Waziri wa Madini na Nishati, Profesa Sospeter Muhongo
Na Freddy Macha
Waziri wa Nishati na Umeme, Profesa Sospeter Muhongo amewasili Uingereza leo jumapili tarehe 24.2.13 kwa ziara ya siku nne.
Waziri alipokewa na Balozi wetu mheshimiwa Peter Kallaghe na anatazamiwa kukutana na viongozi mbalimbali wa serikali ya Uingereza na wataalamu wanaohusiana na shughuli za madini, maendeleo ya kimataifa.
Miongoni mwa maofisa anaotazamiwa kukutana nao kesho Jumatatu ni pamoja na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Kiafrika, Jumuiya ya Madola na nchi za Kigeni, Bwana Mark Simmonds; Naibu Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa Uingereza, Bi Lynne Featherstone na Mbunge wa Stratford chama cha Conservative, Jeremy Leffroy ambaye pia ni mwenyekiti wa kundi la Wabunge wa Uingereza wanaoshughulikia Tanzania (APPG).
Jumanne saa kumi na moja jioni Waziri ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa amepanga kuongea na Watanzania wanaoishi Uingereza ukumbi wa Ubalozi wetu London. Ukumbi uko 3 Stratford Place, London W1C 1AS. Stratford Place iliyojishika na barabara kuu ya Bond- ni sekunde chache tu mbele ya kituo cha magari moshi na mabasi cha Bond Street.
Waziri ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa anaongozana na Dk Athanas Macheyeki wa Ukaguzi wa Madini Tanzania, Seleman Hatibu Chombo wa idara ya Nishati katika Wizara ya Madini na Nishati na Bwana Sosthenes Masau Bigambo Massola, katibu wake muhtasi.
Waziri Muhongo ni msomi aliyebobea ndani ya masuala ya kisayansi na taaluma ya mawe na madini. Mbali na kuwa profesa na mhariri wa jarida la “Journal of African Journal Sciences” ni vile vile mwanachama wa jumuiya mbalimbali za madini na sayansi za kimataifa. Jumuiya hizo ni “Geological Society of London,” “Geological Society of America,” “Chinese Academy of Geological Sciences” na “Tanzania Academy of Sciences.”
Kiongozi huyu ni Makamu Rais wa Tume ya Tume ya Ramani ya Madini duniani iliyoundwa 1881 Ufaransa. Lengo la tume hii ni kuendeleza masuala ya mazingira, madini na hali ya hewa ya ulimwengu na Rais wake ni Philippe Rossi.
Mshindi wa tuzo kadhaa za kielimu na kisayansi, Profesa Muhongo alizaliwa Musoma mwaka 1954 akamaliza masomo yake vyuo vya Dar es Salaam na Ujerumani. Mwaka juzi alizawadiwa “Ordre des Palmes Academiques” ya serikali ya Ufaransa – inayotolewa kwa wataalamu waliochangia masuala ya kielimu na kitamaduni toka lipoanzishwa na Mfalme maarufu Napoelon karne ya 19.
Mwaka 2007 kiongozi huyu alipewa tuzo la heshima (“Honours Award”) na Jumuiya ya Madini ya Afrika Kusini na 2004 akatunukiwa tuzo la “Robert Shackleton” la Jumuiya ya Madini Afrika. Robert Shackleton aliyefariki 2001 ni Mwingereza aliyeendeleza uchimbaji madini Afrika Mashariki.
Nchini Tanzania Waziri Muhongo amepata zawadi ya Makamu wa chuo kikuu (1977), zawadi ya Gondwana (1979) na tuzo la kitaifa la utafiti wa kisayansi na teknolojia (NARST) linalotolewa na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania(2006).
No comments:
Post a Comment