukuzwa kwa wachungaji hao umefanywa wakati Mchungaji Fumbo akidai kwamba yeye bado ni mwenyekiti halali na kutangaza halmashauri yake mpya, jambo ambalo uongozi wa Kanisa la Moravian unasema ni kinyume cha katiba wa kanisa hilo.
Akitoa taarifa ya hatua hiyo mbele ya waumini wa kanisa hilo lililoko Ushirika wa Mabibo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Jimbo la Misheni Mashariki na Zanzibar, Adolf Mwakanyamale, aliwataja wachungaji waliofukuzwa kuwa ni pamoja na mwenyekiti wa Wilaya ya Kaskazini, Alinanuswe Mwakilema.
Wengine na nyadhifa zao kwenye mabano ni Noel Mwakalinga,(Mjumbe wa Halmshauri Kuu), Fanny Ndemange (Katibu wa Idara ya Kina Mama), Angelina Mwamakula (Mchungaji Msaidizi Ushirika wa Kimara) na Mariamu Kasendeka wa Ushirika wa Pugu Kajiungeni.
Wachungaji wengine na sharika zao kwenye mabano ni Tumaini Mwakijale (Tanita) Mosted Kibona (Kitunda), Eliza Kipesile (Kawe), Lugano Anganisye (Mwenge), Baraka Mwakijale (Mlandizi), Azaria Lwaga (Segerea) na Fredy Mwakyusa wa Usharika wa Kiwalani.
Katibu huyo aliwataja wakuu wa idara wanne waliofukuzwa kuwa ni Mchungaji Anyasime Kasebele (Uwakili), Emmanuel Mwaijande (Kwaya), Hezron Mwangaja (Uinjilisti) na Silas Mwakibinga (Miradi na Maendeleo).
“Tumeamua kuwaita pia wachungaji wetu wastaafu, lengo likiwa ni kuziba mapengo yote yaliyotokana na ndugu zetu ambao wameamua kuasi na kujitangazia kanisa lao,” alisema Mchungaji Mwakanyamale.
Wanaoziba nafasi
Katibu Mkuu huyo wa Jimbo la Misheni Mashariki na Zanzibar, aliwataja wachungaji walioteuliwa kuziba nafasi zilizoachwa wazi kuwa ni Aswile Mwamkumbi ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Morogoro kuchukua nafasi ya Samuel Mwaiseje aliyehamishiwa Wilaya ya Kaskazini.
Wengine ni Aran Kajuni na Ester Kapalala ambao wameteuliwa kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu na Makatibu wa Idara; Eliud Nsamuli (Uwakili), Joachim Mwaseba (Uinjilisti), Profesa Meline Mbonile (Miradi na Maendeleo) na Balwege Minga ( Kwaya).
Wachungaji walioteuliwa kwenda sharikani ni Elly Ambukege (Segerea) Jubeck Mapasa (Tabata), Deborah Mwasumbi (Mwenge), Tulibumi Mwaiseje (Kawe), Abel Mapasa (Kimara), Joachim Mwaseba (Magomeni), Bupe Iloge (Kiwalani) Rukhia Mwankenja (Kitunda) na Erica Ludela (Pugu Kajiungeni).
Alisisitiza kuwa vituo vingine vya Golani, Mbezi mwisho, Makhabe na Kigogo vitasimamiwa na wenyeviti wa wilaya hadi hapo vitakapopatiwa watumishi.
Kauli ya Mwenyekiti
Mwenyekiti wa Jimbo la Kusini ambalo ni jimbo mama la eneo hili la Misheni, Mchungaji Clement Mwaitebele alitoa wito kwa kanisa kuendelea kushikamana katika kipindi hiki na kuongeza kuwa wachungaji waliofutwa hawatatambuliwa na Kanisa la Moravian kwa ujumla wake.
“Kitendo walichokifanya wenzetu ni uasi mkubwa sana, tumewaita kwa upole ili tusemezane nao hawajataka kuja, huu ni uamuzi wa kikatiba, kama kweli wameitwa na Mungu wao watarejea, nasi tutawasikiliza na tutakuwa tayari kujirudi,” alisema Mwaitebele.
Kesi mahakamani
Ijumaa iliyopita, Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, Dar es Salaam ilitupilia mbali ombi la Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini, kutaka kufunguliwa makufuli yaliyofungwa katika Kanisa la Ushirika wa Tabata, ili waweze kumsimika mchungaji mpya, Lawi Mwankuga.
Makufuli hayo ni yale yanayodaiwa kufungwa na Wachungaji Gervas Mwakafwila, Silas Mwakibinga, Tukuswiga Mwakabur, Atuganile Mbombo, Isakwisa Ernest na Sekela Mukisele ikiwa ni hatua ya kuzuia bodi hiyo kumsimika mchungaji mpya.
Bodi hiyo kupitia wakili wake, Henry Chaula wa Kampuni ya Uwakili ya C&M 2013 ilitaka kesi hiyo namba 12 ya 2013 isikilizwe chini ya hati ya dharura, lakini Jaji Mathew Mwaimu alikataa ombi la kutaka kufunguliwa kwa makufuli hayo.
Jaji huyo aliruhusu shughuli za kawaida za kanisani hapo kuendelea na kusisitiza kwamba kilichozuiwa ni usimikaji wa mchungaji ili kuondoa uvunjifu wa amani.
Mwananchi

No comments: