![]() |
| Mwandishi wa habari, Erick Kabendera. |
-NDUGU WAOMBA ULINZI!
Stori: Mwandishi Wetu
HUWEZI kuamini lakini ukweli ni kwamba Erick Kabendera ambaye ni mwandishi wa habari wa hapa nchini ana wasiwasi na maisha yake baada ya kwenda kutoa ushahidi uliomwangamiza mfanyabiashara maarufu Reginald Mengi ambaye sasa anatakiwa kumlipa Sarah Hermitage, raia wa Uingereza aliyekuwa amemshitaki mahakamani.
Sarah alimshitaki Mengi akidai kukashifiwa na magazeti yake na katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama Kuu ya London, Uingereza, jaji alimhukumu kumlipa mama huyo paundi za Uingereza milioni 1.2 (ambazo ni sawa na Shilingi Bilioni 2.9 za Kitanzania) baada ya hapo vituko vya kuisumbua familia ya Kabendera mkoani Kagera vikaanza.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chama cha Waandishi wa Habari za Uchunguzi kiitwacho Forum for African Investigative Reporters (FAIR), familia ya Kabendera, imekuwa ikisumbuliwa na maofisa wa uhamiaji ambao wamekuwa wakiwakamata wazazi wake ili ionekane kuwa mzee Mengi ndiye anayefadhili unyanyasaji huo.
“Kuna watu ambao ni maadui wa mzee Mengi wanafadhili unyanyasaji wa familia ya Kabendera ili ionekane Mengi ndiye mhusika kwa lengo la kumharibia jina, tunaomba polisi waweke ulinzi kwa familia hii maana wanaweza hata kuua ili kumtia katika matatizo mzee wa watu wakati hahusiki,” alisema mwanafamilia mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini.
Licha ya familia hiyo kusumbuliwa na maofisa wa uhamiaji mara kwa mara, FAIR kinasema majambazi walivamia nyumba ya familia hiyo wiki sita zilizopita na kuharibu mali na nyaraka kadhaa. Wameomba Kabendera alindwe.
Habari zaidi zinasema tayari Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi ameiagiza idara ya uhamiaji mkoani Kagera kutoisumbua familia ya Kabendera.
Wakati hayo yakitokea, Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (Committee to Protect Journalists -CPJ) katika taarifa yake ya mwaka 2012 imesema Tanzania inaingia katika kundi la hatari ( a danger zone) kwa wana habari.
Hali hiyo imekuja baada ya uchunguzi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), kuchunguza mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi aliyeuawa Septemba mwaka jana na polisi kushindwa kuwahoji polisi sita kutokana na vyeo vyao.
GPL

No comments:
Post a Comment