ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 15, 2013

Wananchi wateketeza nyumba kwa imani za kishirikina


FAMILIA nne katika Kijiji cha Ihahi, Wilaya ya Mbarali hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuteketezwa kwa moto na wananchi wenye hasira baada ya kuwatuhumu kufanya mauaji ya kishirikina.

Tukio la kuteketezwa kwa nyumba hizo lilitokea jana saa 9:00 mchana na kusababisha mali zote zilizokuwa ndani ya nyumba hizo, ikiwamo mifugo kuteketea kwa moto.

Watu waliochomewa nyumba zao walitambulika kwa majina ya Mohamed Mangea (48) ambapo pamoja na mkewe, Pili Hamisi wanahisiwa na ushirikina huo, Ramadhani Mhongole na wengine waliotambuliwa kwa jina moja moja la Mzee Mwampishi na Sekilulumo.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili wamedai kuwa wamefikia hatua ya kuteketeza makazi ya watu hao baada ya Serikali ya wilaya hiyo kupuuza madai yao dhidi ya watu hao walipotoa taarifa za mauaji.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ramadhan Hassan alisema tuhuma za kuwapo kwa mauaji ya kishirikina yaliyofanywa na watu waliochomewa nyumba zao yamekuwapo kwa muda mrefu sasa, lakini Serikali ngazi ya wilaya haikuzifanyia kazi ipasavyo. Alisema taarifa za awali zilipofika Serikali, mapema mwezi uliopita, Serikali ilimtuma afisa wa upelelezi kutoka kituo cha Polisi Chimala kwa ajili yan kushughulikia suala hilo.

Alisema mpelelezi huyo aliendesha kura za siri kwa ajili ya kuwabaini watu wanaojihusisha na ushirikina kijijini hapo,ambapo wananchi walipiga kura bila matatizo.

Alisema matokeo ya kura hiyo yalionyesha watuhumiwa waliochomewa nyumba kuwa ndio vinara wa ushirikina na Polisi iliwakamata na kuwapeleka kituoni.

Alisema hata hivyo watuhumiwa hao walirejea uraiani baada ya muda mfupi,hali iliyosababisha wananchi waliokuwa na hofu ya maisha yao, kupandwa na ghadhabu na kuamua kuteketeza nyumba zao kama njia ya kuwaondoa katika kijiji chao.

Kwa upande wake,Ramle Ibrahim ambaye ni mtoto wa mmoja wa waathirika wa tukio la kuchomewa nyumba alisema kabla ya kuchoma nyumba ya wazazi wake, kundi la vijana walikwenda nyumbani kwao wakiwa wamebeba mapanga na kuanza kuwapiga wazazi wake na kuwataka waondoke kijijini hapo na wakati wa tukio hilo wazazi wake pamoja na wenzake walilazimika kukimbilia kituo cha polisi kwa ajili ya kunusuru maisha yao.

Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili jana jioni, Polisi walikwenda kijijini hapo na kukamata watu wawili, tukio ambalo lilisababisha wananchi kuandamana kwenda kituo cha Polisi cha Chimala ili kushinikiza wenzao kuachiwa huru. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Diwani Athuman alipoulizwa kuhusiana na tukio hili alidai kuwa yupo Dodoma kwa shughuli za kikazi na kumtaka mwandishi wa habari hii kuwasiliana na Kaimu
wake Barakael Msaki.
Mwananchi


No comments: