Haruna Chanongo (kulia) wa simba akishangilia goli lake alilofunga dhidi ya Coastal Union ya Tanga, pamoja na wachezaji wenzake Abdallah Seseme (katikati) na Rashid Ismail wakati wa mechi yao ya Ligi kuu ya Tanzania Bara
Simba iliyojaza wachezaji wa kikosi B ilizinduka kutoka katika mwenendo wake wa matokeo mabovu wakati ilipoibwaga Coastal Union ya Tanga mabao 2-1 katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Nahodha Juma Kaseja, Juma Nyosso, Komalbil Keita, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi 'Boban' na Felix Sunzu walikuwa miongoni mwa nyota wa kikosi cha kwanza cha Simba walioachwa nje katika siku ambayo taarifa zilishazagaa mitaani kuwa majina ya wakali kadhaa yalikabidhiwa na uongozi kwa kocha Patrick Liewig wakidaiwa kuwa wanaihujumu timu.
Nahodha Juma Kaseja, Juma Nyosso, Komalbil Keita, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi 'Boban' na Felix Sunzu walikuwa miongoni mwa nyota wa kikosi cha kwanza cha Simba walioachwa nje katika siku ambayo taarifa zilishazagaa mitaani kuwa majina ya wakali kadhaa yalikabidhiwa na uongozi kwa kocha Patrick Liewig wakidaiwa kuwa wanaihujumu timu.
Wakiongozwa na Mrisho Ngassa, Nassoro Masoud 'Chollo' na Shomari Kapombe, kikosi kilichojaa yosso cha Simba kiliwashangaza wengi kwa magoli mawili ya haraka katika dakika tatu za majeruhi kabla ya mapumziko.
Ngassa aliifungia Simba goli la kuongoza katika dakika ya 45 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Shaaban Kado kufuatia shuti kali la Abdallah Seseme na Haruna Chanongo akaongeza la pili muda mfupi kabla refa Martin Saanya hajapuliza filimbi ya mapumziko.
Coastal walikianza kwa kasi kipindi cha pili na walihitaji dakika nne tu kupata goli lao kupitia Razak Khalfan aliyetumia vyema pasi ya Mohamed Athuman.
Tukio la huzuni kwa Simba ni kuumia kwa Jonas Mkude aliyelazimika kutolewa uwanjani kwa machela katika dakika ya 80 na nafasi yake kuchukuliwa na Mussa Mude.
Ushindi huo ulimaanisha kwamba Simba waliocheza mechi 19 wamejihakikishia kubaki katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 34, tatu juu ya Coastal, Mtibwa na Kagera Sugar zilizocheza mechi 20 kila moja.
Yanga inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 45, nane zaidi ya Azam inayowafuatia katika nafasi ya pili baada ya kila moja kucheza mechi 19.
Mfaransa Liewig aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi na kuwasifu wapinzani wao akisema ni timu nzuri.
"Ni jambo jema kuwa tumeshinda ingawa ni ushindi mwembamba. Tumetumia wachezaji vijana na wamefanya vizuri licha ya matatizo kadhaa ndani ya klabu," alisema Liewig ambaye timu yake huenda ikatozwa faini ya Sh. 300,000 kwa mujibu wa kanuni za ligi baada ya kuchelewa kuingia uwanjani jana huku taarifa zikidai kwamba walizuiwa hotelini wanakoishi kutokana deni la Sh. milioni 25.7.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba, Joseph Itang'are, alikiri timu yao kudaiwa fedha hizo na kuongeza kuwa wamekubaliana na uongozi wa hoteli kuwa watalipa fedha hizo.
Kocha wa Coastal, Hemed Morocco alisema timu yake ilipoteza umakini kueleka mwisho wa kipindi cha kwanza lakini walicheza vizuri katika kipindi cha pili.
Vikosi:
Simba:- Abel Dhaira, Nassoro Masoud 'Chollo', Miraji Adam, Hassan Khatib, Shomari Kapombe, Jonas Mkude/Mussa Mude (dk. 80), Amri Kiemba, Rashid Ismail, Abdallah Seseme, Haruna Chanongo na Mrisho Ngassa/Ramadhani Singano (dk. 73).
Coastal:- Shaaban Kado, Hamad Hamis, Abdi Banda, Mbwana Hamis/Castory Mumbara, Philip Mugenzi, Razak Khalfan, Daniel Lyanga, Mohamed Athumani, Deangelis da Silva/Mohamed Mtindi (dk.75), Selemani Kassim Salembe na Joseph Mahundi/Twaha Shekue (dk.46).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment