Mgombea Urais wa Kenya kupitia muungano wa Jubelee, Uhuru Kenyatta akipiga kura yake katika kituo huko Gatundu South.
Ahmed RajabToleo la 2846 Mar 2013
“UNAWAONA wale walio kwenye meza ile?” Aliniuliza sahibu yangu aliyekuwa amekaa ubavuni mwangu. Yeye ni mmoja wa washauri wakuu wa Uhuru Kenyatta, kiongozi wa chama cha The National Alliance (TNA) cha Kenya na mgombea urais kwa tiketi ya Muungano wa Jubilee Alliance…
Niliitupia jicho hiyo meza na kuwaona Wakenya kama wanne au watano hivi. Walikuwa vijana kila mmoja akiwa na umri usiopindukia miaka 50.
“Ukijumlisha utajiri wao utapata kama shilingi bilioni 15 hivi kama si zaidi,” aliongeza kunambia. Kumbe walikuwa miongoni mwa waliosaidia kuigharimia kampeni ya Uhuru ya kuuwania urais wa Kenya. Uhuru ni mtoto wa mzee Jomo Kenyatta, rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya. Ilikuwa usiku wa manane Jumamosi iliyopita na tulikuwa kwenye hafla katika klabu moja maarufu jijini Nairobi tulikoalikwa na mmoja wa hao wafadhili wa Uhuru. Hafla hiyo ilikuwa ni ya kusherehekea kumalizika kwa kampeni za Muungano wa Jubilee.Vigogo vya TNA, chama chake Uhuru, walihudhuria akiwemo Ferdinand Waititu, mwanasiasa mwenye sifa ya kuwa na machachari na aliyepigania ugavana wa Nairobi.
Waititu, ambaye huenda akashindwa kuunyakua ugavana, alikuwa hoi kwa uchovu. Alikuja baada ya kumalizika mkutano wa mwisho wa hadhara wa kampeni ya Jubilee uliofanyika jijini Nairobi. Waititu alikuwa mmoja wa waandaaji wakuu wa mkutano huo uliothibitisha jinsi Muungano wa Jubilee ulivyokuwa umejiandaa.
Hadi sasa gazeti hili la Raia Mwema linapoingia mitamboni bado mshindi wa uchaguzi wa urais wa Kenya hajulikani rasmi. Hata hivyo, matokeo yasio rasmi yanaonyesha kuwa Uhuru ndiye mwenye kuongoza akifuatiwa na Raila Odinga, kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) na wa Muungano wa CORD.
Uhuru amefanya kazi kubwa sana kufika hapa . Leo yeye siye tena yule kijana aliyelazimishwa kujitosa katika siasa na kuwa chini ya kivuli cha rais mstaafu Daniel arap Moi alipofika, Wala Uhuru huyu si tena mwanasiasa mwanagenzi aliyekuwa na haya na aliyekuwa hajui kufungua mdomo kuhutubia umati wa watu. Kweli Uhuru ni mtoto wa Mzee Kenyatta lakini si tena mtoto wa Mzee. Yeye mwenyewe sasa ndiye Mzee.
Mpinzani wake mkubwa Raila ni mtoto wa mzee Oginga Odinga aliyekuwa makamu wa rais wa kwanza wa Kenya chini ya Kenyatta na baadaye akawa mkuu wa upinzani.
Hivyo, wagombea wakuu wa urais wa Kenya wote ni ‘watoto wa watu.’ Wamezaliwa katika ulwa na katika familia za kisiasa. Bila ya shaka kuna kuzidiana na kwa hili Uhuru amemzidi Raila lakini wote wawili ni matajiri na wanahusika na biashara kubwakubwa.
Kuna dhana kwamba Raila ni mjamaa lakini hiyo ni dhana tu. Anamiliki makampuni makubwa makubwa au ana hisa katika makampuni hayo na amewahi kukumbwa na kashfa za ufisadi.
Labda anafikiriwa kuwa mjamaa zaidi kwa vile yeye ni mtoto wa Oginga Odinga, aliyekuwa mjamaa, au labda kwa sababu alisomea uhandisi Ujerumani ya Mashariki.
Mpinzani wake Uhuru alisomea siasa na uchumi Marekani kwenye chuo cha Amherst ambako mmoja wa waalimu wake alikuwa Abdulrahman Babu, waziri wa zamani wa Tanzania aliyekuwa akifuata itikadi za Kimarx.
Uhuru alizoeana sana na Babu na akipenda kumtembelea mwalimu wake nyumbani kwake ili ale pilau na chapati alizokuwa akizitamani Marekani.
Kiitikadi hakuna tofauti kubwa za kimsingi kati ya siasa na sera za Raila na Uhuru. Hayo yalionekana wazi wakati wa midahalo miwili ya wagombea urais iliyofanywa kabla ya uchaguzi.
Midahalo hilo pia ilidhihirisha mengine yaliyomponza Raila na kumjenga Uhuru. Raila akionekana kama akibaniabania mambo, akisitasita na kwamba hakua mkweli. Uhuru, kwa upande mwingine, akionekana kuwa ni mwanasiasa anayejiamini na aliyekuwa akijua anasema nini.
Uhuru alizivaa siasa bila ya kutaka. Moi ndiye aliyemshawishi ajitumbukize katika siasa. Mamake, Mama Ngina, na jamaa zake wengine walikuwa mwanzo wakimzuiazuia halafu mwishowe wakamruhusu awe mwanasiasa.
Mwanzoni mwanzoni Uhuru akionekana kama anaziogopa siasa lakini katika kipindi cha miaka mitano tangu umalizike uchaguzi uliopita mwana huyu wa Jomo amepevuka. Amethibitisha kwamba anacho kipaji cha kuongoza.
Sidhani kama ni bahati nasibu iliyomfanya awe hivyo; naamini amezicheza vizuri karata zake au amezicheza kama alivyoambiwa azicheze na washauri wake.
Kama miezi minane hivi iliyopita mbunge mmoja wa bunge lililopita akimlinganisha Uhuru na kiongozi mwingine wa kisiasa wa Kenya aliniambia: “Uhuru amebadilika. Anatimiza ahadi. Akisema atafanya kitu basi hufanya.”
Katika kuupanga mkakati wa kampeni yake ya urais Uhuru akiamini kwamba kama atashinda katika uchaguzi huu wa 2013 basi lazima ashinde katika duru ya kwanza. La sivyo, huenda akaja akajikwaa.
Kama uchaguzi utaingia duru ya pili basi Uhuru huenda akakabiliwa na kizingiti kikiwa katika umbo la Musalia Mudavadi. Wafuasi wa Mudavadi wanaweza kuhamia kwenye kambi ya Raila na kumpa kiongozi huyo wa ODM kura zao na hivyo kumwezesha aibuke mshindi wa uchaguzi wa urais.
Kwa hivyo mbinu kubwa ya kwanza aliyoitumia Uhuru na Muungano wake wa Jubilee katika siku za mwisho mwisho za kampeni ilikuwa kujiimarisha katika yale maeneo ambako wako dhaifu na kuhakikisha kwamba wanaongeza idadi ya wataowapigia kura.
Mbinu ya pili ilikuwa kuhakikisha kwamba wafuasi wao wanajitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura tarehe 4 Machi.
Njia waliyotumia ni kuzifanya kamati maalumu za mashinani za vyama vilivyo katika Muungano wa Jubilee ziwe zinashirikiana katika kaunti zote na kuwahimiza wafuasi wao wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura. Kila kamati ilipewa idadi maalumu ya wapiga kura iliyotakiwa iwapate na kuwaingiza kwenye ‘kapu la Jubilee’.
Mbinu nyingine iliyotumiwa na Muungano wa Jubilee ni kuwatumia wakuu wa kidini na viongozi wengine wa jamii wawashawishi wafuasi wa Jubilee wasusie kunywa pombe kwa muda wa angalau siku mbili kabla ya siku ya kupiga kura.
Muungano wa CORD wenye kuongozwa Raila ulichukulia mambo kiuzembezembe. Wao wakitaraji kwamba umaarufu wa Raila utatosha kumhakikishia ushindi.
Kwa kweli Raila ana umaarufu mkubwa na kuna wengi nchini wenye kumpenda lakini kile ambacho yeye au chama chake ilichofanya na ambacho Uhuru na chama chake hakikufanya ni kuwachagulia wananchi nani wawe wagombea wao wa nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi huu.
Tukiziacha kadhia za uteuzi wa kaka yake Obura Odinga na dada yake Ruth Odinga kuwania nyadhifa za ugavana na za unaibu wa gavana Raila hakuingilia kati kuzuia uteuzi wa James Orengo na Profesa Peter Anyang’Nyong’o ijapokuwa wote walikataliwa mashinani na wafuasi wa ODM wakati wa kura za kuwateua watetezi.
Siku chache kabla ya upigaji kura Uhuru alichukua hatua iliyozidi kumjenga ndani na nje ya TNA pale wabunge wa zamani Gideon Mbuvi (maarufu Sonko) na Rachael Shebesh walipoanza kumwandama mwenzao Waititu na kumpigia debe mshindani wake.
Uhuru aliingilia kati kwa haraka na kuwaamrisha Sonko na Shebesh kwamba lazima wamuunge mkono Waititu ambaye ni mwanachama mwenzao wa TNA.
Kwa kufanya hivyo, Uhuru alionyesha kwamba yeye ndiye kiongozi wa TNA, ndiye mwenye kukidhibiti chama na lazima asikilizwe. Pia alionyesha kuwa ni mtu mwenye kuweza kukata maamuzi ya haraka.
Kwa hakika Uhuru aliwashangaza wengi kwa namna alivyounda chama chake cha TNA kwa kasi kubwa na wakati huohuo kuweza kukidhibiti na kukifanya kiwe chama chenye nidhamu ya hali ya juu. Na hiki ni chama ambacho Uhuru alikiunda dakika za mwisho za mchakato wa kuelekea siku ya upigaji kura.
Kenya ni nchi yenye maajabu yake. Sikupata kushuhudia popote duniani mtu akitangaza nia ya kuwania urais halafu baadaye ndo akenda kutafuta chama cha kujiunga au akaunda chama chake kipya, tena katika muda wa miezi tu kabla ya uchaguzi.
Uhuru alifanya hivyo. Na siku aliyokizindua chama chake alikizindua kwa mbwembwe na shamrashamra ambazo hazikuwahi kabla kuonekana katika siasa za Kenya. Bila ya shaka fedha zilifanya kazi. Na Uhuru hana ukosefu wa ngwenje. Alizitumia zake na za wafadhili wake.
Jingine alilolifanya Uhuru ni kuwa makini na mwangalifu katika kuchagua nani na nani watashirikiana naye. Alimpiga chenga Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka na akamng’ang’ania William Ruto, kiongozi wa chama cha United Republican Party (URP), awe mwenza wake katika uchaguzi wa urais.
Ruto na Uhuru wote wanakabiliwa na mashtaka ya jinai mbele ya mahakama ya ICC huko Hague kutokana na vurugu na mauaji ya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.
Wawili hao wanaojulikana kwa ufupi kama UhuRuto wanaonekana kuwa ni wenza waliokinaiana. Ni vijana walioshikamana na waliowavutia vijana wengi wa Keya wawaunge mkono.
Tangu Uhuru na Ruto wakubaliane mkakati wa kuungana na kujipatia ushindi wamekuwa mbioni kujiimarisha mashinani na mijini. Muungano wao wa Jubilee tangu ubuniwe ulionekana kuwa imara na ukizidi kung’ara.
Tatizo kubwa litaloukabili ushindi wao ni kesi inayowakabili Hague ingawa kwa upande mmoja kesi hiyo pia iliwajenga kwa wapigaji kura.
Wakenya wengi kwa jumla hawakufurahishwa na matamshi ya Kofi Annan, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, pamoja na yale ya Balozi wa Uingereza nchini Kenya Dakta Christian Turner na ya Johnnie Carson, waziri mdogo wa Marekani anayehusika na mambo ya Afrika yaliokuwa yakiwatahadharisha Wakenya wasimchague Uhuru na Ruto.
Matamshi hayo yalitafsiriwa kuwa ni njama ya kuwataka Wakenya wamchague Raila badala ya Uhuru. Yalionekana kuwa ni mfano mwingine wa ukoloni mamboleo, wa utundu wa mataifa ya Magharibi wa kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi za Kiafrika. Annan pamoja na serikali za Uingereza na Marekani ziliikana tafsiri hiyo.
Wiki ijayo tukijaaliwa tutaangalia kwa nanma gani mashtaka ya ICC yatavyoweza kuuathiri urais wa Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.
No comments:
Post a Comment