ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 28, 2013

ASASI YA VIJANA WA UMOJA WA MATAIFA TANZANIA KUKUSANYA MAONI YA MIKAKATI BAADA YA 2015


Mwenyekiti wa YUNA Asasi ya vijana ya Umoja wa Mataifa Lwidiko Edward akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo leo wakati alipozungumzia mpango wa Asasi hiyo kukusanya maoni ya mikakati baada ya mwaka 2015. kulia ni Mwenyekiti wa Baraza kivuli la umoja wa Mataifa TIMUN -2013 Catherine Fidelis.

Kama tunavyofahamu, tunaelekea mwishoni mwa Malengo ya Maendeleo ya Kimilenia, Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa Tanzania imeanza harakati za majadiliano ya mikakati baada ya 2015 kati ya vijana kwenye zaidi ya mikoa sita nchini Tanzania. Mwaka huu, mkutano wa Baraza Kuu Kivuli La Kimataifa la Umoja wa Mataifa litafanyika Dodoma katika ukumbi wa bunge wa Pius Msekwa kuanzia tarehe 2 hadi 6 Aprili 2013 ikiwa na mada isemayo, “Malengo ya Maendeleo ya Kimilenia, kutazama mikakati ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi baada ya 2015”. Mkutano huu utashirikisha vijana 160 waliochaguliwa kutoka Tanzania bara na visiwani pamoja na vijana kutoka nchi mbalimbali duniani. Lengo letu kuu ni kuhakikisha kwamba sauti ya vijana inahusishwa katika ajenda za mashauriano ya Malengo ya Maendeleo ya Kimilenia na kuandaa ripoti ambayo itajumuishwa katika taarifa ya taifa itakayopelekwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Mkutano huu wa kimataifa utakuwa majadiliano ya mwisho ya vijana kabla ya kutayarisha taarifa ya mwisho.

Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa Tanzania inayofuraha kuwajulisha kwamba, mwaka huu Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa Baraza Kuu Kivuli La Kimataifa la Umoja wa Mataifa. Kwa miaka kumi na tano, Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa imekuwa ikiandaa mkutano wa Baraza Kuu Kivuli la Umoja wa Mataifa, ambapo washiriki hupata fursa ya kufanya kazi kama wanadiplomasia na hushiriki katika vipindi sawa na vile vya mashirika ya kiserikali. Washiriki hufanya utafiti kuhusu nchi fulani, hupata majukumu kama yale ya wanadiplomasia, hufanya utafiti wa masuala ya kimataifa, hujadili, huelimishana, hushauriana na hatimaye kupendekeza masuluhisho ya matatizo mbalimbali ya dunia.

Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa Tanzania inapenda kutumia fursa hii kukaribisha Watanzania wote kuungana mkono na vijana wa Tanzania watakavyokuwa wanatoa michango na mitazamo yao mikubwa na ya kimataifa katika suala la ajenda ya malengo ya maendeleo ya kimilenia baada ya 2015. Asasi ya Vijana wa Umoja wa Mataifa Tanzania pia inachukua nafasi hii kuwaomba mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali kuwa kipaombele katika kuwasaidia vijana wanaposhiriki katika nafasi hii ya pekee inayokusudia kuwaleta vijana wa Tanzania karibu na Umoja wa Mataifa pamoja na dunia kwa ujumla.

No comments: