Watatu wauawa, wengine 17 wajeruhiwa vibaya
JK atoa maagizo wahusika wote wawajibishwe
Watu wanne akiwemo mkandarasi na viongozi watatu wa Manispaa ya Ilala ya jijini Dar es Salaam wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano, kufuatia kuporomoka kwa Jengo la ghorofa 16 na kuua watu watatu , wengine 17 kujeruhiwa.
Mkandarasi huyo wa jengo hilo alijisalimisha kwa polisi akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Wanaoshikiliwa katika tukio hilo ni viongozi wa Manispaa ya Ilala ambao ni Mhandisi Mkuu, Ogare Salu, Mhandisi wa majengo Godluck Mbaga na Mkurugenzi Mkuu wa ukaguzi wa majengo, Wilbrodi Muliyabuso .
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, ameagiza kusimamishwa kwa ujenzi wa jengo la ghorofa 16 lililopo karibu na jengo lililoporomoka baada ya kubainika kuwa mjenzi ndiye mhandisi aliyehusika kujenga ghorofa lililoporomoka.
Mmiliki wa ghorofa hilo anadaiwa kuwa ni mfanyabishara maarufu jijini Dar es Salaam, Ali Raza.
Tukio la kuporomoka kwa jengo hilo lilitokea majira ya saa 2:30 asubuhi katika makutano ya barabara ya Morogoro na Indira Gandhi karibu na msikiti wa Shia na kusababishia magari zaidi ya manne ambayo yalikuwa yameegeshwa katika eneo hilo kuharibika.
Maelfu ya watu walifurika kushuhudia tukio hilo hali iliyosababisha Jeshi la Polisi kufunga baadhi ya barabara ili kuwazuia watu wasisogee karibu na eneo la tukio ili kurahisisha zoezi la uokoaji watu waliofukiwa na kifusi.
Kazi ya uokoaji ilifanywa na wananchi kwa kushirikiana na Kikosi cha uokoaji, mgambo, JKT, kikosi cha uokoaji, polisi pamoja na jeshi la wananchi (JWTZ).
Mbwa na farasi wa polisi waliletwa katika tukio hilo kwa ajili ya kuwatanya wananchi ambao walikuwa wamefurika katika eneo hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Sadick alisema kuwa ameamua kusimamisha ujenzi katika jengo hilo lingine kwa kuwa amepata taarifa kuwa mmiliki wa jengo hilo pamoja na mhandisi ndio aliyehusika kujenga ghorofa ambalo limeanguka.
Alisema ujenzi huo utasimama mpaka hapo jengo hilo litakapokaguliwa kwa kina na wahandisi wa bodi wathibitisha na kama ujenzi huo ulikuwa hafifu hatua za kinidhamu kuchukuliwa.
Sadick aliwataka wananchi walio jirani na jengo hilo wahame kwa muda kwa taadhari mpaka hapo litakapokaguliwa ubora wake.
Hata hivyo, Sadick alisema uokoaji ulikuwa mgumu kutokana na jana kuwa siku ya sikukuu hali iliyosababisha mitambo pamoja na vifaa vingine kutopatikana kwa urahisi.
Alisema hadi ilipofika mchana shughuli za uokoaji ziliendelea vizuri kutokana na baadhi ya watu kujitolea kupeleka mitambo ya uokoaji katika zoezi hilo.
Sadick alisema baadhi ya watu ambao wameokolewa wamepelekwa katika Hospoitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu.
Alisema kati ya waliookolewa, wawili walikuwa katika hali mbaya na kupumua kwa msaada wa oxygen.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova, alisema kuwa wanashikiliwa viongozi watatu kwa ajili ya mahojiano.
Alisema Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), lilitoa vyombo vya uokoaji kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wadau wengine.
Mkuu wa Oparesheni kutoka JWTZ, Stanslaus Mishako, alisema vijana 200 kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walipelekwa eneo la tukio kushirikiana na wananchi katika zoezi la uokoaji.
Hata hivyo, hadi mchana wananchi walilazimika kutumia ndoo kuchota kifusi kwa kuhofia vijiko hivyo kusababisha maafa zaidi kwa watu waliokuwa wamefunikwa na kifusi hicho.
Kwa upande wa Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Kheri Kessy, alisema wanatoa pole kwa wafiwa pamoja na majeruhi waliopo hospitalini.
Alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza mwaka 2007 na mmiliki aliomba kibali cha ujenzi katika manispaa hiyo ambapo alitakiwa kujenga jengo la ghorofa 10 tu.
Alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya kuzidishwa kwa idadi ya ghorofa hizo, alisema haelewi kama zilzikuwa zimezidi na kwamba kabla ya kuongeza ghorofa, mmiliki alitakiwa kuomba kibali kabla ya kuongeza na kufanyiwa ukaguzi kama ubora wa nondo pamoja na vifaa vingine vimekidhi kiwango.
Naye Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia alisema bado kuna tatizo la vifaa vya uokoaji na kwamba bajeti ijayo inatakiwa itengwe fedha kwa ajili ya kitengo hicho kukabiliana na majanga ya aina hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema kuwa ameshangazwa na serikali kukataa kutoa kibali kwa ndugu waliokwama chini ya jengo hilo ambao wameita vikosi vya uokoaji vya kulipia kutoka nchini Israel kwa gharama zao wenyewe.
Alisema ndugu hao walikuwa wakifuatilia kibali ili kikosi hicho kije kwa kuwa kilikuwa kipo tayari na matokeo yake serikali imekata kutoa kibali.
Naye Aliabbas Karim ambaye ni miongoni mwa watoto ambao walikuwa wanacheza mpira katika eneo hilo anasema baada ya kusikia mshutuko walifanikiwa kukimbia na kueleza kuwa aliwaacha wenzake wanne ambao mpaka sasa hawajapatikana.
Aliwataja kwa majina kuwa ni Salman Damji, Suhail Karim, Zahid Mohamed na Yusup Khaki.
Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walilalamikia kuwa mkandarasi huyo kajenga jengo hilo kwa kiwango cha chini kwani kilichokuwa kikionekana ni mabaki ya vumbi la mchanga ikionyesha dhahiri kuchakachuliwa kwa saruji hali iliyosababisha jengo hilo kuporomoka.
Aidha nondo ziliotumika katika ujenzi huo haziendani na jengo hilo na kuilaumu manispaa hiyo kutolikagua jengo hilo wakati wana wataalamu.
JK ATAMBELEA ATOA MAAGIZO
Kufuatia tukio hilo Rais Jakaya Kikwete alitembelea jengo hilo na kusikitishwa na kuhuzunishwa na maafa yaliyotokea.
Rais Kikwete amewapa pole wafiwa na majeruhi na wanaoendelea kupatiwa matibabu baada ya kubanwa katika kifusi, wakiwamo watoto wadogo ambao walikuwa wanacheza chini ya jengo hilo wakati lilipoporomoka jana asubuhi huku likiendelea kujengwa.
Hata hivyo, amewapongeza na kuwashukuru wananchi wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika zoezi la uokoaji pamoja na vyombo na taasisi za umma na serikali zinazoshiriki katika zoezi na kazi hiyo ya uokoaji.
Aliwataka kuendelea na jitihada hizo ili kama kuna watu ambao bado wamebanwa kwenye kifusi waweze kuokolewa ili wapatiwe matibabu, na kama watakuwa wamepoteza maisha miili yao ipatikane na iweze kupewa mazishi ya heshima yanayostahili mwanadamu.
Rais Kikwete alitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadik pamoja na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova, kuhakikisha kuwa mjenzi wa jengo hilo , Mhandisi Mshauri aliyekuwa anasimamia ujenzi wa jengo hilo, Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam ambaye alitoa kibali cha ujenzi na ndiye Mkaguzi wa ujenzi pamoja na mwenye Jengo, wanapatikana haraka na kuwajibishwa ipasavyo.
Amezitaka taasisi za kitaaluma zinazohusina na shughuli za ujenzi – Wachoraji Majengo, Wakadiriaji Majengo, Wajenzi, Wakandarasi na Wahandisi nazo zichunguze tukio hilo kwa haraka na kwa karibu, ili zibaini yapi yalikuwa ni matatizo na zichukue hatua kwa mujibu madaraka na mamlaka ya taasisi hizo kwa sababu zinayo madaraka na mamlaka hayo.
Alisema kuwa wakati umefika kwa taasisi hizo sasa kujihusisha kwa karibu zaidi na matatizo yanayojitokeza katika shughuli za ujenzi kwa sababu kila yanapoporoka majengo inakuwa heshima mbaya kwa taasisi hizo.
Hivyo ni muhimu kwa taasisi hizo kufanya uchunguzi wa kubaini nini chanzo cha kila tukio kuanzia na lile la leo – kama ilikuwa ni udhaifu katika uchoraji, kama ilikuwa ni udhaifu katika ukandarasi, kama ilikuwa udhaifu na Ushauri ili hatua stahiki zichukuliwe.
NHC YATOA TAARIFA
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na huduma kwa Jamii cha Shirika la Nyumba (NHC), ilisema kuwa shirika hilo na M/s Ladha Construction iliingia kwenye mradi wa ubia Februari 4, 2008 ambapo Shirika hilo litakuwa na hisa asilimia 25 na mbia ana asilimia 75 mara baada ya mradi kukamilika.
Kwa mujibu wa sera ya ubia iliyoanza kutumika mwaka 1993 na kuhuishwa mwaka 1995 na 2005, NHC lilikuwa likitoa ardhi ambayo ilikuwa ikihesabika kama asilimia 25 ya mtaji wake kwenye jengo husika na mbia alikuwa akipata asilimia 75.
Kwa mujibu wa mkataba huo mbia mwendelezaji M/s Ladha Contruction Limited kama walivyo wabia wengine, anapaswa kabla ya kuanza ujenzi kupata vibali kutoka kwenye mamlaka husika na kuwa na wataalam wa ujenzi na washauri waliokubalika na kuthibitishwa na mamlaka husika. Aidha, mbia huyu akishapata wataalam hao ndiye anayehusika kuingia nao mikataba ya kazi ya kujenga na kusimamia ubora wa jengo husika kwa mujibu wa sheria.
Katika mradi huo mbia mwendelezaji aliajiri wataalamu wote waliosajiliwa na Mamlaka husika ambazo ni CRB, ERB, AQRB na Mansipaa husika na mamlaka nyinginezo.
“Kwa kuwa ujenzi ulikuwa bado haujakamilika, Shirika lilikuwa bado halijapata asilimia 25 ya umiliki wake.
Pia tunapenda kuufahamisha Umma kuwa, Shirika la Nyumba la Taifa, lilisimamisha utoaji wa miradi mipya ya ubia mwaka 2010 ili kuweza kutathimini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa miradi ya ubia na hivyo kuwezesha kutengeneza sera mpya. Kama sehemu ya zoezi hilo, shirika pia lilifuta jumla ya mikataba 64 ambayo ilikuwa imesainiwa lakini haijaanza ujenzi.” Ilisema taarifa hiyo.
Katika sera mpya ambayo utekelezaji wake utaanza hivi karibuni Shirika litahusika moja kwa moja katika kuteuwa mjenzi mtaalam (contractor), msimamizi mtaalam wa mradi husika (consultant) na kusimamia kikamilifu shughuli zote za ujenzi.
“Tunapenda kuufahamisha umma kuwa taarifa zaidi zitatolewa baada ya vyombo husika kuwasiliana na mjenzi wa mradi huu au moja kwa moja kutoka M/s Ladha Construction Limited ambaye ndiye mbia mwendelezaji aliyekuwa anasimamia ujenzi huu.”
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment