ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 28, 2013

Wanafunzi 972 watoroka masomo

WANAFUNZI 972 wa Shule ya Msingi Nyamajashi katika Kata ya Lamadi, wilayani Busega, wamekatisha masomo na kujiingiza katika shughuli mbalimbali zikiwamo za uhudumu wa baa na uuzaji wa karanga.
Wanafunzi wengine wa kike,  wameozwa.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Mary Wambura, amemweleza mkuu wa wilaya hiyo, Paul Mzindakaya kuwa kwa sasa shule imebakiwa na wanafunzi 162 tu.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, wanafunzi ni wa madarasa ya kwanza, nne na saba.
Mkuu wa wilaya alikuwa amefanya ziara ya kushitukiza jana  katika shule hiyo.
Mwalimu  Wambura alisema pamoja na tatizo hilo la utoro,  shule  pia inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa.
Alisema tatizo hilo limechangiwa na hatua ya wataalamu kuvunja vyumba vinne vilivyokuwa vimejengwa chini ya viwango na kwamba hatua hiyo imesababisha shule kubakiwa na vyumba viwili vinavyotumiwa na wanafunzi waliobaki kwa utaratibu wa zamanu.
Alitaja matatizo mengine kuwa ni upungufu wa walimu, madawati, vitabu na  nyumba za walimu.
Hata hivyo Wambaru aliishukuru halmashauri ya wilaya hiyo kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa ili kuwawezesha watoto  kusoma kwa unafuu.
Kwa upande wake,  mkuu wa wilaya alielezea kusikishwa kwake kuhusu matatizo yanayoikabili shule na kuitaka halmashauri ya wilaya,kuipa upendeleo wa pekee katika mipango yake ya kuboresha mazingira ya kutolea elimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Naomi Nko, alisema hatua zitachukuliwa ili kuboresha mazingira ya kusoma katika shule hiyo.
Mwananchi


No comments: