ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 27, 2013

Mahakama yatupa maombi kesi ya uchaguzi Kenya

Nairobi. Mahakama ya Juu (Supreme Court) nchini Kenya jana ilitupilia mbali viapo viwili katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta wa Muungano wa Jubilee.
Maombi yaliyotupwa ni lile la muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali lililoitaka mahakama iamuru tume ya uchaguzi kufikisha mahakamani hapo nyaraka zote zilizotumika wakati wa uchaguzi huo.
Kadhalika mahakama hiyo ilitupilia mbali hati ya kiapo yenye kurasa 839 kilichowasilishwa na upande wa Muungano wa Cord ambacho kilidai kwamba kura katika majimbo 120 zilikuwa haziwiani na idadi ya wapigakura, hivyo kuitaka mahakama hiyo iitishe uchunguzi wa kina kwa daftari hilo pamoja na kura zilizopigwa.
Katika kiapo cha Cord, Jaji Phillip Tunoi alisema kwa mujibu wa sheria hati za kiapo si haki ya mlalamikaji au mlalamikiwa hivyo kabla wa kuwakilishwa walalamikaji walipaswa kupata ruhusa ya mahakama, jambo ambalo halikufuatwa.
Kwa upande wake Jaji Mohammed Warsame aliyesoma uamuzi dhidi ya kiapo cha mashirika yasiyokuwa ya kiserikali alitupilia mbali maombi yao kwa maelezo kwamba yalifikishwa mahakamani nje ya muda uliowekwa kisheria.
Katika ombi lao muungano huo wa Africog ulidai kuwa kufeli kwa mfumo wa kielectronikiwa kuhesabu kura ulikuwa umepangwa kwa madhumuni ya kuiba kura. Hivyo tume hiyo iamuriwe kuleta mahakamani hapo nyaraka zote ili zifanyiwe uchunguzi wa kitaalamu.
Mwananchi

No comments: