ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 20, 2013

Watu 54 kizimbani kwa masuala ya Sheikh Ponda

WATU 54, wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, waliokamatwa kwa tuhuma za kufanya maandamano haramu, jana walifikishwa kortini.
Washtakiwa hao walikamatwa Ijumaa iliyopita wakidaiwa kufanya maandamano haramu kwa lengo la kwenda kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kumshinikiza kumpa dhamana Sheikh Ponda na mwenzake Sheikh Mukadamu Swalehe.
Walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, juzi na kusomewa mashtaka manne yakiwamo ya kufanya maandamano yaliyozuiliwa na polisi.
Wakili wa Serikali, Zuberi Mkakati alidai kuwa upelelezi umekamilika. Jana washtakiwa hao walisomewa maelezo ya awali (PH) na kisha kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, ikaanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Akiwasomea mashtaka yao, Wakili wa Serikali Peter Njike akisaidiana na mawakili wengine wa Serikali, Bernard Kongola, Joseph Maugo na Nassoro Katuga, alidai kuwa washtakiwa hao walikamatwa wakifanya maandamano haramu Februari 15, 2013.
Wakili Njike alidai kuwa awali polisi walitoa zuio la maandamano hayo, lakini washtakiwa hao walikaidi na kwamba hata siku ya tukio polisi waliwaamuru kutawanyika katika mikusanyiko waliyokuwa wakiifanya, lakini walikaidi, ndipo wakakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Mshtakiwa wa kwanza Salum Makame, alikiri kukutwa na kisu na kipaza sauti lakini akakana kuwa hakuwa mfuasi wa Ponda. Wengine pia wakikana kuwa wafuasi wa Ponda wala kufanya maandamano hayo.
Kutokana na washtakiwa hao kukana, upande wa mashtaka ulianza kutoa ushahidi ukianzia na Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam (ZPC), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Ahmed Msangi.
Katika ushahidi wake, ACP Msangi alidai kuwa akiwa Kaimu wa Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Februari 11, 2012 alipokea barua ya taarifa ya kuwepo kwa maandamano hayo kutoka kwa Shura ya Maimamu Tanzania na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu.
Alidai kuwa barua hiyo iliyosainiwa na Amiri wa Shura ya Maimamu, Temeke, Sheikh Juma Idd, ilieleza kuwa watafanya maandamano Februari 15,2013, baada ya swala ya Ijumaa kutokea misikiti yote Dar na kwamba wanaomba ulinzi.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo itakapoendelea tena leo.
Mwananchi


No comments: