ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 13, 2013

Waziri afanya ziara ya ghafla, ajionea mengi machafu

Dk. Terezya Huvisa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa, amekifunga kiwanda cha CI Group kilichopo Chan’gombe, jijini Dar es Salaam baada ya kukukuta kikifaya kazi katika mazingira hatarishi yakiwamo vyoo vichafu na wafanyakazi wake kufanya kazi bila ya kuwa na vifaa maalum.

Kadhalika, Dk. Huvisa amezitaka baadhi ya hoteli kuwasilisha vyeti vya mazingira kabla hajachukua uamuzi wa kuzifungia kufanya biashara.

Alitangaza uamuzi huo jana alipofanya ziara ya ghafla akiwa na maofisa wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ya kuvitembelea baadhi ya viwanda na hoteli kuangalia uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na shughuli zinazofanywa katika maeneo hayo.
Dk. Huvisa alikumbana na vizingiti baada ya uongozi wa CI group kufunga lango la kuingilia sehemu za kiwanda hicho zilizoathirika kwa uchafu huku viongozi wanaohusika wakitimua mbio na kumuacha peke yake.

Kiwanda hicho kilichofungiwa kinahusika na uchapishaji wa vipeperushi, kuandaa mabango pamoja na kutengeneza maandishi ya tisheti pamoja na kofia.

Maeneo yaliyotembelewa na Dk. Huvisa ni kiwanda cha Bia cha Serengeti (SBL), Hoteli za Coco Beach, Golden Tulip na Sea Cliff.

Katika hoteli ya Sea Cliff, Dk. Huvisa aliagiza kubomoa bomba linalotiririsha maji machafu ili kuona kama mfumo wake unaelekea baharini ama kabla ya kuchukua uamuzi wa kuifungia ama kuiacha.

Mwishoni mwa mwaka jana, Dk. Huvisa alifunga hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano ya Double Tree by Hilton na Girrafe Ocean View, iliyopo Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam kwa kosa la kuvunja sheria za masharti ya utunzaji wa mazingira.

Alisema hatua hiyo ni mkakati endelevu wa mwaka 2013 wa kukagua hoteli zote na viwanda vilivyopo ufukweni mwa bahari zinazokiuka sheria za uendeshaji.

No comments: