ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 5, 2013

Uchaguzi Kenya: Uhuru Kenyatta aongoza,watu 22 wauawa

Kura zikihesabiwa kwenye kituo kilichopo Viwanja vya Kibera Social, jijini Nairobi baada ya wananchi wa Kenya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo jana. Picha na AFP  
Matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu nchini Kenya yanaonyesha kuwa Uhuru Kenyatta, mtoto wa Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta anaongoza, huku akifuatiwa kwa karibu na aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Raila Odinga.
Kama alivyo Uhuru, Raila pia ni mtoto wa mmoja wa waasisi wa taifa la Kenya, ambaye alikuwa Makamu wa Mzee Kenyatta, Jaramong Oginga Odinga.
Hadi majira haya ya  saa 6.45 usiku wa kuamkia leo,  Uhuru ambaye ni mgombea wa TNA alikuwa amepata kura 744,648 sawa na asilimia 56.1 wakati Raila ambaye ni mgombea wa ODM alikuwa akifuatia kwa kupata kura 527, 780 sawa na asilimia 39.7.
Matokeo hayo ni kutoka katika vituo zaidi ya 5000 kati ya 31,000 na yalikuwa yakionyeshwa moja kwa moja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kadri yalivyokuwa yanaingia.
Hata hivyo Mwenyekiti wa IEBC, Isaack Hassan akizungumza na vyombo vya habari jana usiku alisema matokeo hayo ni ya awali na kwamba matokeo kamili yangetangazwa na tume yake baada ya kukusanya taarifa kutoka vituo vyote vya kupigia kura.
Wagombea wengine walikuwa wameachwa mbali. Hao ni Musalia Mudavadi, Peter Kenneth, James Kiyiapi, Martha Karua, Mohamed Dida na  Paul Muite.
Waliokufa wafikia 22
Wapema watu 22 wakiwamo askari polisi tisa waliripotiwa kuuwawa  baada ya kuvamiwa na kikundi cha watu zaidi ya 200 huko Mombasa na Kilifi saa chache kabla ya Wakenya kuanza kupiga kura jana.
Saa chache kabla ya uchaguzi huo, askari polisi tisa waliuawa katika mashambulizi yaliyotokea kwenye miji ya Mombasa, Kilifi na Kwale na kuacha wavamizi wapatao 10 na raia wa kawaida watatu pia wakifariki.
Baada ya vifo hivyo, serikali ilipeleka vikosi vya askari kutoka Mariakani Barracks kwenda kutuliza ghasia hizo wakati kundi lingine la askari lilitoka Nyali Barracks kwa ajili ya kuweka doria katika miji ya Mombasa na North Coast.
Taarifa zilizopatikana baadaye jana zilisema kuwa kwenye mji wa Mombasa askari polisi wanne waliuawa na watu zaidi ya 100 waliovamia kituo cha kura cha Miritini.
Polisi pia ilithibitisha kuuawa kwa watu saba katika mapigano hayo huku na wengine kadhaa kutiwa nguvuni.
Wavamizi wengine waliuawa katika miji ya Kisauni na Kilifi huku polisi wanne wakiuawa Chumani na mmoja huko Chonyi huku watu watatu wakiuawa kwa kupigwa risasi.
Wakati huo huo, mwanamke mmoja wa miaka 72 alianguka na kufariki akiwa kwenye foleni ya kupiga kura katika kituo cha Kaunti ya Murang’a.
Marehemu aliyefahamuika kwa jina la Wanjiku Maina alianguka saa tatu asubuhi katika kituo hicho kilichopo Shule ya Msingi Kaganda katika jimbo la Kiharu na alifariki wakati akikimbizwa Hospitali ya  Muriranjas.
Mkuu wa Polisi Kenya, David Kimaiyo alisema Kikundi cha Mombasa Republican Council (MRC), ndicho kinachohusika na shambulio hilo na wafuasi wake wawili wametiwa mbaroni.
“Askari wameelekezwa kutumia silaha kadiri wanavyotakiwa na sheria, ili kuhakikisha hakuna mauaji mengine ya polisi na raia yanatokea,” alisema Kimaiyo.
Wajitokeza kwa wingi
Wananchi walijitokeza kwa wingi katika maeneo mbalimbali jana kupiga kura.
Wakati vituo vilikuwa vinafunguliwa saa 12 asubuhi, watu walianza kufurika vituoni saa 8.00 na saa 9.00 usiku ili kuwahi nafasi na ilipofika muda uliopangwa, misururu ilikuwa mirefu kupindukia.
Katika vituo, ambavyo Mwananchi ilitembelea, pamoja na wingi wa watu, bado wapigakura walikuwa na matumaini ya kuchagua viongozi wao.
Hata hivyo, kulikuwa na matukio kadhaa ya kukatisha tamaa, ikiwamo kukwama kwa mashine za digitali za kutambua alama za vidole za waliojiandikisha (biometric machines).
Baadhi ya mashine, ziliathiriwa na hitilafu wakati nyingine zikikosa umeme katika vituo vingi vya maeneo mbalimbali ya Kenya, hivyo makarani kulazimika kutumia daftari la wapigakura.
Mwenyekiti wa IEBC, Hassan alikiri kuwapo kwa hali hiyo na kusema ingetafutiwa ufumbuzi na kuahidi kuwa muda ambao ungepotea ungefidiwa baadaye jioni.
Katika hatua nyingine; watu wawili akiwamo mwanamke mwenye umri wa miaka 72, walianguka na kufariki dunia wakati wakisubiri kupiga kura.
Mwanamke huyo alipoteza maisha saa 5.08 asubuhi  katika Kituo cha Kihalu kwenye Shule ya Msingi Kaganda, Kaunti ya Muranga. Mpigakura mwingine alianguka saa nne asubuhi katika Kituo cha St Mathew, eneo la Hardy, Nairobi. Alifariki akiwa hospitalini.
 
Kura Arusha, Dar
Mamia ya wananchi wa Kenya wanaoishi Tanzania walipiga kura katika majiji ya Dar es Salaam na Arusha.
Wakenya hao walipata fursa kwa mujibu wa Katiba Mpya ya nchi hiyo iliyoanza kufanya kazi mwaka 2010.
Ofisa wa IEBC, David Maina ambaye alikuwa anasimamia upigaji huo Arusha, alisema kwamba hadi kufikia saa tisa alasiri jana watu 145 kati ya 200 waliojiandikisha, walipiga kura.
MWANANCHI


No comments: