ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 7, 2013

KAULI YA POLISI NA WAZIRI NCHIMBI KUHUSU HUYU MHARIRI ALIETOBOLEWA JICHO NA WASIOJULIKANA

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini na Mhariri Mtendaji wa New Habari Corporation Absalom Kibanda usiku wa kuamkia march 6 2013 ameshambuliwa na watu wasiojulikana na kuumizwa vibaya na baadhi ya viungo vyake kunyofolewa.

Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Theophil Makunga amesema tukio lilitokea saa sita usiku wakati kibanda alipokua akiingia nyumbani kwake akitokea kazini, alipiga honi geitini ili afunguliwe na mlinzi ndipo lilipotokea kundi hilo na kuvunja vioo vya gari na kuanza kumshambulia.

Baada ya mlinzi kupiga kelele kuomba msaada ndipo kundi hilo lilipokimbia huku tayari likiwa limemng’oa jino Kibanda pamoja na kumtoboa jicho la kushoto ambapo kwa sasa inasubiriwa ripoti ya Madaktari wa Taasisi ya mifupa (Moi) ambako amelazwa.
Picha imetoka mtandao wa Mabadiliko.

Afisa Mtendaji wa New Habari Hussein Bashe amesema baada ya kukamilika kwa mpango wa kufatilia hati ya kusafiria ya Kibanda ambayo Serikali iliizuia kama dhamana ya kesi inayomkabili, wanatarajia kumpeleka Afrika Kusini kwenye hospitali ya Mil Park.

Kamanda Suleiman Kova wa Kanda maalum ya Dar es salaam amesema Polisi imeteua maafisa wanne wenye uzoefu wa ishu za upelelezi ambao watashirikiana na maafisa kutoka makao makuu ya jeshi hilo kufanya uchunguzi.

Pamoja na hayo, Waziri wa mambo ya ndani Dr. Emmanuel Nchimbi nae amezungumzia hili tukio kwa kusema Serikali inalaani vikali hilo tukio na itatumia nguvu zake zote kuwasaka waliohusika.

1 comment:

Anonymous said...

Tanzania,Tanzania...nakupenda kwa moyo woteeee...nchi yangu Tanzania jina lako ni tamu sana.....naimba si kwa furaha bali kwa huzuni...Tz yetu imeharibika kabisa sio ile ya zamani...mambo kama haya yanasikitisha sana....tukizamia mtoni msitulaumu kabisaaaaa......
Bi mkora....Pole sana Kibanda...