ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 27, 2013

Kibadeni atoa angalizo, asema ni mapema sana kushangilia

Pamoja na ushindi mnono wa Tanzania wa mabao 3-1 dhidi ya Morocco Jumapili, Taifa Stars bado ina kibarua kigumu cha kusaka kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Kwa ushindi huo, Stars sasa imefikisha pointi sita na hivyo kuendelea kushika nafasi ya pili katika Kundi C ikiwa nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba ambayo iliifunga Gambia mabao 3-0 Jumamosi.
Kwa mujibu wa kanuni za Fifa, Afrika itawakilishwa na mataifa matano kwenye fainali za Kombe la Dunia 2014, ambapo washindi kumi wa kwanza katika kila kundi watacheza mechi mbili za mtoano ili kupata timu tano za mwisho.
Ili kupata nafasi ya kwanza, Stars inahitaji kushinda mechi yake ya marudiano ugenini dhidi ya Morocco Juni 8, kabla ya kurejea Dar es Salaam kuikabili Ivory Coast hapo Juni 15 (mechi itakayotoa hatima ya Tanzania) na kumalizia kampeni yake huko Gambia mwezi Oktoba.
Kutokana na ratiba hiyo ngumu, wadau wa soka nchini wameitaka Serikali pamoja Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukaa pamoja na kuandaa mikakati itakayoisaidia timu hiyo kufanya vizuri katika mechi zake zilizobaki.
Akizungumza na gazeti hili jana kocha wa Kagera Sugar, Abdallah Kibaden alisema kutokana na hali hiyo, Serikali na TFF kwa kushirikiana na wadhamini wakuu wa timu hiyo wakae chini kwa pamoja na kuandaa mikakati kwa ajili ya mechi zilizobaki.
“Bado tunakabiliwa na kazi kubwa mbele yetu, tushangilie ushindi huu, lakini tukumbuke kazi iliyopo mbele yetu ni ngumu, Serikali, TFF pamoja na wadhamini wakuu wa Stars wanatakiwa kutopoteza muda, wakae pamoja na kupanga mikakati ya kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi hizo zilizobaki,” alisema Kibaden.
Wakati huohuo, Serikali imetangaza rasmi kuwa ipo tayari kugharimia mkataba mpya wa kocha wa timu ya Taifa Stars, Kim Poulsen.
Hatua hiyo imeondoa giza totoro lililotanda kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lililokuwa likisita kutangaza hatima ya kocha Kim ambaye mkataba wake unamalizika Mei 15 mwaka huu.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Amos Makalla alisema jana kuwa walikuwa kimya muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali na moja kubwa ni uhusiano uliolega kati ya Serikali na TFF.
Makalla alisema kuwa baada ya tofauti zilizokuwapo kati ya TFF na Serikali kumalizika wanaitaka TFF kuandaa mkataba mpya wa kocha huyo ili uwe tayari kwa ajili ya kusainiwa.
Alisema kuwa hivi sasa wameridhika na maendeleo ya timu ya Taifa hasa katika michuano ya kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia la 2014 nchini Brazil.
Makalla alisema kuwa Taifa Stars imejengeka na kuwa moja ya timu ngumu barani Afrika kutokana na matokeo mazuri katika mechi za kimataifa za kirafiki na hata zile za mashindano.
Mwananchi

No comments: